…………………………………………………………………………………….
MADINI ya makaa ya mawe yanayochimbwa mkoani Ruvuma yameingiza zaidi ya shilingi bilioni 400 na kutengeneza ajira za watanzania zaidi ya 700.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema kiasi hicho cha fedha kimepatikana kutokana na mauzo ya madini ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 3.3 ambayo yameuzwa kuanzia Agosti 2017 hadi Oktoba 2020.
Ameutaja uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe unafanyika katika wilaya za Songea ,Mbinga na Nyasa na kwamba Mkoa wa Ruvuma una hazina kubwa ya mashapo ya madini ya makaa ya mawe yaliyofanyiwa utafiti na kampuni tatu kubwa za uchimbaji.
“Kwa mujibu wa utafiti unaoendelea kufanyika,Mkoa wa Ruvuma una mashapo ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 457,mashapo hayo tulionayo,tunaweza kufanya uchimbaji kwa miaka 718 bila kumaliza hazina hii’’,amesisitiza Mndeme.
Hata hivyo Mndeme amesema katika kipindi cha mwaka 2019/2020 zaidi ya tani 636,000 za makaa ya mawe yaliyochimbwa mkoani Ruvuma ziliuzwa ndani na nje ya nchi.
Amesema Mkoa wa Ruvuma umebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali yakiwemo madini ya vito na dhahabu ambayo yanachimbwa kwa wingi katika wilaya za Tunduru,Songea ,Mbinga na Nyasa.
Mndeme amesema katika Mkoa wa Ruvuma kuanzia Mei 2019 yalifunguliwa masoko ya madini ya vito na dhahabu katika wilaya za Songea na Tunduru ambapo hadi sasa kupitia masoko hayo zimeuzwa gramu zaidi ya milioni moja zenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 7.7 na kwamba watanzania zaidi ya 1000 wamepata ajira za uchimbaji kwenye madini hayo mkoani Ruvuma.
Amesema tayari limejengwa jengo kubwa la kituo cha umahiri cha madini la Mkoa ambalo litatumika kutoa elimu ya madini kwa wachimbaji wadogo,elimu ya upatikanaji wa masoko ya madini na elimu ya utambuzi wa madini.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
No comments :
Post a Comment