Monday, October 19, 2020

TUNATAFUTA MASOKO YA UHAKIKA YA MAZAO YA WAKULIMA -KM KUSAYA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (kulia) akifuatilia taarifa ya hali ya kilimo toka kwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt. Seif Shekalaghe (aliyesimama).Katibu Mkuu huyo ameanza ziara ya kikazi ya kukagua shughuli za kilimo mkoani Songwe.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig.Jen. Nicodemus Mwangera (kushoto) akiwa kwenye mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya (kulia) ofisini kwake leo Vwawa Mbozi. Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig.Jenerali Nicodemus Mwangela(kushoto) akiwa kwenye mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (kulia).Kulia  aliyevaa shati la njano ni Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga.

 Katibu Mkuu Kilimo Bw. Gerald Kusaya (katikati) akisikiliza maelezo ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu (ASA) Dkt. Sophia Kashenge ( kulia) wakati alipowasila kijiji cha Iganya wilaya ya Mbozi kukagua shamba la mbegu bora za mahindi na michikichi.

*************************************

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya leo (19.10.2020) ameanza ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Songwe kwa lengo la kukagua shughuli za sekta ya kilimo.
Kusaya mapema asubuhi amekutana na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela ambaye ameishukuru wizara ya Kilimo kwa usimamizi mzuri wa sekta hali inayowafanya wakulima wazalishe mazao kwa wingi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Kusaya alisema anatembelea Songwe ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe na Rais Dkt.John Pombe Magufuli kuwa Mtendaji Mkuu wizara ya Kilimo hapo mwezi Machi mwaka huu.
” Nimekuja hapa Songwe kwa lengo la kufuatilia utendaji kazi wa taasisi zangu za ASA,NFRA na TACRI kwani serikali imetoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo hivyo nataka kuona endapo thamani ya fedha imezingatiwa” alisema Kusaya.
Akiwa mkoani Songwe Kusaya atakagua shamba la mbegu bora la Wakala wa Mbegu (ASA) ,atakagua mradi wa ujenzi wa vihenge vya kisasa chini ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) pia atakagua utendaji kazi wa kituo cha utafitiwa zao la kahawa (TACRI).
Aliongeza kusema ” mimi ni Katibu Mkuu wa Kilimo na wakulima wapo vijijini ndio maana nakuja huku kuonana na wakulima ili kutatua changamoto na kufanya wanufaike na kazi za kilimo” alisema Kusaya.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt.Seif Shekalaghe alisema mkoa wa Songwe unaendelea vema na maandalizi ya msimu wa kilimo wa 2020/21 ambapo halmashauri zote tayari zinahamasisha wakulima kujipanga.
Dkt. Shekalage alisema changamoto iliyopo kwa sasa ni soko la mahindi ya wakulima kutokana na uwepo wa uzalishaji mkubwa msimu uliopita.
” Sisi (Songwe) ni mkoa wa tatu kwa uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula hususan mahindi  nchini ,tunahitaji shilingi Bilioni mbili ili tununue mahindi ya wakulima ambayo tayari yapo vijijini sasa.”alisema Dkt. Shekalaghe.
Akijibu hoja hiyo Katibu Mkuu Kilimo Kusaya alisema sokola mahindi na mazao mengine ya chakula limeathiriwa na tatizo la COVID 19 kwenye nchi nyingi zinazotuzunguka ambapo ndi tegemeo la wafanyabiashara wengi.
Kusaya aliongeza kusema jitihada zinafanywa na wizara ya Kilimo kupata masoko ya uhakika ikiwemo fedha za serikali ili wakulima wapate soko la mazao yao.
” Lengo  la serikali ya awamu ya Tano na maelekezo ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli ni kuhakikisha mkulima anapata uhakika wa soko ili kukuza uchumi wa kaya na taifa. Hivyo wizara itatafuta masoko kwa mazao yote ya wakulima” alisisitiza Kusaya.

No comments :

Post a Comment