Haki
ya kupata taarifa nchini Tanzania imeainishwa, kusisitizwa na kulindwa
na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na
Sheria ya Kupata Taarifa ya mwaka 2016 na Kanuni zake. Kwa mujibu wa
sheria hizi, kila Mtanzania anayo haki ya kupokea na kutoa taarifa
zinazoathiri maisha yake ya kila siku.
Haki
ya kupata taarifa inahusisha uhuru wa raia kupata taarifa zenye maslahi
kwa umma kutoka wizara, idara na taasisi za umma. Taarifa zenye maslahi
kwa umma zinajumuisha taarifa kuhusu huduma mbalimbali za kijamii
zinazoathiri haki, ustawi na maendeleo ya raia katika maeneo ya utawala
bora, afya, elimu, miundombinu, na upatikanaji wa haki.
Ripoti
mbalimbali zinaonesha uwepo wa changamoto ya kutafuta na kupata taarifa
zenye maslahi kwa umma kutoka kwenye vyombo vya serikali na taasisi za
umma nchini Tanzania (MISA, 2020; MCT, 2019).
Tafiti
zilizofanyika zinaonyesha kwamba maombi ya wananchi wengi ya kupata
taarifa kutoka taasisi za serikali hayakujibiwa na/au kukataliwa. Mfano.
Utafiti uliofanywa na MISA Tanzania mwaka 2020 uliohusisha wizara na
taasisi 14 nchini Tanzania umeonesha vikwazo mbalimbali vinavyokwamisha
wananchi kupata taarifa zinazohodhiwa na taasisi husika.
Ingawa
wananchi wengi wana mwamko wa kutafuta na kupata taarifa kutoka taasisi
za umma pamoja na kuongezeka kwa vyanzo vya utoaji taarifa ikiwemo
tovuti na mitandao ya kijamii, bado upatikanaji wa taarifa imeendelea
kuwa kikwazo.
Mojawapo
ya changamoto hizo zilizoainishwa kwenye ripoti ya utafiti wa MISA
Tanzania zinahusisha kukosekana kwa afisa anayeshughulikia maombi ya
taarifa, ucheleweshaji wa utoaji mrejesho na/au kutotolewa mrejesho wa
maombi ya kupata taarifa.
Kwa
kiasi kikubwa, ukuaji wa sekta ya mawasiliano nchini Tanzania
kunakochochewa na maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano hususan
matumizi ya simu za kiganjani na upatikanaji wa intaneti umerahisisha
utafutaji na upatikanaji wa taarifa kutoka taasisi za serikali.
Kwa
mujibu wa ripoti ya MISA Tanzania, wizara zote za serikali na taasisi
za umma zinatoa taarifa zake kupitia tovuti na mitandao ya kijamii.
Matumizi
ya mitandao ya kijamii hususan Facebook, Instagram, Twitter na YouTube
katika kutoa taarifa mpya kwa wananchi yameongezeka miongoni mwa taasisi
husika na hivyo kuongeza uelewa kuhusu taasisi na/au wizara husika.
Hata
hivyo, ripoti imebaini kwamba pamoja na uwepo wa vyanzo hivyo vya
taarifa bado kuna changamoto ya kukosekana kwa taarifa muhimu na
ucheleweshaji wa kuweka taarifa mpya katika tovuti bado kikwazo kwa
wananchi kupata taarifa za taasisi za serikali na umma.
Kwa
upande mwingine, haki ya wananchi kupata taarifa imeathiriwa na uelewa
hafifu wa aina ya taarifa zinazotafutwa, vyanzo vya kupata taarifa
husika, taratibu za kupata taarifa na namna sahihi ya matumizi ya
taarifa inayoombwa.
Aidha,
uwepo wa vifungu vya sheria na kanuni vinavyozuia wananchi na
wanahabari kupata na kutoa taarifa zenye maslahi kwa umma. Sheria
ambazo asasi za kiraia na haki za binadamu, mashirika yasiyo ya
kiserikali na wananchi wanapaza sauti kutaka vifungu vyake vifanyiwe
marekebisho ni pamoja na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, 2016;
Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, 2003; Sheria ya Mawasiliano
ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni na Utangazaji) 2016; na
Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015.
Mabadiliko
ya sheria hizi na nyinginezo sio tu ni muhimu katika kuhimiza uwazi,
demokrasia na utawala bora lakini pia italinda haki ya kikatiba ya kila
raia wa Tanzania ya kupata na kutoa taarifa zenye maslahi kwa umma.
No comments :
Post a Comment