Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwa katika zoezi la
kuwapigia simu wamiliki wa ardhi katika jiji la Dar es Salaam
walioshindwa kuzifuata hati zao zilizokamilika kwenye ofisi za ardhi za
mikoa. Kushoto ni Msajili wa Hati Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam Juma
Ligela. Jumla ya Hati 20,752 hazijachukuliwa na wamiliki wake katika
ofisi za ardhi za mikoa.
Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akiwa katika zoezi la
kuwapigia simu wamiliki wa ardhi katika jiji la Dar es Salaam
walioshindwa kuzifuata hati zao zilizokamilika katika ofisi za ardhi za
mikoa. Kushoto ni Msajili wa Hati Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam Juma
Ligela. Jumla ya Hati 20,752 hazijachukuliwa na wamiliki wake katika
ofisi za ardhi za mikoa.
Msajili wa Hati Msaidizi mkoa wa Pwani Rachel Kilasi akimkabidhi moja ya Hati za Ardhi 128 za Shirika la Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma ( PSSSF) kwa Afisa Milki wa Shirika hilo Hamidu Rashid Mkama alipoitikia wito wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuzifuata Hati baada ya kupigiwa simu. Jumla ya Hati 20,752 hazijachukuliwa na wamiliki wake katika ofisi za ardhi za mikoa.( Picha na Munir Shemweta WIZARA YA ARDHI).
*******************************************
Na Munir Shemweta, DAR ES SALAAM
Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameanza kazi ya kuwatafuta
wamiliki wa ardhi walioshindwa kuchukua hati zao kwenye ofisi za Ardhi
za mikoa kwa kuwapigia simu wamiliki wa jiji la Dar es Salaam na
kuwataka kuzifuata hati zao katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia
Desemba 29, 2020.
Jumla ya Hati 20,752
hazijachukuliwa katika ofisi za ardhi kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara
na hivyo kufanya kuwepo mlundikano wa hati katika ofisi za Wasajili wa
Hati Wasaidizi katika Ofisi za Ardhi za mikoa.
Miongoni mwa wamiliki
wa ardhi waliopigiwa simu ni kutoka maeneo ya Salasala, Kibada na Mbezi
Msakuzi Dar es Salaam ambapo baadhi yao walionesha kushangazwa na
uamuzi wa Waziri Lukuvi kuwapigia simu na kuielezea hatua hiyo kama
ishara ya kuonesha Wizara ya Ardhi imejipanga kuwahudumia wananchi.
Akitaja idadi ya Hati
katika mikoa wakati wa zoezi la kuwapigia simu wamiliki hao leo tarehe
29 Desemba 2020 Lukuvi alisema mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaoongoza
kwa kuwa na idadi kubwa ya Hati 5,218 ambazo wahusika wameshindwa
kuzichukua ukifuatiwa na mkoa wa Pwani wenye Hati 3,341 na Dodoma Hati
3,076.
Mikoa mingine na
idadi ya Hati katika mabano ni Singida (201), Morogoro (1,345), Mtwara
(470), Lindi (235), Ruvuma (118), Kilimanjaro (224), Manyara (143),
Arusha (135), Tanga (711), Mbeya (266), Iringa (137), Njombe (45), Rukwa
(23), Songwe (68), Kigoma (555), Tabora (626), Katavi (261), Mwanza
(1,532), Geita (251), Simiyu (213), Kagera (382), Shinyanga (817) na
Mara (559).
Lukuvi amewahimiza
wananchi kujitokeza kuchukua hati kwenye ofisi za ardhi za mikoa na
kusisitiza kuwa, hivi sasa wamiliki wamerahisishiwa uchukuaji hati
katika ofisi za ardhi za mikoa tofauti na huko nyuma ambapo walilazimika
kusafiri mpaka ofisi za kanda zilizohusisha zaidi ya mikoa miwili.
Alisema, mmiliki
yoyote wa ardhi anayejua amelipia kodi pamoja na tozo zote ajue kwamba
ni miongoni mwa watu ambao hati yake imekamilishwa na iko katika ofisi
ya Msajili wa Hati.
“Tafadhali kama una
hati na kiwanja kilichopimwa na umelipa kodi na tozo zote za
kutayarishiwa hati nenda ofisi ya ardhi mkoa umtafute msajili wa hati
ili uthibitishe na uchukue hati, tunataka zoezi hili liishe haraka kila
mwenye hati afuate mwenyewe na kama kuna kodi anadaiwa alipe” alisema
Lukuvi.
Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka makamishna wote Wasaidizi wa
Ardhi katika mikoa kuhakikisha wanafuatilia katika kila wilaya na
kuangalia aliyemilikishwa kama hajachukua hati akachukue mwenyewe na
isiwe zaidi ya siku 30 kuanzia tarehe 29 Desemba 2020.
Katika hatua
nyingine, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
amewataka wamiliki wa ardhi wanaotaka kujenga kuhakikisha wanafuata
sheria na taratibu zote wakati wa kufanya ujenzi.
Lukuvi alisema,
sheria inamtaka mmiliki wa ardhi anayetaka kufanya ujenzi kupata kibali
kutoka halmashauri za miji, manispaa na majiji na kuongeza kuwa sheria
hiyo inakataza kufanya ujenzi bila kibali kutoka mamlaka husika.
” Naelekeza watendaji
wote wawe wa ardhi au mipango miji kuhakikisha sheria zinafuatwa kwa
kudhibiti ujenzi holela na sheria inakataza kabisa kujenga bila kupata
kibali kutoka katika mamlaka husika” alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi,
zoezi la urasimishaji linaloendelea sasa maeneo mbalimbali ni kwa
majengo yaliyojengwa tu na kusisitiza kuwa zoezi la urasimishaji isiwe
sehemu endelevu ya kuvunja sheria na kubainisha kuwa angetaka kuona
maeneo yote ya miji hasa Dodoma yanajengwa kwa kupatiwa kibali.
Aliwataka wataalamu
wote hasa waliopo halmashauri katika yale maeneo yaliyotangazwa kimji
kwa mujibu wa sheria wananchi wake waelimishwe kujenga katika viwanja
vilivyopangwa na kupimwa na wawe wamepatiwa vibali na mamlaka za
halmashauri husika.
” hatua zichukuliwe
kuzuia jambo hili tunataka miji endelevu ambayo wananchi wanaishi na
kujenga kwa mujibu wa sheria” alisema Lukuvi
No comments :
Post a Comment