Na Christian Gaya, HakiPensheni Center
Elimu ya Mpiga Kura ina lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya mambo ya msingi yatakayowawezesha kutekeleza kwa usahihi jukumu la kupiga kura Siku ya Uchaguzi Mkuu ambayo ni siku ya Jumatano, tarehe 28 Oktoba, 2020.
Kwa mfano, kabla ya kuanza kupiga kura msimamizi wa kituo kwa kawaida atatakiwa kufungua masanduku ya kuhifadhia kura na kuwaonesha Mawakala wote na watu wengine wanaohusika na
Uchaguzi watakao kuwepo katika kituo. Masanduku ya kuhifadhia kura yatafungwa na kuwekewa lakiri, ambayo ni vigumu kufungua pasipo kuvunja, baada ya hapo yatatakiwa kuwekwa mahali pa wazi wakati wote wa upigaji kura.Msimamizi wa Kituo pia atatakiwa kuonesha bahasha yenye karatasi za kupigia kura ambazo zimefungwa kuonesha kuwa hakuna mtu aliyezifungua hapo kabla. Uratibu wa upigaji kura ni kwamba mpiga kura atatakiwa kumkabidhi Msimamizi wa Kituo kadi yake ya kupigia kura.
Jina la Mpiga Kura litatakiwa kusomwa kwa sauti kubwa ili Mawakala wa Vyama vya siasa waliopo wasikie. Msimamizi wa Kituo na Mawakala wa Vyama vya Siasa kama watajiwa na shaka watakuwa na haki ya kukuuliza maswali ili wajiridhishe.
Msimamizi wa Kituo atamkabidhi Mpiga Kura karatasi za kura za aina ya 1 (ya Rais) au 2 (ya Urais na Ubunge) au 3 yaani (Urais, Ubunge na Udiwani) na pia atamwonesha jinsi ya kukunja karatasi hizo.
Baada ya hapo Mpiga Kura atatakiwa kwenda sehemu maalumu iliyotengwa kwa ajili ya kupiga kura. Mpiga Kura ataweka alama ya vema (v) ndani ya chumba kilichopo ndani ya picha ya mgombea anayemtaka.
Mpiga Kura atatakiwa kutumbukiza karatasi zake za kura katika masanduku kwa jinsi atakavyoelekezwa, na kabla ya kuondoka kituoni Mpiga Kura atatakiwa kuchovya kidole chake kidogo cha mkono wa kushoto katika wino maalumu usiofutika.
Pia ni kosa la jinai: kujaribu kupiga kura zaidi ya moja katika uchaguzi, kujaribu kupiga kura kwa kutumia kadi ya mtu mwingine na kujaribu kupiga kura wakati muda wa kupiga kura umekwisha. Makosa mengine ni kujaribu kupiga kura wakati hauruhusiwi kisheria kupiga kura, na kuchana orodha ya wapiga kura au mabango yoyote ya elimu kwa mpiga kura yaliyopo vituoni.
Kura Yako, Sauti Yako, Nenda Ukapige Kura
No comments :
Post a Comment