Thursday, December 10, 2020

DKT KIJAZI-WANANCHI MSIDANGANYIKE MAINI NA MAFUTA YA TEMBO SIO DAWA YA KANSA YA INI WALA KANSA YA KIZAZI

Dkt Allan Kijazi,Kamishna wa uhifadhi wa tanapa na naibu katibu mkuu wa Wizara ya maliasili na utalii alifungua mkutano wa TANAPA na wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Kamishna msaidizi mwandamizi wa shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA)Pascal Shelutete akitoa mada inayohusu mikakati ya TANAPA kuhusu utekelezaji wa ilani ya chama tawala kwenye kikao kazi cha TANAPA na wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Baadhi ya wahariri na waandishi waandamizi kutoka vyombo mbalimbali nchini wakifuatilia mada zinazotolewa katika kikao cha TANAPA na wahariri.

******************************************

Na Editha Karlo,Dodoma

KAMISHNA wa uhifadhi shirika la hifadhi la Taifa(TANAPA)na naibu katibu mkuu wa Wizara ya maliasili na utalii Dkt Allan Kijazi amesema kuna mbinu mpya ya ujangili wa kuua tembo

imeibuka kwa kudanganya wananchi kuwa maini na mafuta ya tembo ni dawa kansa ya ini na kansa ya kizazi pamoja na vidonda vya tumbo.

Kijazi ameyasema hayo kwenye hotuba yake katika ufunguzi wa mkutano wa tanapa na wahariri wa vyombo vya habari nchini.

Dkt Kijazi alisema kuwa shirika kwa kushirikiana na mikakati iliyowekwa imesaidia kupunguza wimbi la ujangili nchini kwa kiasi kikubwa.

Alisema majangili wamebuni mbinu mpya ya kuhakikidha tembo wanauliwa na kuibua wimbi jipya la ujangili wa tembo ambalo linahamasishwa na watu wachache wenye nia ya kuhamasisha wananchi na kuwajengea imani kuwa maini na mafuta ya tembo yanasaidia kuponya kansa ya ini,kansa ya kizazi kwa akina mama na vidonda vya tumbo.

Alisema kutokana na kuaminishwa huko baadhi ya wananchi wameanza kutumia mbinu za kuweka sumu kwenye maboga na misumari kwenye maeneo wanayopita tembo ili kuweza kupata maini na mafuta ya tembo.

“Lakini pia wanapowaua tembo hao,wananunua meno ya tembo hao,wanaofanya kampeni hizo wananunua meno ya tembo hao”alisema

Dkt Kijazi amewataka wananchi kuachana na imani potofu za kwamba mafuta ya tembo na maini yanatibu magonjwa hayo kwani hizo ni mbinu zinazotumika kuwadanganya wananchi ili wawatumir kufanikisha biashara yao ya meno ya tembo.

Alisema lengo lao ni kupata meno ya tembo kwani mafuta na maini ya tembi hayana soko lolote bali ni mbinu ya majangili kuhakikisha wanapata meno ya tembo.

“Nitoe rai kwa wananchi kwamba hakuna ushahidi wowote wa kitaalam unaonyesha kwa maini na mafuta ya tembo yanatibu magonjwa ya kansa ya ini,kansa ya kizazi kwa akina mama na vidonda vya tumbo natoa onyo hatutasita kumchukulia hatua mwananchi yoyote bila kujali uwezo wake au nafasi yake katika jamii”alisema Dkt Kijazi

Pia Dkt Kijazi amewataka wananchi kuacha tabia ya kuwinda wanyama wakidai ni kitoweo,matokeo yake wanageuza hifadhi kama sehemu ya biashara kwa kuuza nyama nje ya mipaka ya nchi.

Naye Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi wa shirika la hifadhi za Taifa(TANAPA) Pascal Shelutete alisema kuwa vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa katika kutangaza shirika pamoja na majukumu yake kwa jamii.

“Vyombo vya habari vimetoa mchango mkubwa katika kukuza utalii kwani vimeweza kutoa kwenye kufanikisha uwanja wa ndege wa Ruaha kuchaguliwa kuwa wa kwanza Afrika na wa pili duniani kuwa uwanja wenye mandhari nzuri kuliko viwanja vingine vyote Afrika na Duniani”alisema.

 

No comments :

Post a Comment