Friday, October 16, 2020

VIWANDA VYA CHAI LUPEMBE NA IKANGA VYATEKELEZA AGIZO LA SERIKALI KUWALIPA WAKULIMA-KUSAYA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (kushoto)akiongea na Mkurugenzi wa Kiwanda cha Chai Lupembe Yusufu Mulla mara baada ya kikao chake na wakulima na viongozi wa Chama cha Ushirika wa wakulima wa chai Lupembe (MVIULU) .Kiwanda cha Chai Lupembe kilmelipa shilingi milioni 469.8 kati ya deni la milioni 594.1 lililokuwa linadaiwa na wakulima mwaka 2018 ambapo Katibu Mkuu huyo amegiza ifakapo Novemba 15 mwaka huu deni hilo lilipwe lote.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (katikati) akizungumza na Mkurugenzi wa kiwanda cha chai Lupembe Yussuf Mulla (kushoto) na Meneja kiwanda cha chai Ikanga Gerald Ngenzi (kulia) mara baada ya kikao na wakulima wa chai Tarafa ya Lupembe wilaya ya Njombe leo. Katibu Mkuu alikuwa huko kufuatilia agizo lake alilolitoa Julai 15 mwaka huu kuhusu kulipwa wakulima wanaodai viwanda hivyo amabalo limeanza kutekelezwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (kushoto) akikabidhi pikipiki mbili kwa Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Ichenga wilaya ya Njombe Esther Mwanjonde leo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Julai 13,2020 alipotembelea kituo hicho.

 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya akipokelewa na Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Ichenga wilaya ya Njombe Esther Mwanjonde  leo alipotembelea kituo hicho kukagua utekelezaji wa maagizo yake kuhusu ukarabati wa miundombinu ya kituo hicho.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (kushoto) akitazama kisima cha maji alipotembelea kituo cha wakulima Ichenga wilaya ya Njombe. Kisima hicho kimefungwa pampu inayowezesha maji kusambazwa kwenye makazi ya watumishi na maeneo ya miradi kufuatia fedha zilizotolewa na Katibu Mkuu huyo mwezi Julai 2020 ili kuboresha miundombinu ya kituo hicho kinachotumika kufundisha wakulima kuongeza tija ya uzalishaji.

Katibu Mkuu Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kushoto ) akitazama maeneo ya miradi wakati alipotembelea kituo cha mafunzo ya wakulima Ichenga wilaya ya Njombe leo. Kituo hicho ni moja ya vituo vinne chini ya Wizara ya Kilimo vinavyotumika kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima .

Kitalu nyumba kilichotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya kufuatia zaiara yake mwezi Julai 2020 kwa kituo cha Mafunzo ya Wakulima Ichenga Njombe.Kitalu nyumba hicho kinatumika kufundishia wakulima na kanuni bora za uzalishaji na teknolojia mpya katika kilimo.

………………………………………………………………………………………….

Viwanda vya chai vya Lupembe na Ikanga vya mkoani Njombe vimetekeleza agizo la serikali la

kulipa wakulima julma ya shilingi Bilioni 1.433 zilizotokana na mauzo ya awali ya majani mabichi ya chai mwaka 2018.

Akizungumza na wakulima wa chai wa Lupembe Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alisema amefurahi kuona agizo alilolitoa mwezi Julai alipofanya ziara kijijini hapo kuona limeanza kutekelezwa na wakulima wameanza kupata fedha zao.

“Nimekuja hapa Lupembe kufanya ufuatiliaji wa agizo langu la kutaka wakulima walipwe fedha zao baada ya kuuza majani ya chai kwenye viwanda vya Lupembe na Ikanga mwaka 2018 na nimeridhika kuona sehemu kubwa ya fedha zimelipwa tayari” alisema Kusaya.

Akizungumza kwenye kikao hicho Meneja wa Kiwanda cha Chai Ikanga Gerald Ngenzi alisema wametekeleza agizo la serikali kwa kulipa jumla ya shilingi 539,902,534 kati ya deni lote la shilingi 839,870,331 wanazodaiwa na wakulima ikiwa ni malipo ya awali ya mwaka 2018.

Ngenzi alisema deni la shilingi 299,964,701 kiwanda kinatarajia kulipa mapema mwakani baada ya kuuza chai iliyopo kwenye maghala kufuatia soko la nje ya nchi kuathiriwa na ugonjwa wa Korona.

Hata hivyo, wakulima walikataa ombi hilo la kiwanda kumalizia deni lao mwezi Mei na kuwa wanataka walipwe mapema hali iliyomfanya Katibu Mkuu Kusaya kuagiza kiwanda hicho kukamilisha malipo ifikapo tarehe 01 Januari 2021.

“Nataka kiwanda cha Ikanga ifikapo Januari mosi mwakani deni hili la shilingi milioni 299 liwe limelipwa kwa wakulima wa chai waliobaki na msizalishe tena deni. Nitarudi hapa tena Januari 2021 kufutilia na endapo mtashindwa tutaanza kuwatoza riba” alisema Kusaya

Naye Mkurugenzi wa Kiwanda cha Chai Lupembe Yusuf Mulla alisema wametekeleza agizo la serikali kwa kulipa Shilingi 469,835, 060 kati ya deni lote la Shilingi 594,125,280 la wakulima wa Lupembe na kubakiwa na deni la Shilingi 124,290,215

Ili kukamilisha deni lililobaki Mulla alisema wanaomba serikali iwape muda wa mwezi mmoja ili walipe deni  la Shilingi Milioni 124,290,215 za malipo ya awali ya wakulima waliouza chai kiwandani mwaka 2018.

