Mkurugenzi wa ununuzi na ugavi kutoka wizara ya maji Dkt Christopher Nditi kushoto akiongea na baadhi ya akina mama wa kijiji cha Mkowela wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma waliokutwa wakichota maji katika moja kati ya vituo vya kuchotea maji alipotembea mradi wa maji katika kijiji hicho jana akiwa katika ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maji mkoani Ruvuma. Mkurugenzi wa ununuzi na ugavi wa wizara ya maji Dkt Christopher Nditi akimsaidia mkazi wa kijiji cha Mkowela wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Monica Olfu kubeba ndoo ya maji mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa na wakala wa maji vijijini Ruwasa wilaya ya Tunduru,
Picha zote na Muhidin Amri
**************************************
Na Mwandishi Wetu,
Tunduru
IMEELEZWA kuwa ujenzi wa miradi ya maji kwa kutumia njia ya force akaunti katika maeneo mengi hapa nchini, umeleta tija kubwa na kupata miradi ya kiwango na ubora wa hali ya juu hivyo serikali kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya kumtua mama ndoo kichwani na
kuharakisha maendeleo ya wananchi.Hayo yamesemwa jana na mkurugenzi wa ununuzi na ugavi wa wizara ya maji Dkt Christopher Nditi alipokuwa akiongea na wananchi wa kijiji cha Mkowela kata ya Namakambale wilaya ya Tunduru, mara baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho unaotekelezwa na wakala wa maji vijijini Ruwasa.
Pia alisema, mfumo wa force akaunti umesaidia kukoa fedha nyingi na kuwaongezea ujuzi wataalam wa wizara ya maji ili waweze kuwa na weledi katika kutekeleza na kusimamia miradi mbalimbali ya maji hapa nchini badala ya kutumia wakandarasi ambao kwa muda mrefu wamekwamisha juhudi za wizara kufikisha huduma ya maji kwa wananchi.
Ameipongeza Ruwasa ngazi ya wilaya na mkoa kwa kufanya kazi kwa pamoja wakati wote wa Utekelezaji wa miradi, jambo lililowezesha miradi mingi ya maji katika mkoa wa Ruvuma kukamilika kwa wakati na hivyo kuleta tija iliyokusudiwa ya Serikali ya kufikisha huduma ya maji katika makazi ya wananchi.
Kwa upande wake meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Primy Damas alisema, mradi wa maji Mkowela umegharamiwa na Serikali kuu kupitia wizara ya maji na umwagiliaji na kutekelezwa na wakala wa maji vijijini na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kwa kutumia njia ya lipa kutokana na matokeo(force account).
Alisema,kipindi cha Utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji ni siku 90 na utekelezaji ulianza mwezi Mei 2020 na unatarajiwa ulitarajiwa kukamilika Mwezi Julai,hata hivyo kutokana na sababu mbalimbali muda wa kukamilika mradi huo uliongezwa hadi kufikia Mwezi Oktoba mwaka huu.
Alisema, gharama ya mradi ni shilingi milioni 160.4 ambazo tayari zimetolewa na serikali ambapo zaidi ya wakazi 3,300 wa kijiji hicho wameanza kunufaika na mradi huo kwa kupata maji safi na salama.
Aidha alisema, katika ujenzi huo kazi zilizopangwa kufanyika ni kujenga tenki la juu lenye ujazo wa lita 50,000,ujenzi wa nyumba ya mitambo,kuchimba mitaro na kujaza mabomba ya maji km 3.2 kujenga vituo vya kuchotea maji na kufunga mita za maji na kujenga uzio eneo la chanzo na tenki, na kuvuta umeme katika nyumba ya mitambo kazi ambazo zimekamilika kwa asilimia 90.
Baadhi ya wananchi waliokutwa katika moja ya vituo vya kuchotea maji Asia Ahmad na Monica Olfu, wameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kupeleka huduma ya maji safi na salama na hivyo kupunguza muda wa kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji katika mito na visima vya asili .
Monica Olfu alisema, changamoto kubwa iliyokuwepo katika kijiji cha Mkowela ni maji safi na salama kwani hapo awali walilazimika kutumia kati ya masaa 2-3 kwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.
No comments :
Post a Comment