Thursday, December 17, 2020

KIGOMA KUWA KINARA WA UZALISHAJI MICHIKICHI NCHINI-KUSAYA


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye (kulia) akisamiliana na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( kushoto) leo alipowasili Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kigoma kwa ziara ya kikazi kukagua shughuli za kilimo.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya ( kushoto) akisaini kitabu cha wageni alipowasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma leo kwa ziara ya kikazi. Kulia ni Mhe. Thobias Andengenye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ( kulia) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya leo mjini Kigoma ambapo Katibu Mkuu huyo ameanza ziara ya kikazi kukagua shuguli za kilimo.

Habari na picha na Wizara ya Kilimo

………………………………………………………………………………………….

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe.Thobias Andengenye amesema wamejipanga kuhakikisha agizo

la serikali la kuongeza uzalishaji michikichi nchini ambapo wakulima wameanza kupanda aina mpya ya miche ya Tenera yenye kutoa mafuta mengi.

Mhe. Andengenye amesema hayo leo (17.12.2020) wakati alipofanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya aliyepo Kigoma kwa ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa shughuli za kilimo.

“ Zao la michikichi ndio lenye upekee wa kuwafanya wakulima wa Kigoma kuwa na uchumi imara na uhakika wa kipato kutokana na malighafi hiyo ya kuzalisha mafuta ya kula kuhitajika nchini kwa wingi “ alisema Mkuu wa Mkoa Andengenye.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Kigoma aliotoa ombi kwa Wizara ya Kilimo kupitia Kituo cha Utafiti wa zao la Michikichi  (TARI) Kihinga na Wakala wa Mbegu (ASA) waongeze kasi ya kuzalisha miche bora ya michikichi aina ya Tenera na kuisambaza kwa wakulima kwenye wilaya zote za Kigoma.

“Halmashauri zetu zimejipanga kutekeleza agizo la serikali la kuongeza uzalishaji michikichi na mazao mengine ya biashara ikiwemo korosho ili wakulima wetu wawe na uhakika wa kipato hivyo wizara itusaidie kupata miche na mbegu bora na ziwafikie wakulima kwa gharama nafuu.” alisisitiza Mhe. Andengenye.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya alisema Wizara inaendelea kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kuhakikisha zao la michikichi linalimwa kote nchini ambapo hali ya hewa inafaa ili nchi ikabiliane na taitizo la upungufu wa mafuta ya kula.

Kusaya alibainisha mikakati ya wizara kuwa vituo vya utafiti vya TARI Kihinga na shamba la mbegu la ASA Bugaga vilivyopo Kigoma vitaendelea kuzalisha mbegu bora na miche ya michikichi na kuigawa kwa wakulima kwa gharama nafuu.

“Wizara ya Kilimo imejikita zaidi katika michikichi ili kuondoa upungufu wa mafuta na kuachana na utaratibu wa nchi kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi yanayogharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 443 kwa mwaka “ alisema Kusaya.

Katibu Mkuu huyo wa kilimo alitoa wito kwa uongozi wa mkoa wa Kigoma kuhamasisha halmashauri zake kupanda walau miche bora 100,000 ya michikichi bora ili mkoa huo ulio na hali nzuri ya hewa iongeze uzalishaji.

Wizara ya Kilimo inaendelea na jitihada za kuzalisha miche mingi zaidi na kuisambaza kwenye mikoa 17 nchini ambapo zao la michikichi linastawi vema.

Katika hatua nyingine Kusaya alitoa wito kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kuelekeza wataalam wa kilimo wa halmashauri zake kufuatilia na kujua maendeleo ya wakulima wote amabao wamegawiwa miche ya michikichi kujua maendeleo yao .

“Tunahitaji sensa ya wakulima wa michikichi Kigoma ikionesha idadi ya miche iliyopandwa na kiasi cha eneo la mkulima ili iwe rahisi kwa watafiti wetu wa TARI na Maafisa Ugani kuwafikia wakulima na kutoa huduma za kuboresha uzalishaji wa zao hilo nchini” alihitimisha Kusaya .

Katibu Mkuu Kusaya yupo mkoani Kigoma kwa ziara kikazi ya kukagua utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu kuhusu uzalishaji wa zao la michikichi pamoja na kuhamasisha kilimo cha mazao ya biashara ili kuinua hali za wakulima na kuchangia katika pato la Taifa na uchumi kaya.

Mwisho.

Imeandaliwa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

KIGOMA

 

No comments :

Post a Comment