…………………………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
Katibu Mkuu Wizara ya
elimu, sayansi na teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amewaasaa baadhi ya
wadhibiti ubora wa shule nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi na
kuacha lugha za vitisho kwa wateja.
Dkt. Akwilapo
aliyasema hayo katika ufunguzi wa mafunzo maalum kwa wathibiti wakuu
ubora wa Shule kanda na Wilaya zote Tanzania bara, wapatao 217,
yanayofanyika wilayani Bagamoyo kwa muda wa siku tatu .
Anasema,lengo la
mafunzo ni kuwaongezea ujuzi wa masuala mbalimbali ya utendaji katika
utumishi wa umma na kuwasaidia wathibiti wakuu ubora wa shule kuondoa
ama kurekebisha changamoto za kiutendaji ambazo zimekuwa zikiripotiwa
kwa uongozi wa wizara mara kwa mara katika maeneo wanayosimamia.
“Wizara imekuwa
ikipokea malalamiko kutoka kwa wadau na watoaji wa elimu kuhusu mwenendo
usiofaa wa baadhi ya Wathibiti Ubora wa Shule kutoa lugha za vitisho
kwa wateja na wakati mwingine kuwaomba Rushwa ili kufanikisha usajili wa
Shule au Vyuo vyao .
“Hii ni kukiuka
maadili ya utendaji katika utumishi wa umma kwa kutozingatia sheria,
kanuni na maadili ya utendaji katika utumishi wa Umma na wadhibiti ubora
wa elimu wanaofanya vitendo hivi waache mara moja kwani taarifa zako
zitakapotufikia hatutasita kukuchukulia hatua za kinidhamu” Amesema Dkt.
Akwilapo.
Nae Mshiriki wa
Mafunzo hayo Bi. Tatu Tamizi Kutoka Wilaya ya Gairo akizungumza kwa
niaba ya Washiriki wenzake wa mafunzo hayo amesema, wanashukuru Wizara
ya elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwaandalia mafunzo hayo ambayo
wanaamini yatawaongezea weledi na ufanisi katika utendaji kazi wao na
hivyo kuboresha utoaji huduma za elimu Nchini.
No comments :
Post a Comment