Wednesday, December 23, 2020

Fahamu uhusiano wa hatifungani za serikali na wastaafu wawekezaji

Central Bank of Tanzania in Background, with Tanzania Shilings in foreground

Na Christian Gaya

Wiki iliyopita tuliona ya kuwa hatifungani za serikali ambazo Benki Kuu ya Tanzania kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huuza hizo dhamana za serikali ikiwa ni njia ya kukopa fedha kutoka kwa ama taasisi au mwananchi mmoja mmoja.

Kwa hufanya hivyo huwa inakuwa ni fursa nzuri kwa wastaafu na kwa wawekezaji wengine hasa kwa wastaafu wanaohitaji kuwekeza fedha na kupata faida bila kutumia nguvu nyingi au kuwekeza bila kupata hasara ukilinganisha na umri waliokuwa nao.

Ingawa taasisi za fedha mbalimbali kama vile mabenki ni miongoni mwa taasisi zinazowekeza mara kwa mara kwenye hatifungani za Serikali ukilinganisha na wastaafu na wawekezaji wengine.

Wiki hii tunaangalia mwenendo wa hizi hatifungani serikali za au dhamana za serikali kwa ujumla. Ieleweke ya kuwa baadhi ya taasisi nyingine za fedha zinazowekeza mara kwa mara kwenye hatifungani za serikali ni pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo hutokana na michango ya wanachama mbalimbali kwa ajili ya mafao ya muda mrefu kama vile fao la kustaafu na mafao ya muda mfupi kama vile fao la uzazi, ikiwemo na mifuko ya uwekezaji wa pamoja, mashirika ya bima na makampuni mengine hasa makubwa.

Hapa ijulikane ya kuwa riba ya hatifungani za serikali kwa upande mwingine ni gharama kwa serikali, hivyo kushuka kwake ni inakuwa ni habari njema kwa wastaafu wawekezaji na kwa wawekezaji wengine. Lakini kumbuka ya kuwa kwa wastaafu wawekezaji na kwa wawekezaji wengine kushuka kwa bei za hatifungani za Serikali za muda mrefu na za muda mfupi vile vile kunapunguza faida.

Hapa ikumbukwe ya kuwa kwa taasisi za fedha kama vile mabenki, hatifungani za Serikali hasa za muda mfupi ni dhamana zenye ukwasi mkubwa, na dhamana hii inatumika kiuwekezaji, yaani kama chanzo cha mapato. 

Lakini kwa wakati mwingine inaweza kutumika kwa matumizi mengine kama vile kuwekea rehani kwa ajili ya kukopea na pia inaweza kutumika kama dhamana ya dharura wakati wa unapokuwa na uhitaji mkubwa wa fedha tasilimu.

Mpaka sasa tulipofikia tunajua ya kuwa dhamana za serikali au hatifungani za serikali huuzwa kupitia minada ambapo kila mstaafu mwekezaji au mwekezaji yeyote huwasilisha zabuni inayoonesha riba ambayo yuko tayari kulipa kulingana na mahitaji na uwezo wake.

Na kwamba maombi ya wawekezaji, kwa kawaida hushindanishwa kufuatana na kiasi ambacho serikali imepanga kukopa kwa mnada husika. Kwa kawaida siku hiyo wawekezaji wakiwa wengi na ikatokea ya kuwa wanahitaji kiasi kikubwa cha fedha kulingana na mahitaji ya kukopa ya serikali, hufanya riba za hatifungani za serikali kushuka chini, na kwa upande mwingine siku hiyo wakija wanunuzi wachache ushindani unakuwa mdogo na hatimaye kusababisha serikali kuuza dhamana zake kwa riba kubwa.

Hapa ifahamike ya kuwa mara nyingi mabenki yakiwa na ukwasi wa kutosha baada ya kukopesha hupendelea kuwekeza katika hatifungani za serikali za muda mfupi, tofauti na taasisi nyingine kama vile mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii kama vile ZSSF, NSSF, na PSSSF ambayo hupendelea zaidi hati fungani za muda mrefu.

