Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imebaini mchezo mchafu katika mikopo
inayotolewa na halmashauri kwa vikundi.
"Ndugu
waandishi wa habari,nimewaalika kuja hapa ili kupitia kwenu, Watanzania
wote wafahamu kazi zilizofanywa na TAKUKURU Mkoa wa Pwani kwa kipindi
cha mwezi Julai mpaka Septemba, 2020.
"Ikumbukwe
kuwa ni utaratibu wetu kufanya hivyo ili umma wa Watanzania wafahamu
tunafanya nini na watuelewe kwa kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi
ya rushwa nchini.
"Kwa msingi huo naomba kuainisha kazi zilizofanywa na TAKUKURU Mkoa wa Pwani kwa kipindi hicho kama ifuatavyo:
UCHUNGUZI NA MASHITAKA
Kwa
robo hii ya mwaka Ofisi ilipokea malalamiko 318 kati ya hayo malalamiko
157 uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali na malalamiko 74
yalionekana kuangukia katika sheria nyinginezo hivyo walalamikaji
walishauriwa na kuelekezwa sehemu husika kwa lengo la kutatua kero zao.
Aidha,
jumla ya kesi 34 ziliendelea kuendeshwa katika mahakama mbalimbali za
mkoa wa Pwani ambapo kesi 10 zilitolewa hukumu na upande wa Jamhuri
ulishinda kesi 6 kwa washitakiwa kuamuliwa kufungwa jela au kulipa
faini, na kesi 4 watuhumiwa hawakukutwa na hatia na hivyo waliachiwa
huru.
Katika
kushughulikia malalamiko yaliyowasilishwa, ofisi imefanikiwa kuokoa
mali mbalimbali zikiwemo fedha, nyumba na viwanja kama ifuatavyo;-
Ofisi ya TAKUKURU Chalinze
Katika
robo hii ya mwaka, Ofisi hii imefanikiwa kurejesha kiasi cha Shilingi
6,470,000 kwenye akaunti ya Halmashauri ya Chalinze.
Fedha
hizi zinatokana na ukiukwaji wa taratibu za mikopo inayotolewa kwa
vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu uliofanywa na kikundi
cha MIONO SACCOS cha kata ya Miono huko Chalinze kilichokuwa kimekopa
kiasi cha shilingi 9,100,000 toka Halmashauri ya Chalinze.
TAKUKURU
ilibaini kwamba viongozi wa Kikundi hicho cha Miono Saccos yaani
Mwenyekiti na katibu alipokea mkopo huo usio na riba toka Halmashauri ya
Chalinze na wao kwenda kukopesha kwa wafanyabiashara pasipo hata
kuwajulisha wanakikundi wengine kinyume na masharti ya mkopo huo
unaotolewa kwa mujibu wa sheria ya fedha za Serikali za Mitaa Sura 290
kifungu cha 37 (a) (4).
Pia ofisi ilifanikiwa kurejesha kiasi cha Shilingi 1,368,000 kwenye akaunti ya kijiji cha Msoga Kata ya Msoga.
Fedha
hizi zilirejeshwa zinatokana na ubadhirifu wa fedha za mapato
yatokanayo na madini ya ujenzi uliofanywa na aliyekuwa Mtendaji wa
Kijiji hicho cha Msoga.
Kwani
ilibainika kuwa mtendaji huyo wa kijiji alipokea kiasi cha Shilingi
1,368,000 kwa nyakati tofauti kutoka kwa mkusanya ushuru wa kijiji hicho
na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi. Baada ya mtuhumiwa kuhojiwa
alikubali kukabidhiwa fedha hizo na kuomba kuzirejesha na ndipo
alipozirejesha kwenye akaunti ya kijiji cha Msoga.
Ofisi ya TAKUKURU Kibaha
TAKUKURU
mkoa wa Pwani imefanikiwa kurejesha nyumba ya Bi. MAYASA ALLY MMELEKE
iliyokuwa ikishikiliwa na kutaka kuuzwa na Bw. GODLISTEN NDIMBO baada ya
Bi. MAYASA kushindwa kumalizia deni alilokuwa anadaiwa na Bw. NDIMBO.
Awali
ilidaiwa kwamba tarehe 15/09/2019 Bi. MAYASA alikopa Shilingi
3,000,000/= kutoka kwa mkopeshaji na kuweka rehani Hati ya nyumba yake
namba MZR/MKZ/641 iliyopo kitongoji cha MKUZA wilaya ya KIBAHA kwa
makubaliano ya kulipa riba ya shilingi 1,200,000 ambapo mkopaji
angerejesha jumla ya shilingi 4,200,000/=.
