Makamu Wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiangalia maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar {ZRB} Gombani Chake Chake Pemba na kuonya Mkandarasi asiyezingatia Muda wa Mkataba hatopewa tenda nyengine.Mkandarasi wa Ujenzi wa Jengo la ZRB Pemba kutoka Kampuni ya Advent Construction Mhandisi Frenk Mohan akimpatia maelezo Mh. Hemed juu ya ujenzi wa Jengo hilo hapo Gombani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akionyeshwa Ramani ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya ZRB Gombani litakavyokuwa baada ya kukamilika Ujenzi wake.
*********************************
Na Masanja Mabula , Pemba.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa indhari ya kutozipa Tenda Kampuni au Taasisi zozote iwe za Kibinafsi na hata zile za Umma zinazopewa jukumu la Kusimamia Miundombinu ya Ujenzi wa Miradi ya Maendeleo na zikashindwa kuheshimu pamoja na kuzingatia muda wa
utekelezaji wa Mikataba yao.Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa indhari hiyo alipofanya ziara maalum ya kutembelea maendeleo ya Ujenzi wa Ofisi ya Bodi ya Mapato Zanzibar {ZRB} liliopo Gombani sambamba na lile la Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} liliopo Mkanjuni Chake Chake Pemba.
Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema tabia ya baadhi ya Wahandisi wababaishaji wanaopenda kutafuta sababu zisizo na msingi wakati hushangiria kutia saini Mikataba ya Tenda wanazopewa kwa sasa hawatakuwa na nafasi tena.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiagiza Kampuni ya Frenk Mohan inayojenga Jengo la ZRB Gombani na Chuo cha Mafunzo kinachojenga Jengo la ZBC Mkanjuni kukamilisha majengo hayo ndani ya muda mfupi ujao, vyenginevyo Serikali haitakuwa na muda wa kuwapatia tena fursa kama hizo.
Alisema Wafanyakazi wa ZRB na ZBC wamekuwa na usumbufu wa Afisi za kufanyia Kazi ndani ya Kisiwa cha Pemba hali iliyopelekea Serikali kuridhia Ujenzi wa Majengo hayo na haitafurahia kuona Wahandisi waliopewa nafasi hiyo wanaendelea kutoa sababu zisizokubalika na Serikali.
“ Inasikitika kuona Jengo la ZRB lilipangiwa kukabidhiwa Serikalini Mwezi Disemba 2020 lakini bado halijafikia mazingira ya kukamilika na lile la ZBC tayari limeshapindukia Miezi Mitatu sasa”. Alisema Mh. Hemed Suleiman.
Alimuelekeza Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar aangalie Mikataba ya Ujenzi na pale itakapothibitika uzembe wa Mkandarasi kutotimiza wajibu wake atoe Taarifa Serikalini ili Kampuni hiyo ityolewe kabisa katika orodha ya Taasisi zinazopewa jukumu la kuendesha Miradi Visiwani Zanzibar.
Mapema Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar Nd. Joseph Abdulla Meza alisema Jengo hilo la Ghorofa Sita litakapokamilika litasaidia kuondosha usumbufu wa nafasi za Kazi kwa Watendaji wa Taasisi hiyo inayosimamia Mapato ya Taifa.
Nd. Meza alisema mfumo wa Jengo hilo katika sehemu ya chini itazingatia kutoa huduma za Kibenki na Ghala, wakati ile ya pili na Nne zitatumiwa na Wafanyakazi wakati ghorofa ya Tano na sita zitatoa huduma kwa Viongozi na Wajumbe wa Bodi ya Mapato Zanzibar.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Nd. Chande Omar Omar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ujenzi wa Jengo kubwa la Kisasa umekuja kutokana na mabadilikon ya utendaji wa Shirika hilo.
Mkurugenzi Chande alisema Jengo hilo litakapokamilika litakuwa na Studio Mbili zitakazokidhi mahitaji ya kutangazia pamoja na vipindi kwa vile Studio mpya itajengewa mazingira ya kutoa matangazo ya moja kwa moja kutegemea matukio yatakayojiri.
Alisema Studio hizo zitakwenda sambamba na Ofisi za Wafanyakazi huku Wahandisi wakazingatia Wananchi wenye mahitaji maalum watakaofika studio hizo kupata huduma za mawasiliano, matangazo na huduma nyengine.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla ameutaka Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kuanza mara Moja Ujenzi wa Bara bara ya Kipapo hadi Mgelema ili kutekeleza agizo la Serikali ililolitoa la kutaka kazi hiyo ianze mara baada ya kumalizika kwa Bara bara ya Ole Kengeja.
Akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Mgelema baada ya kuikagua bara bara hiyo Mh. Hemed ametoa muda usiozidi saa 12 kuanzia sasa kukutana na Uongozi wa Bodi ya Mfuko wa Bara bara kwenye Makaazi yake Pagali Chake Chake Pemba ili kulijadili suala la Bara bara hiyo iliyokuwa kero kubwa kwa Wananchi wa Maeneo hayo.
Alisema Bara bara ya Kipapo hadi Mgelema bado ninastahiki ijengwe ili kuwaondoshea shida Wananchi waliojenga matumaini makubwa kwa Serikali kutokana na ahadi na Mikakati yake ya kuwatumikia wakati wote.
Alifahamisha kwamba inatia huruma kuona Wananchi wa Vijiji hivyo hasa Kina Mama Wajawazito wanafikia hatua ya kujifungua Majumbani kwa kukosa usafiri wa kuwapeleka kwenye Vituo vya Afya pamoja na Hospitali jambo ambalo ni hatari kwa Maisha.
Mapema Mhandisi wa Ujenzi kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasliano na Usafirishaji Mhandisi Khamis Masoud alisema Ujenzi wa Bara bara hiyo tayari umeshaingizwa ndani ya Mpango wa Wizara kwa ajili ya Ujenzi wa Kiwango cha Lami.
Mhandisi Khamis alisema Wizara inayosimamia Mawasiliano ya Bara bara imeshajipanga kutumia shilingi Milioni Mia 500,000,000/- kwa ajili ya hatua za Ujenzi wake huku Mfuko wa Bara bara ukitenga shilingi Miklioni 200,000,000/- ili zitumike kwa hatua ya awali ya bara bara hiyo kupitika hata kipindi cha mvua.
Alisema ujenzi wa Bara bara hiyo kwa kiwango cha Lami hadi kukamilika kwake utahitaji jumla ya shilingi Bilioni Mbili Nukta Mbili.
No comments :
Post a Comment