Tuesday, December 8, 2020

MAGONJWA YA MLIPUKO NA KUAMBUKIZA BADO NI CHANGAMOTO KUBWA NCHINI

 Mratibu wa dhana ya Afya moja katika ofisi ya Waziri Mkuu  Harrison Chinyuka  akifungua mkutano mkuu wa 37 na Kongamano la Kisayansi la Chama cha Wataaamu wa Afya ya Jamii Tanzania (TPHA)  jijini Arusha jana,
Mwenyekiti wa chama hicho Dkt. Philbert Nyinondi akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo.
Mwenyekiti Mteule wa TPHA Dkt. Mariam Ongara akitoa shukrani kwa mgeni rasmi mara baada ya kufungua mkutano huo.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa  wa Arusha, Hergeberg Chitukuro akitoa salamu za mkoa huo kwa wajumbe wa mkutano huo.
Magreth Orumbe akiimba wimbo wa kumsifu Mungu mbele ya wajumbe kabla ya kutoa sala ya kuukabidhi mkutano na majadiliano hayo kwa Mungu kwa ajili ya siku zote nne watakazokuwa mkoani Arusha.
Prof.Robinson Mdegela kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) akichokoza mada kwenye kongamoano hilo kuhusu Hatari,Athari,Utayari na Jinsi ya kujilinda na Magonjwa ambukizi.
   Muwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni, Ritha Njau akiwasilisha mada ya pili kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 na changamoto zake.
Mwenyekiti wa chama TPHA  Dkt. Philbert Nyinondi akimtambulisha mwenyekiti Mteule Dkt.Dkt. Mariam Ongara (anayepungia mkono)

Wanachama na wajumbe wa mkutano na kongamano hilo wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa. 

 

Na. Calvin Gwabara, Arusha.

PAMOJA na
juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali, watafiti na wadau wengine wa maendeleo


katika kuyakabili magonjwa ambukizi na yasiyoambukizi na usugu wa vimelea vya
magonjwa lakini bado bado yameendelea kuwa
changamoto kubwa nchini.

Hayo
yamebainishwa na mratibu wa dhana ya afya moja katika ofisi ya Waziri Mkuu  Harrison Chinyuka wakati akifungua mkutano
mkuu wa 37 na Kongamano la Kisayansi la Chama cha wataaamu wa afya ya jamii
Tanzania (TPHA) jijini Arusha.

Alisema kuwa
Tanzania ni miongoni mwa nchi za uchumi wa kati lakini nayo ipo katika hatari
ya kupatwa na magonjwa hayo na kuathiri jamii hivyo mkutano huo ni muhimu sana
kujadili vichocheo vya magonjwa hayo na jinsi ya kuyakabili .

“Kumekuwa na
ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ambukiza katika jamii yetu kama vile magonjwa
ya moyo,kisukari,kansana mengineyo hivyo nina imani kuwa wataalamu mlio hapa
mnafahamu kuwa magonjwa haya yamekuwa tishio kubwa pia kwa jamii na kuhatarisha
uchumi wa nchi kwa ujumla tumieni nafasi hii kujadili kwa pamojajinsi ya
kuyakabili na athari zinazotokana na magonjwa haya” Alisisitiza Chinyuka.

Mratibu huyo
wa dhana ya afya moja katika ofisi ya Waziri Mkuu aliendelea kusema kuwa kwa
muda mrefu Tanzania imekuwa ikikabiliwa na matatizo mengi ya afya za
Binadamu,Wanyama na usugu wa vimelea vya magonjwa lakini Wizara,Idara na wakala
mbalimbali wa Serikali na za binafsi kila mmoja imekuwa ikipambana na namna
yake mmojammoja lakini ili kupata ufanisi mkubwa wa kuzuia,kujiandaa na
kuakabili lazima dhana ya afya moja itumike ili kuwa na nguvu ya pamoja.

“Dhana ya
afya moja inatumika zaidi kwa kuzingatia kuwa vimelea vingi vinavyosababisha
magonjwa kwa binadamu vinatokana na wanyama na kasi ya maambukizi inaongezeka
pale binadamu anapoingilia makazi ya wanyama hao katika mazingira yao bila
tahadhari” Aliongeza Chinyuka.