Hata hivyo mpaka kufikia mwezi Novemba, 2019 mkopaji alikuwa amesharejesha kiasi cha shilingi 2,400,000.
Aidha, kiasi kilichokuwa kimebaki ndio kilipelekea mkopeshaji kutaka kuuza nyumba ya Bi. MAYASA kitu ambacho ni dhuluma.
TAKUKURU
ilifanya uchunguzi wa kina na kubaini ukiukwaji mkubwa wa sheria
uliofanywa na mkopeshaji kwa kufanya biashara ya ukopeshaji wa fedha
bila kusajiliwa, kinyume kifungu cha 6(1) cha sheria ya mabenki yaani
“Banking and Financial Act” ya mwaka 2006 ambacho kinakataza mtu kufanya
shughuli za kibenki au kutoza riba pasipo kuwa na leseni kutoka benki
kuu.
Pia
mkopeshaji alibainika kukwepa kulipa kodi kutokana na biashara hiyo
anayoifanya kinyume cha Sheria. Mtuhumiwa ameelekezwa kuacha biashara
hiyo mpaka atakapofuata taratibu za kisheria zinazotakiwa.
Ofisi
ya Kibaha pia imefanikiwa kuwasaidia viwanja watumishi wapatao 12
waliokuwa wanadai mishahara kwa kazi ya ulinzi katika kampuni iitwayo
PRC ASSOCIATES SECURITY (T) LTD ya mjini Kibaha. Kwani watumishi hao
walifanya kazi katika kampuni hiyo ya ulinzi kwa takribani miaka mitatu
pasipo kulipwa mishahara yao na kufanya jumla ya deni la mishahara
wanayodai kufikia Shilingi 23,000,000.
Mmiliki
wa kampuni tajwa alipofuatwa na TAKUKURU alionyesha ushirikiano na
kuamua kuwalipa viwanja watumishi wake badala ya fedha chini ya
usimamizi wa serikali ya mtaa na watumishi hao kuridhika na hatua hiyo
kwani walihangaika sana kutafuta haki yao katika sehemu mbalimbali bila
mafanikio yoyote na hatimaye sasa watumishi hao wamelipwa na kupata haki
yao.
Ofisi
pia imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi milioni ishirini na tano
(25,000,000) kutoka kampuni ya MAFUBILO ikiwa ni sehemu ya deni la
wakulima wa korosho wanaounda umoja wa UVUKI wilaya ya Kibaha.
Ofisi ya TAKUKURU Mafia
TAKUKURU
wilaya ya Mafia ilifanikiwa kuokoa shilingi 4,261,675/= ambazo
zilikusudiwa kuchepushwa na baadhi ya watumishi na mawakala katika
Halmashauri ya wilaya ya Mafia wenye dhamana ya kukusanya ushuru kwa
kutumia mashine za kieletroniki “Point Of Sale”.
Aidha kiasi cha shilingi 4,925,000/= zimerejeshwa katika akaunti ya Chama Cha Ushirika wa Korosho na Nazi wilayani Mafia.
Fedha
hizo zilikuwa zimechepushwa na viongozi wa chama hicho ambao kwa sasa
wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi. Hata hivyo uchunguzi wa tuhuma
dhidi ya viongozi hao bado unaendelea.
Ofisi ya TAKUKURU Kibiti
OFISI
imefanikiwa kuokoa bati zipatazo 168 zenye thamani ya shilingi
4,704,000/= zilizotakiwa kuezekwa kwenye madarasa ya shule shikizi ya
msingi ya NYAMBANGALA iliyopo kata ya DIMANI wilaya ya Kibiti.
Awali
ilibainika kwamba mkataba wa ujenzi wa madarasa hayo ulihitaji kuezeka
mabati ya “gauge 28” lakini madarasa hayo yaliyojengwa kwa mtindo wa
“Force Account” yaliezekwa kwa bati za “gauge 32”, hivyo TAKUKURU
iliingilia kati na hivyo kufanyika marekebisho kwa mujibu wa mkataba.
Hujuma
hii ilifanywa kwa njama baina ya Mwalimu Mkuu wa shule aliyekuwa
msimamizi mkuu wa ujenzi huo pamoja na mzabuni aliyepewa kazi ya
kuwasilisha mabati hayo.