Unafikiri kwa nini inakuwa hivi, hii ni kwa sababu mabenki kwa kawaida yanatakiwa yawe na ukwasi mara kwa mara ili kuwezesha watu walioweka amana zao wazipate kwa wakati wanapokuja kuzitoa kwa mhitaji yao ya kila siku.

Mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii hupendelea kuwekeza kwenye dhamana za muda mrefu yaani kwenye hatifungani za muda mrefu kwa sababu wateja wao wengi huweka pesa wakitarajia kuzitoa baada ya kufikia mwaka wa kustaafu kwa hiyari miaka 55 au kwa lazima yaani miaka 60.

Pamoja na hayo yote hapa ifahamike wazi ya kuwa mabenki yakiwekeza zaidi kwenye dhamana za serikali au kwenye hatifungani za serikali yanaweza kusababisha kushuka kwa riba. Kwa maana hiyo ni kwamba kushuka kwa riba mara nyingi kunasababisha kushuka kwa mapato ya benki yatokanayo na riba na hatimaye faida za mabenki kupungua.

Kumbuka ya kuwa, pia kushuka kwa riba kunaweza kusababisha mabenki na hata wawekezaji wengine kuamua kuwekeza kwenye fursa zingine.

Hata hivyo mara nyingi mabenki hutumia fursa za kuwekeza kwa kukopesha benki zingine kwa kupitia masoko ya fedha baina ya mabenki.

Mabenki mengi hushiriki kwenye soko la dhamana za muda mfupi kwa lengo la kuwekeza hivyo kwa kitendo hiki kunaashiria ya kwamba kuna ukwasi baina ya mabenki.

Hivyo ifahamike wazi ya kuwa ukwasi kwa mabenki ni jambo jema kiuchumi ili mabenki yaweze kuwekeza kwa kukopesha kwenye miradi mbalimbali inayochochea maendeleo ya nchi.

Ingawa pamoja na kwamba ushiriki wa mabenki kununua hatifungani za Serikali za muda mfupi kwa kiwango kikubwa kunaashiria ukwasi wa kutosha, pia kunaweza kuashiria kukosekana sehemu nyingine za kuwekeza mathalani mikopo kutoka kwa wateja wao wa mabenki.

Chukulia kwa mfano, ikiwa mikopo mingi hailipiki, na kumbuka ya kuwa kwa kawaida mikopo ni chanzo kikuu cha mapato ya mabenki, uhai na afya na ya uendelevu wa mabenki, ili kuepuka hasara mabenki yatachagua kwenda kuwekeza kwenye dhamana za Serikali ili kuepuka hasara, na hivyo basi kuchangia ushukaji wa riba inayotolewa kwa kuwekeza kwenye dhamana za serikali.

Hivyo mara nyingi, kushuka na kupanda kwa bei ya dhamana za serikali kunaweza kutazamwa kwa namna mbili. Namna ya kwanza ni kuwepo kwa ukwasi wa kutosha kwenye masoko lakini pia kukosekana kwa sehemu nyingine za kuwekeza zenye athari ndogo.

Hapa ijulikane ya kuwa, bei za dhamana za serikali zinaweza kuwa na athari pia hata kwa wawekezaji wengine. Hebu chukulia kwa mfano, mifuko ya pensheni ya hifadhi ya jamii inapowekeza kwenye dhamana za serikali za muda mrefu zaidi, ambapo inategemea kupata faida kubwa ili iweze kulipa wanachama wake wanapofikia umri wa kustaafu.

Hata hivyo riba inaposhuka, faida pia hushuka na kuipunguzia taasisi ya aina hii ya hifadhi ya jamii, uwezo wa kulipa mafao na pensheni nzuri zaidi kwa wanachama na wastaafu wake.

Kumbuka ya kuwa mwanachama anapokaribia kustaafu mara nyingi hujawa na matumaini makubwa ya kupata pensheni ya kumtosha kupata mahitaji yote ya lazima na ya muhimu na familia yake, hivyo anapokuja kupewa pensheni ndogo huishia kukata tamaa na hatimaye kujawa na msongo wa mawazo makubwa.

Christian Gaya ni mwanzilishi wa kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni na kustaafu. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com na kwa habari zaidi za HakiPensheni unaweza kutembelea tovuti www.hakipensheni.co.tz  simu +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment