Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzora akieleza jambo wakati wa sherehe za kuhitimu mafunzo ya Ushirika kwa Viongozi na Watendaji wa Ushirika. Mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) kwa njia ya Masafa Sherehe zilizofanyika Bukoba, Kagera hivi karibuni
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akieleza masuala ya Sekta ya Ushirika wakati wa sherehe za kuhitimu mafunzo ya Ushirika kwa Viongozi na Watendaji wa Ushirika.
Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof. Alfred Sife akiwaeleza matarajio ya Chuo kwa wahitimu wa Ushirika katika kuongeza ufanisi na tija ya utendaji katika Vyama vya Ushirika. Wakati wa sherehe za kuhitimu mafunzo kwa njia ya Masafa zilizofanyika Bukoba, Kagera hivi karibuni
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzora akikabidhi Cheti cha kuhitimu mafunzo ya Ushirika kwa Zaituni Dotto Mtunza Fedha wa Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo (SACCOS) kiitwacho Jitihada kilichopo Biharamulo Mkoani Kagera. Katikati ni Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akifuatiwa na Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Kagera Bw. Godfrey Mpepo wakati wa sherehe za kuhitimu mafunzo ya Ushirika kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) kwa njia ya Masafa zilizofanyika Bukoba, Kagera hivi karibuni
Sehemu ya Wahitimu wa mafunzo ya Ushirika Wakati wa sherehe za kuhitimu mafunzo kwa njia ya Masafa zilizofanyika Bukoba, Kagera hivi karibuni
……………………………………………………………………………..
Kagera, Bukoba
Elimu ya Fedha imetajwa kuwa moja ya nyenzo muhimu katika kuimarisha na kuendeleza Ushirika kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Serikali za kuondoa umaskini na kuinua
uchumi wa Wananchi.Hayo yamesemwa na Mgeni rasmi Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Prof. Faustine Kamuzora wakati wa Sherehe zilizofanyika Bukoba Mkoani Kagera kukabidhi Vyeti kwa Wahitimu wa Programu za mafunzo ya Uongozi na Usimamizi pamoja na Utunzaji wa Hesabu za Vyama vya Ushirika kwa njia ya masafa. Mafunzo yaliyokuwa yakitolewa na kuratibiwa na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kwa viongozi wa Vyama vya Ushirika wa mikoa ya Kagera, Tabora, Geita na Simiyu.
Akiongea katika Sherehe hizo Prof. Kamuzora amewataka Wahitimu hao ambao wengi wao ni Viongozi wa Vyama vya Ushirika kutumia elimu waliyopata katika kusimamia Vyama vya Ushirika kwa weledi ili kulinda maslahi ya Wanachama wa Ushirika. Akisisitiza suala la Viongozi hao kutumia elimu ya fedha waliyopata kuongeza na kubuni mbinu mbalimbali za kuongeza vipato kwa Vyama vyao vya Ushirika wanavyosimamia.
“Hakikisheni mnaendelea kuitumia elimu ya Fedha mliyoipata kwaajili ya kuimarisha na kuongeza mapato ya Vyama vya Ushirika na elimu hiyo mkawashirikishe Wanachama katika Vyama vyenu vya Ushirika” alisema Prof. Kamuzora
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege katika hotuba yake amewataka Viongozi waliopata mafunzo ya Ushirika kwenda kuleta mabadiliko chanya katika Vyama wanavyosimamia, akisisitiza utendaji utakaondoa changamoto za ubadhilifu na Hati zisizoridhisha ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.
“Moja ya sababu ambazo zimekuwa zikileta changamoto katika Sekta ya Ushirika ni watendaji na Viongozi kutokuwa na uelewa sahihi wa namna bora ya utunzaji wa hesabu na Kumbukumbu za Vyama vya Ushirika, ni imani yangu mafunzo haya yanakwenda kuongeza ufanisi na Hati safi kwa Vyama vyetu,” alisema Mrajis
Aidha, Mrajis ametoa wito kwa Wanawake wengi kushiriki nafasi mbalimbali za Uongozi wa Vyama vya Ushirika hususani wakati huu ambao Vyama vingi vya Ushirika vinakwenda kufanya Uchaguzi wa nafasi za Uongozi ikiwemo Wajumbe wa Bodi, Mameneja na Watendaji wengine.
“Ushirika ni Sekta ambayo inahitaji kutekeleza na kuonesha usawa wa Kijinsia kwa vitendo kwa kuwa na viongozi wanawake katika Vyama vyetu vya Ushirika kwani wanawake ndio msingi na walezi wa familia na Jamii kwa ujumla,” alisisitiza Mrajis
Mrajis Ndiege pia amewataka Warajis Wasaidizi wa Mikoa kwa kushirikiana na Maafisa Ushirika wa Wilaya katika Mikoa mingine kuendelea na jitihada za kujiendeleza kimaarifa hususani katika masuala ya Uandishi mzuri wa Vitabu vya Ushirika mara baada ya msimu wa mazao ili kuondokana na dosari mbalimbali zinazoleta taswira hasi kwa Sekta ya Ushirika.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof. Alfred Sife alieleza kuwa mafunzo hayo awali yalikuwa yakifanyika kwa njia ya Posta, ambapo hivi sasa kutokana na maendeleo ya kiteknolojia mafunzo ya Ushirika yanafanyika kwa masafa. Mkuu huyo alifafanua kuwa utoaji huo wa elimu ni miongoni mwa mikakati ya Chuo hicho katika kuhakikisha wigo wa upatikanaji wa elimu unaongezeka na Vyama vya Ushirika vinakuwa imara zaidi kwa kuwafikishia mafunzo mahali walipo.
Baadhi ya masuala yaliyotajwa kuwa ni sehemu ya mafunzo hayo ni pamoja uelewa wa dhana ya Ushirika, Misingi ya Ushirika, Uongozi wa Asasi za Ushirika, Kanuni za Utunzaji wa Mahesabu ya Ushirika, uchanganuzi wa Ushirika wa mazao, utunzaji Kumbukumbu pamoja na mada nyingine zenye kuongeza tija ya utendaji wa Vyama vya Ushirika.
Katika Sherehe hiyo jumla ya Viongozi 120 wamehitimu mafunzo hayo ya Ushirika na kukabidhiwa Vyeti vya kumaliza mafunzo. Akisoma risala kwa niaba ya Wahitimu Mjumbe wa Bodi KDCU Bw. Fidolin Kasenene ameshukuru Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi pamoja na Wadau wa Ushirika waliofanikisha mafunzo hayo, huku akiomba mafunzo kama hayo yawe endelevu ili kuongeza ufanisi na usimamizi bora wa Vyama vya Ushirika nchini.
No comments :
Post a Comment