Ofisi
imefanikiwa kuokoa na kurejesha fedha taslimu shilingi 64,966,094/
ambazo zimechepushwa na wanunuzi wa korosho (50,000,000/) na nyingine
(14,966.094/ ) zilikuwa zimechepushwa na viongozi wa AMCOS.
Fedha walilipwa wakulima waliokuwa wanadai katika AMCOS za Juhudi, Mwambao na Ruarushe
Ofisi ya TAKUKURU Rufiji
Wakati
huo huo, TAKUKURU kupitia ofisi yetu ya wilaya ya Rufiji tuliweza
kuokoa kiasi cha shilingi 2,500,000 kutokana na tozo za kodi kutoka kwa
mfanyabiashara JAFARI MCHEKWA aliyekiuka taratibu za uvunaji wa mazao ya
misitu kwa kuvuna magogo ya mti wa mkuruti katika maeneo yasioruhusiwa.
Fedha za faini hiyo tayari zimekwishaingizwa katika akaunti ya Mtendaji wa wakala wa misitu Tanzania.
TAKUKURU
wilaya ya Rufiji tuliweza kuokoa kiasi cha shilingi 1,264,500/
kilichotokana na ukiukwaji wa taratibu uliofanywa na maafisa wa
halmashauri ya wilaya ya Rufiji kufanya ukadiriaji mdogo wa ujazo wa
magogo yaliyokua yanapigwa mnada katika kijiji cha NYAMWAGE, kwani
ilibainika kuwa ujazo uliowasilishwa na maafisa wa Halmashauri ulikua na
meta za ujazo 21 badala ya 25.5 zilizopatikana baada ya TAKUKURU
kuingilia kati na kufanya upimaji upya kwa kushirikiana na ofisi ya
wakala wa misitu nchini, na hivyo kufanikiwa kupata ongezeko la meta za
ujazo 4.5 zilipelekea kijiji kujipatia fedha za ziada shilingi 1,264,500
baada ya mauzo.
Pia,
kiasi cha Shilingi 900,000/= kiliokolewa kutokana na malipo hewa ya
mauzo ya korosho yaliyolipwa kwa mfanyabiashara ABDALLAH GOCHI kinyume
na taratibu kwani hakustahili kupata malipo hayo, hivyo TAKUKURU
iliingilia kati na kuamuru mfanyabiashara huyo kurejesha fedha hizo ili
mhusika aliyestahili malipo hayo aweze kupata haki yake.
Katika
kipindi hicho hicho TAKUKURU Wilaya ya Rufiji ilifanikiwa kurejesha
shilingi 1,200,000 ambazo maafisa ardhi wilaya ya Rufiji ambao ni
MASHAKA ABDALAH na OMARY MAZORA walijipatia kwa njia zisizo halali kwa
kuuza viwanja vya halmashauri bila mwajiri wao yaani Mkurugenzi Mtendaji
wa Halmashauri kujua.
Pia
tuliweza kukamilisha urejeshwaji wa fedha kiasi cha shilingi
12,000,000/- kwa mwalimu mstaafu YUSUPH RASHID KIMWERI ambazo alikuwa
amemlipa Bw. IBRAHIM MAREMA MASWE kupitia akaunti yake. Fedha hizi
zinatokana na mkopo umiza uliokopeshwa kwake wa Tshs. 700,000/- na hivyo
kutakiwa kurejesha Tshs. 13,000,000/- zikiwa ni fedha alizokopeshwa
Tshs. 700,000/- pamoja na riba ya mkopo huo.
Ofisi ya TAKUKURU Kisarawe
Kupitia
Ofisi ya TAKUKURU wilaya ya Kisarawe tuliweza kumsaidia mwananchi
mnyonge Bi. KHADIJA BANI mkazi wa mtaa wa Bomani wilayani Kisarawe
kulipwa kiasi cha shilingi 12,500,000.
Fedha
hizi ni sehemu ya Shilingi 26,000,000/= alizotakiwa kulipwa kama fidia
ya mazao katika shamba lake lililochukuliwa na kampuni ya RAK KAOLIN Co.
LTD mwaka 2016. Shamba hilo lilichukuliwa kwa shughuli za uchimbaji wa
madini ya Kaolin lakini haikumlipa fidia mama huyo aliyetwaliwa shamba
lake mpaka TAKUKURU ilipoingilia kati ndipo wakamlipa kiasi hicho na
kuahidi kumalizia kiasi kilichobaki ndani ya mwezi huu Oktoba, 2020.
