Monday, December 28, 2020

DKT. NDUGULILE AIPA TCRA MIEZI MITATU KUMALIZA CHANGAMOTO ZA VIFURUSHI NA BANDO KWA WANANCHI


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (katikati) akipata maelezo kuhusu makumbusho ya mawasiliano kutoka kwa Raphael Mwango, Afisa Makumbusho wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania wakati wa ziara yake kwenye taasisi hiyo, Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (hawapo pichani) kabla ya kumkaribisha Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile (anayesikiliza) kuzungumza wakati wa ziara yake ya kutembelea taasisi hiyo, Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo A. Mathew (wa tatu kushoto) akiuliza utendaji kazi wa mitambo ya kufuatilia matumizi ya masafa kwa Jumanne Ikuja (wa kwanza kushoto), Mhandisi wa masafa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, wakati wa ziara ya kutembelea taasisi hiyo, Dar es Salaam. Anayesikiliza wa pili kushoto ni Waziri wa Wizara hiyo, Dkt.Faustine Ndugulile.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (wa pili kushoto) na Naibu Waziri wake, Mhandisi Kundo A. Mathew (wa tatu kushoto) wakimsikiliza Mhandisi Jumanne Ikuja akiwaeleza kuhusu gari lenye mitambo maalumu linalofuatilia matumizi ya masafa wakati wa ziara yao Mamlaka ya mawasiliano Tanzania, Dar es Salaam. Wa nne kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Mhandisi James Kilaba

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo kwa Menejimenti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (hawapo pichani), wakati alipotembelea taasisi hiyo, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Mhandisi James Kilaba (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (wa tatu kulia) na Naibu Waziri wake, Mhandisi Kundo A. Mathew (wa pili kulia) kuhusu mifumo ya TEHAMA inayotengenezwa na taasisi hiyo. Wa nne kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

*********************************************

  • Aipongeza kwa Kazi Nzuri ya Kudhibiti Sekta
  • Asema Wanaweza Kuboresha Zaidi ili Kuchangia Pato la Taifa

Na Prisca Ulomi, WMTH

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.Faustine Ndugulile ameipa Mamlaka ya

Mawasiliano Tanzania (TCRA) miezi mitatu kumaliza changamoto za bando na vifurushi zinazotolewa na kampuni za simu za mkononi kwa wananchi

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ziara yake alipotembelea TCRA ikiwa ni moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kufahamiana, kutambua majukumu yao na kuzungumza na Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa taasisi hiyo ili kuwa na uelewa wa pamoja na kushirikiana kwa kufanya kazi kwa pamoja katika kuhudumia wananchi kuelekea Mapinduzi ya Nne ya Viwanda na kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi wa kidijitali

Ameongeza kuwa TCRA ishughulikie malalamiko ya wananchi kwa kuwa wananchi hawana imani na vifurushi na bando, na kuwe na mfumo wa kuhakiki gharama halisi za mawasiliano kuendana na fedha aliyotoa mwananchi na kuwe na namba ya bure ambayo wananchi watapiga ili kuwasilisha malalamiko yao ili kuwawezesha wananchi kuongeza imani yao kwa Serikali

Amesisitiza kuwa ni heri tufanye maamuzi mabaya kuliko kutokufanya maamuzi na amewataka washirikiane na Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC) kumaliza changamoto hiyo kwa kuwa watanzania sio wajinga, anataka aone kapata shilingi moja anaitumia shilingi moja yake kupiga simu

Pia, amehimiza wahakikishe kuwa chaneli tano za bure za runinga zinaonekana hata baada ya muda wa kulipia kumalizika kwa kuwa chaneli hizo hazionekani kwenye baadhi ya ving’amuzi 

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew ameipongeza TCRA kwa kutengeneza mifumo ya TEHAMA, kutambua changamoto zilizopo na imejipanga kuzifanyia kazi kwa kuwa lazima TEHAMA ichukue nafasi yake na itufikishe watanzania tunakotaka kwenda

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.Zainab Chaula amewataka wafanyakazi wa TCRA kujiongeza na kujituma zaidi badala ya kusubiri maagizo na maelekezo kwa kuwa wao ni wataalamu, hivyo washirikiane kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa wanaendelea kuwahudumia watoa huduma na watumiaji wa huduma za mawasiliano

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amekiri uwepo wa changamoto za bando na vifurushi na ameahidi kuzifanyia kazi kwa kuwa TEHAMA imeongeza mnyororo wa thamani kwenye sekta zote na imesogeza huduma mbali mbali viganjani

 

No comments :

Post a Comment