Wednesday, November 11, 2020

TAASISI ZA KIFEDHA NCHINI ZATAKIWA KUSAIDIA WAKULIMA

…………………………………………..

Na.Denis Mlowe , Iringa

ILI kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano chini Rais John Pombe  Magufuli mdau wa Maendeleo wilayani Mufindi, Dk. Basil Tweve ametoa wito kwa taasisi za kibenki kugeukia sekta ya

kilimo katika kuwakopesha kwa masharti nafuu yanayoendana na nadharia ya kilimo kwa wakulima nchini ili kuleta tija katika kilimo cha kisasa.

Akizungumza na mwanahabari, Dk. Tweve ambaye alitia nia ya kugombea ubunge jimbo la Mafinga Mjini na kushika nafasi ya pili, alisema kuwa taasisi za kifedha pamoja na serikali ziangalie kwa undani kumgombea mkulima kwani ndio uti wa mgongo wa taifa la Tanzania.

Alisema kuwa kwa upande wa serikali kupitia taasisi zake kama ugavi, elimu imejitahidi kusambaza maafisa kilimo hivyo watu wengi wamekimbilia kwenye kilimo na kutokana na hilo benki na taasisi nyingine za kifedha ziangalie kwa umakini sekta hiyo kwa kuweka masharti ambayo yanafanana na sekta ya kilimo.

Alisema kuwa mikopo ya kilimo iwe na taswira tofauti na mikopo ambayo inahusu mfanyabiashara wa duka au anayepasua mbao hivyo fursa iliyopo ni benki zianze kukabiliana na wakulima kwa kuwatambua  na kutambua changamoto zao katika kilimo ambapo kubwa zaidi ni mitaji katika kuanzisha kilimo.

Dk Tweve alisema kuwa mwanzoni taasisi za kifedha zilikuja na kasi kubwa ya kuwafanya watu wajikite kwenye kilimo lakini wakulima hawakuwa makini hivyo kutokana na changamoto za maisha watu wengi wameanza kujikita katika kilimo hivyo  mahitaji ya huduma za kifedha ni makubwa kwa wakulima hivyo wito wangu kwa benki kuwekeza zaidi katika kilimo.

“Natoa wito kwa taasisi za kifedha kuwa karibu na wakulima na kutambua changamoto wanazokabiliana nazo hasa katika suala la mitaji kwani ndio inawakumba wakulima waliowengi nchini, hivyo huu ndio wakati sahihi kabisa wa kuendana na juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kumkomboa mkulima” alisema

Aliongeza kuwa mabenki yafike hatua ya kufungua  madirisha kwa ajili ya kutoa huduma katika sekta ya kilimo na wafugaji ili kuzitumia fursa na kupata elimu kutoka kwenye benki husika, bima kwa ajili ya mazao na wanyama wanaowafuga hii itawasaidia wakulima na wafugaji kuondokana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo mitaji.

Aidha Dk. Tweve alisema kuwa katika kukuza uchumi nchini miundo mbinu ya barabara inachelewesha maendeleo na kutoa wito kwa serikali kuangalia suala la miundo mbinu ambayo ina umuhimu mkubwa katika kuunganisha maeneo ambayo ni muhimu kiuchumi.

Alisema kuwa ilani ya CCM awamu hii imegusa sana miundo mbinu hivyo uhakika wa kutengenezwa kwa miundo mbinu hasa ya barabara itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa wilaya ya Mufindi na nchi kwa ujumla na kutoa rai kwa serikali kuhakikisha barababara zinajengwa .

Dk tweve alimpongeza  Rais John Pombe Magufuli kwa uzalendo wake wa kuifanya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati na kuwafanya wakulima na wafugaji wafanye shughuli zao kwa umakini na kukuza uchumi wa Tanzania kwa muda mfupi tangu aingie madarakani.

 

No comments :

Post a Comment