“Katibu Mkuu tunaomba muda wa mwezi mmoja hadi tarehe 15 Novemba mwaka huu tukamilishe deni lote la shilingi milioni 124 za wakulima wa chai na jitihada zetu zinaendelea vema kutafuta fedha .Nakuahidi kiwanda chetu tutamaliza deni hilo kama ulivyoagiza” alisema Mkurugenzi Mulla.

Kufuatia hali hiyo, Katibu Mkuu Kusaya alitoa agizo kuwa kiwanda hicho kilipe madeni yaliyosalia ifikapo tarehe 16 Novemba 2020 na kuwa anataka kuona wakulima wa chai Lupembe wakianza mwaka mpya bila kudai fedha zao kwa wawekezaji wa viwanda hivyo.

“Tunataka tuanze mwaka mpya 2021 bila madeni ili wakulima wanufaike na kazi zao kwa kuuza majani mabichi ya chai na kulipwa mara moja. Endapo mwekezaji hawezi kulipa wakulima ni bora akaondoka na kuachia viwanda vyetu mlivyouziwa na serikali” alisisitiza Kusaya.

Katibu Mkuu huyo aliongeza kusema Wizara ya Kilimo inafanya ufuatiliaji wa karibu kujua uhalali wa umiliki wa kiwanda cha Lupembe kupitia Msajili wa Hazina na kuwa ikibainika kuwa kiliuzwa kinyemela hatua za kukirejesha serikalini au kwa wanaushirika zitachukuliwa .

Aidha, alitoa rai kwa wanaushirika nchini hususan viongozi  waliojimilikisha mali za ushirika bila kufuata taratibu kuwa warudishe mara moja kwani tayari Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alishaagiza utaratibu wa kuzirejesha mali hizo ufanyike.

“Kama kuna mtu au kiongozi alichukua mali za ushirika Lupembe awe hai au amekufa tunamtaka azirudishe mara moja kabla serikali haijachukua hatua za kisheria kuzitwaa “alisema Kusaya.

Katika hatua nyingine Kusaya alimwagiza Mrajis Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Njombe kusimamia Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Chai Lupembe (MVIULU) kuwalipa wakulima fedha zao shilingi milioni 17 wanazodai baada ya kuuza majani mabichi ya chai.

Mrajis Msaidizi wa Ushirika mkoa wa Njombe Consolata Kiluma alisema tayari taratibu za kulipa fedha hizo za wakulima wa chai zilikwama kufuatia akaunti ya benki ya MVIULU kuzuiwa na uongozi wa mkoa ili kufanya uchunguzi kufuatia mgogoro wa viongozi unaoendelea.

Consolata alisema kuwa kuanzia wiki ijayo wakulima wa chai wanaodai ushirika wa MVIULU wataanza kulipwa kufuatia uchunguzi kukamilika na mkoa kutoa ridhaa ya malipo yaendelee.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Kusaya alitembelea Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Ichenga kilichop Kata ya Uwemba wilaya ya Njombe kufanya ufuatiliaji wa maagizo yake aliyotoa mwezi Julai kuhusu ukarabati wa kituo hicho.

Akiwa kituoni hapo alifurahishwa na kuridhishwa  kukamilika kwa ukarabati wa nyumba ya mtumishi, kukamilika kwa kisima cha maji na ujenzi wa zizi bora la ng’ombe kufuatia fedha shilingi milioni 3 alizotoa kwa kazi hiyo.

Akitoa taarifa ya kituo hicho Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Wakulima Ichenga Esther Mwanjonde alimshukuru Katibu Mkuu huyo kwa kutoa fedha Shilingi milioni 3.6 zilizotumika kufanya ukarabati wa kituo hicho kama alivyoahidi .

“ Tunashukuru sana serikali kwa kutoa fedha za ukarabati wa kituo hiki, awali tulikuwa na shida ya maji lakini tumesaidiwa kisima na mashine inayosambaza maji kwenye maeneo yote ya kituo pia ukarabati wa nyumba ya mtumishi “ alisema mkuu wa kituo hicho.

Katibu Mkuu Kusaya alimpongeza Mkuu huyo wa kituo kwa kutumia vema fedha za ukarabati na kutoa wito kwa watumishi wa wizara ya kilimo kote kwenye taasisi, Idara na wakala kuhakikisha wanatumia vema fedha zinazotolewa na serikali ili zilete tija.

“Fedha ya serikali hata iwe ndogo kiasi gani lazima tuone thamani ya fedha kwa kazi iliyokusudiwa hivyo yeyote atakaye tumia vibaya fedha za serikali sitamfumbia macho, nitachukua hatua kali “  alisema Kusaya.

Katibu Mkuu huyo wa wizara ya Kilimo alikabidhi pia pikipiki moja aina ya Suzuki na pikipiki moja ya miguu mitatu (guta) kwa kituo cha mafunzo Ichenga ili zisaidie usafiri na usafirishaji wa mazao toka shambani.

 

No comments :

Post a Comment