Thursday, October 22, 2020

TANZANIA YAPIGA HATUA SEKTA YA AFYA, MAGONJWA YA KIBINGWA SASA YANATIBIWA NCHINI NA WATAALAMU WAZAWA.


Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Edward Mbaga akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari mbalimbali nchini katika mkutano wao na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya leo jijini Dodoma.
Wahariri wa Vyombo Mbalimbali vya Habari nchini wakifuatilia mkutano wao na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bernard Konga leo jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)Bernard Konga akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari leo jijini Dodoma.
 

 Charles James, Michuzi TV


SERIKALI imesema katika kuongeza ubora wa utoaji huduma kwenye sekta ya afya, bajeti ya afya

imeongezwa hadi kufikia zaidi ya Sh Bilioni 200 kwa bajeti ya mwaka 2020/21 kulinganisha na ile ya mwaka 2015/16 ambayo ilikua Sh Bilioni 31.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Idara Kuu ya Sera na Mipango Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Edward Mbaga wakati akifungua mkutano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini.

Mbaga amesema maboresho yaliyofanyika kwenye sekta ya Afya ni makubwa kiasi kwamba imeokoa gharama zilizokua zikitumika kusafirisha wagonjwa kwenda ya nchi kutibiwa na badala yake hivi sasa wanatibiwa nchini.

" Hivi sasa Hospitali zetu zinatoa huduma za kibingwa ambazo awali iliwalazimu wagonjwa kusafirishwa nje ya Nchi, mathalani upandikizaji wa figo, upasuaji wa moyo na ubongo vyote hivyo vinafanyika hapa nchini tena na wataalamu wazawa," Amesema Mbaga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa NHIF, Bernard Konga amewashukuru Wahariri wa vyombo vya habari kwa kukubali kuhudhuria mkutano huo ambao umelenga kukuza mahusiano ya kazi.

" Kuelekea miaka 20 ya kuanzishwa kwa NHIF tumeona tukutana na Wahariri kama ilivyo kawaida yetu ya kukutana na tungependa tubadilishe uzoefu ili tuone namna ambavyo tunaweza kuwafikia watanzania wengi zaidi ili waweze kunufaika na mfuko huu wa Taifa wa Bima ya Afya," Amesema Konga

No comments :

Post a Comment