Naibu Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza na watumishi wa
kituo cha afya Town Clinic (hawapo pichani) Mpanda mkoani Katavi.
Katibu Tawala wa Mkoa
wa Katavi, Bw. Abdallah Mohamed Malela akisisitiza jambo kwa watumishi
wa watumishi wa kituo cha afya Town Clinic (hawapo pichani) Mpanda
mkoani Katavi.

Watumishi wa Kituo
cha Afya Town Clinic kilichopo Mpanda mkoani Katavi wakimsikiliza Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima (hayupo pichani
…………………………………………………….
Na. Majid Abdulkarim, Katavi
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy
Gwajima ameagiza Halmashauri zote nchini kufanya sensa na tathmini ya
wataalamu wa afya waliopo katika vituo vya kutolea huduma za Afya ili
kujua iwapo kila mtaalamu anafanya kazi zake kikamilifu bila vikwazo
vyovyote.
Dkt. Gwajima ameagiza hayo hivi karibuni wakati
alipokutana na watumishi wa kituo cha afya Town Clinic Mpanda mkoani
Katavi ambapo amebaini kuwepo kwa mtaalamu wa afya ya kinywa na meno
ambaye hatumiki kikamilifu kutokana na changamoto ndogo zilizo ndani ya
uwezo wa Halmashauri.
Dkt. Gwajima ameeleza kuwa lengo la kufanya
sensa hiyo ni kubaini mapungufu ambayo yamekuwa yakichelewa kujulikana
na kuweza kufanya uwezeshaji kwa wataalamu ambao hawafanyi kazi zao
kikamilifu kwa sababu mbalimbali ambazo nyingi ufumbuzi wake uko ndani
ya uwezo wa Halmashauri.
Amefafanua kuwa amekuwa akikutana na matukio
kama haya kwenye maeneo kadhaa kitu kinachoashiria kuwa waajiri
wanatakiwa kuimarisha ziadi ufuatiliaji wa wataalamu na kazi
wanazotakiwa kufanyika kama zinafanyika kama ilivyokusudiwa na kama zipo
changamoto ni zipi kwani nyingi wana uwezo wa kuzipatia majibu.
Hata hivyo, amewapongeza Halmashauri ya Mji wa
Mpanda kwa kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanafanya uwekezaji wenye
ubunifu kwa ajili ya kuhakikisha mtumishi huyo anatumika kutoa huduma
kikamilifu.
“Wataalamu wetu wa afya wawezeshwe kwa wao
kuwasilisha mipango yao hatua kwa hatua jinsi gani wataweza kupanuka
kutoka hatua moja ya huduma kwenda ingine ukizingatia hizi ni nyakati za
fursa ya uwepo wa Bima za Afya ikiwemo Mfuko wa Bima ya Afya
ulioboreshwa (ICHF) hivyo, wananchi wanapochangia bima hizi
wanachohitaji ni huduma”, amesema Dkt. Gwajima.
“Kwa hali hii lazima tubadilishe mitazamo yetu
ya jinsi gani wananchi wananufaika na ajira tunazotoa siyo mtaalamu yupo
huduma hakuna na anahitaji mahitaji machache tu tena yako ndani ya
uwezo wa Halmashauri”, ameongeza Dkt. Gwajima.
Lakini pia Dkt. Gwajima ameelekeza timu za afya
mikoa na halmashauri zote nchini kumiliki yaliyomo kwenye Ilani ya
Uchaguzi Mkuu 2020 wa Chama kilichomo madarakani CCM ili ahadi zote
zilizotolewa zitekelezwe kwa kasi na kwa wakati.
Dkt. Gwajima amesema kuwa maisha ya watanzania
ya miaka mitano yako katika ilani hivyo ni wakati sahihi ya kila
mtendaji kwa nafasi yake kutekeleza ilani hiyo kwa nguvu zake na akili
zake zote maana yako mambo ambayo kila ngazi ya utekelezaji inaweza
kuibuka na mpango wa utekelezaji wakati maelekezo ya mikakati mikubwa
zaidi yakiendelea kutolewa.
“Ilani hii ndiyo mkataba na wananchi na sisi
watendaji ndiyo tunaotekeleza hayo yatokee hivyo, mara baada ya Mhe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli
kuapishwa tayari hiyo ilikuwa ni ishara tosha ya kupulizwa kwa kipenga
cha kuanza kutekeleza ilani kwa manufaa ya watanzania wote na taifa kwa
ujumla”, amesisitiza Dkt. Gwajima.
Kwakuongezea Dkt. Gwajima amesema kuwa kiongozi
wa afya ngazi yoyote hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya
anapokuwa hajui kitu gani kimeandikwa kwenye Ilani hiyo kuhusu afya basi
yeye atakuwa amegeuka kuwa tatizo katika kufikia malengo
yaliyokusudiwa.
Dkt. Gwajima
ameinisha moja ya majukumu yaliyopo katika Ilani hiyo ni kuhakikisha
kila mwananchi anajiunga na bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa
huduma za afya hivyo, uhamasishaji wa wananchi kujiunga na bima hizo
uende sambamba na wataalamu waliopo kuwezeshwa kutoa huduma.
No comments :
Post a Comment