Karibu Mkuu wa Wizara ya Madini Profesa Simon Msanjila akizungumza kwenye uzinduzi wa kamera hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula akizungumza kwenye uzinduzi wa kamera hizo kwa kufanya kazi kwa uadilifu.
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Manyara, Missaile Mussa akiwaleza watendaji wa sekta mbalimbali
wanaofanya kazi kwenye ukuta huo kushirikiana kwa upendo.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Madini Profesa Simon Msanjila kushoto akimkabidhi kitufe cha
kuashiria uzinduzi wa mfumo wa kamera ndani na nje ya ukuta unaozunguka
machimbo ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro
Mkoani Manyara.
……………………………………………………………………………
Na Gift Thadey, Mirerani
SERIKALI imezindua
mfumo wa usalama wa kamera 306 zenye thamani ya shilingi bilioni 1.2
kwenye ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa
Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wenye lengo la kuhakikisha
usalama na ulinzi wa rasilimali hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Madini Profesa Simon Msanjila akizungumza jana mji mdogo wa Mirerani
wakati wa uzinduzi wa kamera hizo amesema kutokana na udhibiti na
ulipaji kodi kwa wachimbaji wa Tanzanite hivi sasa Serikali inaendelea
kuingiza kipato kupitia sekta ya madini.
Profesa Msanjila
amesema kamera hizo zimefungwa na kampuni ya kizalendo ya Starfix
Enterprises ya jijini Dar es salaam kwa gharama ya shilingi bilioni 1.2.
Amesema wakati wa
mchakato wa kutafuta mzabuni wa kutengeneza kamera hizo kuna baadhi ya
kampuni zilipeleka maombi ya kuweka kamera hizo kwa gharama mbalimbali
ikiwemo shilingi bilioni 80 na shilingi bilioni 30.
“Kampuni hii ya
kizalendo inapaswa kupongezwa kwani wamefanya kazi hii kwa maslahi ya
Taifa tofauti na makampuni mengineyo ambayo yalitaka kujineemesha,”
amesema.
Mkuu wa wilaya ya
Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula amesema kamera hizo zitarahisisha
kazi ya kulinda madini hayo na itaondoa kero ya kubaini wahalifu kwenye
migodi hiyo.
Mhandisi Chaula
amesema kupitia kamera hizo kutakuwa na ushahidi usiotia shaka endapo
mtu atakamatwa akifanya uhalifu ikiwemo kupitisha madini.
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Manyara, Missaile Mussa amewataka wadau wa madini ya Tanzanite
wasikubali kuumbuliwa na kamera hizo kwa kufuata sheria katika eneo
hilo.
Mussa amewataka
watendaji wa sekta mbalimbali wanaofanya kazi kwenye ukuta huo
unaozunguka machimbo hayo washirikiane kufanya kazi kwa upendo.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt Faraja Mnyepe ameahidi
kuhakikisha askari wanaendelea kutimiza wajibu wa kulinda rasilimali
hiyo kupitia kamera hizo zinazofanya kazi katika mazingira ya giza,
mwanga, jua, mvua, mchana na usiku.
Hata hivyo, mmoja
kati ya wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite Elisha Mollel pamoja na
kupongeza hatua ya kufungwa kwa kamera hizo ameiomba serikali ifanyie
kazi changamoto ya miundombinu ya barabara.
Mollel amesema
miundombinu inayotumika kupanda na kushuka kuelekea kwenye migodi ni
mibovu hivyo serikali iitengeneze kupitia kodi zinazolipwa.
No comments :
Post a Comment