Thursday, December 3, 2020

Mahakama mkoani Manyara imetoa amri kutaifishwa gramu 46ya Madini ya Tanzanite.

*******************************************

Na John Walter-Manyara

Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Manyara katika kesi ya Uhujumu Uchumi  namba 7/2020 imemuamuru Raymond Alex Ngowi @Tarimo kulipa faini ya shilingi laki moja au kutumikia

kifungo cha miezi 12 jela kwa kosa la kupatikana na madini bila kibali.

Hata hivyo mshtakiwa huyo amelipa Kiasi cha Shilingi 863,856.613 kama fidia kwa serikali.

Mwendesha Mashtaka Wakili wa serikali Mwandamizi Mutalemwa Kishenyi,  alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo Septemba 16,2020 eneo Tengefu la Ukuta wa Mirerani uliopo wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara akiwa na madini ya Tanzanite aliyoyaficha sehemu zake za siri.

Akisoma shauri hilo  leo Desemba 3,2020 Mheshimiwa Saimon Kobelo Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mfawidhi wa Mahakama ya mkoa wa Manyara alisema mtuhumiwa alikiri kosa na mahakama imemtia hatiani na kumuamuru kulipa faini  au kutumikia kifungo.

Mtuhumiwa alikuwa anakabiliwa na Makosa matatu, kuongoza genge la uhalifu chini ya sheria ya uhujumu uchumi, Kupatikana na madini bila kibali pamoja na utakatishaji fedha.

Awali mshtakiwa aliandika barua kwenda kwa Mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kuomba kukiri makosa yake ambapo aliridhia ombi hilo na leo Desemba 3,2020 mshtakiwa alisomewa kosa la kupatikana na Madini ya Tanzanite bila kuwa na Kibali ambapo  yalipofanyiwa tathmini yaligundulika kuwa na Gramu 46 yenye thamani ya shilingi Milioni 8,638,566.13  ambapo  mahakama imemuru kuyataifisha.

Katika kesi hiyo Upande wa mashtaka uliwakilishwa na wakili wa serikali Mwandamizi Mutalemwa Kishenyi akisaidiana na mawakili wa serikali Petro Ngassa na Rhoida Kisinga.

Kishenyi aliwataka wananchi wafuate sharia,miongozo na kanuni zinazoongoza biashara ya madini ili kuepuka kukumbana na mikono ya sharia.

Attachments area

 

No comments :

Post a Comment