Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.
KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia
Sekta ya Ujenzi, Mhandisi. Elius Mwakalinga Novemba 30, 2020 amefanya ziara na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam. Katika ziara hiyo Mhandisi. Mwakalinga amepitia na kuona maendeleo mbalimbali yanayoendelea katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kujiridhisha na utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa alipotembelea Oktoba 20, 2020.Akizungumza na Uongozi wa TBA ambao ni Wakandarasi na Washauri Elekezi wa mradi huo, Mhandisi. Mwakalinga amesema kuwa alipotembelea Oktoba 20, 2020 maendeleo ya mradi yalikuwa ni asilimia 81 lakini kwa sasa ujenzi huo umefikia kiwango cha asilimia 88. Vilevile ameipongeza TBA kwa kuzingatia maelekezo yake aliyoyatoa pamoja na kuonesha ubunifu kwa kujenga majengo ya kupokelea wageni, na majengo ya maduka ambayo yatatoa huduma kwa wakazi hao wa Magomeni Kota.
Aidha, ameagiza TBA kupitia Idara ya Miliki kuweka Afisa katika eneo la mradi huo kuanzia sasa kwa ajili ya kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wateja ambao wangependa kuuziwa au kupangishwa nyumba hizo na kufanya tathmini ambayo itasaidia kutambua mahitaji ya soko kwa nyumba nyingine zitakazojengwa mkabala na majengo ambayo yanaendelea kujengwa.
Pia ameongelea ubunifu unaoendelea katika mji wa Serikali awamu ya pili pamoja na ukarabati wa nyumba unaoendelea katika mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam.
Mradi wa ujenzi wa nyumba za Magomeni Kota utakapokamilika unatarajiwa kutoa makazi kwa kaya 656.
No comments :
Post a Comment