Kwani
sheria za uchimbaji madini zinamtaka mwekezaji kulipa fidia za wote
walioathirika na mradi huo kabla shughuli ya uchimbaji haijaanza, kitu
ambacho kampuni tajwa ilikiuka.
Ofisi ya TAKUKURU Mkuranga
Kupitia
Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mkuranga tuliweza kuwarejeshea wakulima wa
chama cha Msingi cha KIMANZICHANA KUSINI kiasi cha Shilingi 34,081,840/=
ambazo walikuwa wamedhulumiwa na Viongozi wa Bodi ya AMCOS na kampuni
ya COFEE TRADERS.
Aidha
shilingi 7,753,000/=ziliokolewa kutoka kwa viongozi wa Bodi wa vyama
vya msingi vya KISEGESE, KILIMAHEWA KASKAZINI na MUUNGANO ambazo
zilikuwa mali ya wakulima. Fedha hizo zilitokana na mauzo ya korosho
msimu wa 2018/2019. Utaratibu wa kuwarejeshea wakulima husika
unaendelea.
TAKUKURU
wilaya ya Mkuranga pia ilifanikiwa kurejesha kwenye akaunti ya
Halmashauri kiasi cha Shilingi 930,000/= kutoka kwa Bw. SHABAN MPONDA,
Afisa Mtendaji wa Kata ya Vikindu.
Fedha
hizo alizikusanya kutoka kwa watendaji wa vijiji kwa ajili ya ujenzi wa
Ofisi ya Kata lakini mtendaji huyo alizifanyia ubadhirifu.
Aidha
tuliweza kufanikisha kufufuliwa kwa mradi wa maji wa Shule ya Sekondari
PANZUO mradi ambao ulikufa tangu mwaka 2017 baada ya Mkandarasi SEBA
CONSTRUCTION & DRILLING CO.LTD kutumia “solar panel” na “pump”
ambazo hazikuwa na ubora.
Hivyo
TAKUKURU ilianzisha uchunguzi kujua kwanini mkandarasi hakufuata
matakwa ya mkataba uliomhitaji kuweka vifaa vyenye ubora kitu
kilichopelekea mradi kushindwa kutoa maji kama ilivokusudiwa, lakini
baada ya TAKUKURU kuingilia kati tulimtaka mkandarasi kufanya
marekebisho yaliyotakiwa kwa kuzingatia mkataba wa kazi aliopewa na
serikali, hivyo basi, mkandarasi alifanya marekebisho na sasa mradi
unafanya kazi na maji yanatoka katika shule hiyo ambapo Shilingi
32,296,600/= zilitumiwa na mkandarasi ili kufanya marekebisho hayo.
Kwa
hiyo mkoa wa pwani kwa robo hii tumefanikiwa kuokoa mali na fedha
taslimu zenye dhamani ya shilingi 243,120,709/= ( milioni miambili
arobaini na tatu mia moja na ishirini elfu, mia saba na tisa).
ELIMU KWA UMMA.
Ndugu waandishi wa habari,
Katika
kipindi hicho tumeweza kuelimisha jumla ya wananchi 6,224 kupitia
semina 74, mikutano 62, maonesho 2 na vipindi 6 vya redio. Pia kwa
kufungua klabu za wapinga rushwa 18 na kuimarisha klabu zipatazo 71
Elimu
tuliyotoa ilihusu Madhara ya Rushwa katika chaguzi za kisiasa kwani
mnatambua kuwa nchi yetu ipo katika mchakato kuelekea uchaguzi mkuu wa
Rais, wabunge na madiwani mwezi huu kwahiyo wananchi ni lazima wapate
elimu ya madhara ya Rushwa katika uchaguzi na kuwajengea uwezo wa
kuchagua viongozi waadilifu watakaosaidia nchi katika kuleta maendeleo
ya kweli.
Pia
elimu ya Rushwa ya Ngono ilitolewa kupitia kampeni yetu ya VUNJA UKIMYA
KATAA RUSHWA YA NGONO yenye lengo la kuondoa kero ya rushwa hii kwa
jamii hasa katika vyuo vya elimu ya juu na mashuleni ambako waadhirika
wakubwa wa rushwa hii ni ndugu zetu akina dada. Aidha tulitoa elimu juu
ya “Wajibu na ulinzi wa mwananchi katika mapambano dhidi ya Rushwa”,
UZUIAJI RUSHWA
Katika
eneo la Uzuiaji Rushwa tulifanya uchambuzi wa mifumo 12 katika maeneo
Mbalimbali ambayo ni; Ukusanyaji wa mapato yatokanayo na huduma (Service
Levy), pia tulichambua mfumo wa upatikanaji wa leseni za biashara
zitolewazo na Halmashauri za wilaya ili kubaini mianya ya rushwa na
kutafuta mbinu za kuziba mianya hiyo.