Alibainisha
kuwa hali ni hatarishi zaidi kwa bara la Afrika kwa kuzingatia kuwa bara hili
hususani sehemu zinazokaribia misitu mikubwa ya Kongo yenye wanyama wengi wa
aina mbalimbali na hivyo kuwa chanzo kikubwa cha magonjwa ya milipuko kama vile
Ebola,Homa ya bonde la Ufa,Marburg na mengineyo.

Akizungumza
kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo wa kisayansi, Mwenyekiti
wa chama hicho Dkt. Philbert Nyinondi alisema kuwa chama hicho kiliundwa mwaka
1980 kwa lengo la kufanikisha vita dhidi ya
adui maradhi dira ambayo bado wanaendelea kuiishi.

Aliongeza
kuwa ili kuhakikisha wanajenga taifa na dunia iliyo salama chama hicho
kimeshiriki kikamilifu kutoa elimu kwa Umma,kushauri sera,sheria na kanuni bora
katika kuimarisha afya ya jamii,kushirikiana na Serikali na washirika wa
maendeleo katika utekelezaji wa mipango ya Serikali inayolenga kuimarisha afya
ya jamii pamoja na kuandaa majukwaa ya wadau na kutoa fursa kwao kutoa mchango
wa kimawazo na kimkakati kuimarisha afya.

“Tunajivunia
miaka 40 ya utendaji kazi wa chama chetu bila kuwa na migongano na serikali za
awamu zote tano  na sisi wana TPHA
tunaungana na Rais wetu Dkt. John  Magufuli katika nia yake ya kuimarisha
na kujenga miundombinu mipya ya afya kwani imeimarisha huduma za afya nchini” alibainisha Dkt. Nyinondi.

Alisema
mkutano huo unatoa fursa kwa wadau kushiriki kikamilifu kutathimini mafanikio
makubwa waliyoyapata,kujipanga na kuiandaa jamii kwa magonjwa ya mlipuko na
yanayoibuka na kuishauri Serikali na ulimwengu namna bora ya kukabiliana
na  milipuko taraji na siayotarajiwa bila
kuathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya watu.

Akitoa
shukrani kwa mgeni rasmi Katibu wa TPHA Dkt. Mariam Ongara alisema wao kama chama watayafanyia kazi yale yote yaliyoshauriwa na mgeni rasmi hususani dhana
ya afya moja  ili kuweza kuingeza tija
katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na
yasiyo ya kuambukizakwa maslahi mapana ya jamii na Taifa.

Alibainisha
kuwa wao kama chama wanafanya kazi kwa kufuata miongozo na taratibu zote za
serikali na zinazosimamia masuala ya afya na kuisaidia serikali kufikia malengo
yake kwa kufanya tafiti na kushauri njia bora ambazo zinafaa kutumika katika
kuimarisha afya za watu.

Akiwasilisha
mada ya kwanza iliyobeba mkutano huo Profesa. Robinson Mdegela kutoka Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  alisema kuwa awali ilionekana tatizo la magonjwa ya
kuambukizwa na mlipuko ni ya Afrika,China na kwenye maeneo ya misitu ya
Amazon  pekee lakini sasa ni dunia nzima
na hii ni kutokana na kurahisishwa sana kwa njia za usafiri na hivyo kusamnbaza
magonjwa hayo kirahisi.

Prof.Mdegela
alisema tafiti zinaonyesha magonjwa hayo mengi ya milipuko na kuambukizwa
yanatokana na Wanyama ambao sio binadamu kama vile nyani,Sokwe na Ngedere, Popo
na Panya wanyama ambao wapo kila kona ya Tanzania na jamii inaishi nao wengine
bila hata kuchukua tahadhari.

Alisema kuna
mambo kadhaa ya kufanya ikiwemo kuangalia kama utaalamu na taaluma hiyo ipo
nchini ya kutambua magonjwa hayo na kisha kujulisha umma uwepo wa magonjwa hayo
kwani kuna maeneo ambayo wasambazaji wa magonjwa hayo ni kitoweo kwao kama vile panya.
 

Mkutano na
Kongamano hilo la kisayansi la chama Cha Wataalamu wa Afya ya Jamii Tanzania (TPHA), umebeba Mada isemayo “Magonjwa ambukizi yanayojitokeza na 
yale
yanayojirudia: Hatari,Athari,Utayari na Jinsi ya Kuyakabili”
 

 

No comments :

Post a Comment