Friday, November 13, 2020

Fahamu kuhusu mkopo wa elimu unaotolewa na ZSSF

 

Wahitimu wakiwa katika Mahafali ya 14 ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) ambao baadhi yao ni wafanyakazi walionufaika kwa mkopo wa elimu unaotolewa na mfuko wa hifadhi ya jamii wa Zanzibar (ZSSF) kwa wanachama wachangiaji wenye lengo kuwapa fursa za kujiendeleza kielimu ngazi yoyote. (Na Mpigapicha Wetu)

Na Christian Gaya. Majira Ijumaa 13. Novemba. 2020

Tanzania mpaka sasa inaendelea kukabiliana na tatizo la uhaba wa fursa ya mikopo ya elimu pamoja na ajira. Hiyo ni kutokana na wigo mdogo wa fursa za mikopo ya elimu na ajira, tatizo la utaalamu na ukosefu wa uzoefu kwa wafanyakazi unaozidi kutanuka nchini.

Hivyo basi, suala la mikopo ya elimu na ajira kwa vijana linatakiwa kubaki kuwa ajenda kuu nchini.

Kwa sababu pamoja na kuwepo na maendeleo ya kuridhisha kidogo katika suala la mikopo ya elimu na ajira kwa vijana, hata serikali imekiri kwamba ukosefu wa mikopo ya elimu na ajira bado ni tatizo kubwa duniani na kwa taifa kwa ujumla.

Hata hivyo vijana wanaoamua kujiajiri wenyewe wamekuwa wakikabiliana na tatizo kubwa la mtaji, mikopo ya elimu, maeneo ya kufanyia kazi na utaalamu katika ujasiriamali utakaowawezesha kuendesha miradi wanayoibuni.

Kutokana na uwapo wa sera, mipango na miradi ya maendeleo kuhusu mikopo ya elimu na ajira kwa vijana inayoendeshwa kitaifa na kimataifa kumekuwepo na dalili njema za kupungua kwa ukosefu wa ajira.

Kwa mfano, kwa utafiti uliofanywa wa mwaka 2014 ulionesha kwamba ukosefu wa ajira ulipungua kutoka asilimia 11.7 kwa mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 10.3 ka mwaka 2014 huku kwa vijana (wenye umri wa miaka 15 hadi 35) ukipungua kutoka asilimia 13.2 kwa mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 kwa mwaka 2014.

Utafiti uliofanywa mwaka 2012 unaonesha ya kuwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 23 wako milioni 16.

Hao ni sawa na asilimia 31 ya watanzania wote, huku nguvukazi yao ikitegemewa kwa asilimia 59.

Takwimu pia zinaonesha tatizo la ajira liko zaidi mijini ambayo ni asilimia 18.3, ukilinganisha na asilimia 8.6 kwa vijana waishio vijijini.

Na takwimu hizi zinaathiri zaidi vijana wa kike, wakati watu wenye kufanya kazi ni asilimia 10.3.

Ingawa takwimu zinaonesha ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua.

Mafanikio yaliyopatikana hayaondoi ukweli kuwa kuna tatizo kubwa la ajira miongoni mwa vijana na kutokana na mazingira ya sasa ni vyema wadau wa ajira kuangalia kwa undani tatizo la ajira la sasa ili kutoa ushauri wa kukabiliana nalo kwa kipindi kifupi na kirefu.

Hivyo kuna haja kwa wachambuzi yaani watafiti kuelekeza nguvu zao katika kutafiti soko la ajira ili kusaidia watengeneza sera kuona mahitaji ya soko katika miaka kadhaa ijayo.

Ingawa wakati uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia 7 kwa mwaka kwa miaka kumi iliyopita ajira zimekuwa haziendi sambamba na ukuaji wa uchumi na hivyo kuleta maswali mengi ya sintofahamu.

Taarifa za idadi ya watu nchini zinaonesha kuwa asilimia 45 ya watanzania wote wana umri chini ya miaka 15. Hili ni kundi lingine kubwa mno la vijana watarajiwa ambao inabidi kuwaandaa kama nguvukazi ya Taifa letu.

Imedhihirika kuwa wafanyakazi na vijana walioandaliwa vizuri katika Taifa lolote lile, wanao mchango mkubwa katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii.

Kwa hiyo, serikali ina wajibu mkubwa wa kuwasaidia wafanyakazi na vijana kutambua fursa na nafasi zao katika maendeleo ya Taifa kwa kuwaendeleza kielimu katika nyanja mbalimbali.

Pia idadi kubwa ya wafanyakazi na vijana wasomi walioko vyuoni wengi wana tatizo la kutopata ada za vyuo zinazotosheleza hasa kutokana na ufinyu wa bajeti ya serikali ambapo inashindikana hata wanafunzi wote kupata mikopo ya elimu ya juu hata kwa asilimia mia.

Hivyo, kwa kutambua umuhimu na changamoto za elimu katika jamii ya sasa hasa za wafanyakazi na vijana, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa kushirikiana na Benki ya Posta nchini umebuni huduma ya mkopo wa elimu kwa ajili ya wanachama wake kujiendeleza kielimu, ambapo wanatoa fursa kubwa kwa wanachama wake kupata mikopo yenye uhakika na masharti nafuu.

Huduma za mkopo ya elimu ni huduma muhimu sana kwa wafanyakazi kwani wanapata fedha za kujiendeleza, kwa sababu imekuwa ni changamoto kubwa kwa wafanyakazi hivyo kupatikana kwake kumeanza kufungua milango kwa wafanyakazi kujiendeleza kielimu bila vikwazo.

Kulingana na Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF Sabra Machano anasema mfuko umetambua mzigo mkubwa uliobebwa na serikali katika kuwasomesha wafanyakazi na vijana hivyo umeamua kubeba jukumu la kuwasaidia wafanyakazi kukopa kwa lengo la kujiendelea kielimu.

"ZSSF unaendelea kubuni huduma mbalimbali za kihifadhi ya jamii kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wananchi wa kila kada hapa nchini" anasema Sabra.

Mkopo huu wa elimu ulizinduliwa kwa lengo la kumsaidia mwanachama wa ZSSF kutimiza ndoto zake kwa kujiendeleza kielimu katika ngazi yoyote, stashahada, shahada, shahada ya uzamili na nyinginezo.

Mfuko unagharamia ada kwa kipindi chote cha masomo ya mwanachama mchangiaji wa ZSSF.

"Mwanachama wa ZSSF anayetaka kukopa aina hii ya mkopo atadhaminiwa na mwajiri wake, pia mkopo huu una bima, hivyo endapo mkopaji atafariki familia yake haitaendelea kudaiwa. Na riba inayotozwa kwa mkopo huu ni asilimia 12 tu kwa mwaka ambao ni nafuu mno ukilinganisha na aina ya riba ya mikopo mengine inayotozwa sokoni" Sabra anafafanua.

Anasema kuwa vigezo vinavyozingatiwa katika kutoa mkopo huu wa elimu ni mwanachama kuwa amethibitishwa na mwajiri wake, mwanachama awe amekubaliwa kujiunga na chuo cha ndani au nje ya nchi, mwanachama awe na kibali cha mwajiri wake.

 “Natoa wito kwa watanzania wenzetu kujiunga na mfuko wa hifadhi ya jamii wa ZSSF ili waweze kufaidika na fursa hizi” Sabra anasisitiza.

Mfuko wa ZSSF kama zilivyo Taasisi nyingine za hifadhi ya jamii katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati, ulianzishwa kwa Sheria ya Baraza la Wawakilishi mnamo mwaka 1998, Sheria ambayo ilifanyiwa mabadiliko na mapitio mara kadhaa ikiwemo mwaka 2002, kutungwa upya mwaka 2005 na pia kufanyiwa marekebisho mwaka 2016.

 

No comments :

Post a Comment