Baadhi
ya mianya iliyobainika katika uchambuzi wa mfumo wa ukusanyaji wa
mapato ni pamoja na wafanyabiashara wengi kutokuwa na elimu ya huduma ya
“service levy” kama ilivyo kwa ada, ushuru na kodi nyinginezo. Na
katika uchambuzi wa mfumo wa upatikanaji wa leseni za biashara tulibaini
kuwa wafanyabiashara wengi wanafanya biashara zao pasipo kuhuisha
leseni zao za biashara na kuipotezea mapato serikali na pia kuna
wafanyabiashara wanaopewa notisi za kulipia leseni zao lakini hawafanyi
hivyo na kuendelea na biashara.
Na
katika kufuatilia wafanyabiashara wasiolipa service levy, kuna
mfanyabiashara mmoja alikaidi kulipa kwa muda mrefu lakini baada ya
TAKUKURU kufuatilia alikimbia na kwenda kulipa mara moja kiasi cha
shilingi 18,218,420.37 na hivyo kuiingizia fedha Halmashauri ya mji wa
Kibaha. Hayo ni baadhi ya matunda ya chambuzi za mifumo tunazofanya
katika utendaji wetu
UFUATILIAJI WA MIRADI
Ndugu waandishi wa habari,
Mtakumbuka
kuwa ni jukumu la TAKUKURU kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo katika
nchi yetu inakuwa na tija na kuleta matunda yaliyokusudiwa. Katika robo
hii ya mwaka tumekagua jumla ya miradi ya maendeleo 16 katika sekta za
elimu, afya, na ujenzi, Miradi hiyo ina thamani ya shilingi Bilioni
tatu, milioni mia tisa therathini na tano, laki nane tisini na moja elfu
mia tatu na arobaini na senti hamsini na tano (Shilingi
3,935,891,340.55). Aidha, katika ufuatiliaji wa miradi hiyo baadhi ya
miradi ilibainika kuwa na udhaifu katika usimamizi wa sheria, kukosekana
kwa elimu kwa walipa ushuru, udanganyifu katika utoaji wa taarifa za
mapato katika biashara, wafanyabiashara wengi kutolipa ushuru wa huduma
(Service Levy), na katika baadhi ya miradi ilibainika kuwa na mapungufu
yaliyotokana na manunuzi ya vifaa vingi kuliko uhalisia na kukiuka
taratibu za manunuzi hivyo uchunguzi umeanzishwa kwa lengo la kupata
hasara iliyotokana na manunuzi hayo, na watakaobainika kuhusika
watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
MIKAKATI YETU KWA KIPINDI CHA OKTOBA HADI DISEMBA 2020
Kama
ilivyo dira ya Taifa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na
madiwani mwaka huu, mikakati ya mkoa wa Pwani ni kuhakikisha uchaguzi
huu unafanyika pasipokuhusisha vitendo vya Rushwa kwa kufanya yafuatayo;
Kufikisha
elimu ya madhara ya Rushwa kwa wananchi wote mpaka ngazi ya kijiji ili
waone umuhimu wa kuchagua viongozi waadilifu watakaokuwa mstari wa mbele
katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wakati wa uchaguzi. Na
kuwajengea uwezo wananchi kutambua viongozi sahihi wenye nia ya dhati ya
kumkomboa mtanzania, viongozi watakaokuwa mstari mbele kuunga mkono
mapambano dhidi ya Rushwa na ufisadi.
Kufanya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazotufikia, zikiwemo tuhuma za rushwa katika Uchaguzi kwa lengo la kupata ushahidi.
WITO WA TAKUKURU KWA WANANCHI
Ndugu waandishi na wananchi,
"Naomba
kutumia fursa hii kuwasihi wananchi wa mkoa wa Pwani na watanzania kwa
ujumla kutumia haki yenu ya kupiga kura hapo tarehe 28/10/2020 kwa
kuchagua viongozi wasiojihusisha na vitendo vya Rushwa. Aidha mwananchi
unaweza kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa TAKUKURU kupitia namba za
BURE 113 AU kwa ujumbe mfupi wa simu kwa kupiga *113# kisha fuata
maelekezo,"Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani,Suzana Raymond amefafanua kwa
kina leo Oktoba 16,2020 mkoani humo.
No comments :
Post a Comment