Friday, October 9, 2020

“Shiriki Maonesho ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania Kupanua Ujuzi” Mhe Ole Sanare


***************************

Morogoro- Tarehe 9 Oktoba, 2020

Mkuu wa Mkoa wa Morogogo, Loata Ole Sanare amewasihi wamiliki wa viwanda kwa mkoa wa

Morogoro kushiriki kwenye Maonesho ya tano ya bidhaa za viwanda vya Tanzania ili kuweza kupanua ujuzi wa kuviendesha viwanda na pia kutumia fursa ya kukutana na wamiliki na wenye viwanda kutoka mikoa mingine wakati wa maonesho.

Hayo yamesemwa leo tarehe 9 Oktoba, 2020 kwenye kikao cha kujadili ustawi wa maendeleo ya viwanda kwa mkoa wa morogoro uliokutanisha wamiliki wa viwanda kwa mkoa huo na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).

Ameendelea kusema kuwa uwekezaji kwenye viwanda umepewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dr. John Pombe Joseph Magufuli ambapo utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda (1996 – 2020) ambayo malengo yake ni kuiwezesha Sekta ya Viwanda kuchangia katika kufikia Malengo ya Maendeleo ya muda mrefu kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, lengo ni ujenzi wa viwanda ili kulifikisha Taifa letu kwenye uchumi wa Kati ambao tumeshaufikia.

Amehimiza wawekezaji kuanzisha viwanda hususan vidogo vidogo vya kusindika mazao ya Kilimo, Mifugo na uvuvi ili kupanua wigo wa ajira kwa wananchi wetu na amewaelekeza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wawekezaji kwenye maeneo yao kujadili kila mara changamoto wanazokutana nazo ili kuboresha uwekezaji nchini.

Nae Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Biashara kutoka TanTrade Bw Boniface Michael amewaeleza wamiliki wa viwanda kwa mkoa wa Morogoro kutumia jukwaa la Maonesho ya tano ya bidhaa za viwanda vya Tanzania yanayoandaliwa na TanTrade ili kupanua wigo wa masoko nje ya mkoa wa Morogoro ili kuimarisha soko la ndani, kutambulisha bidhaa wanazozalisha kwa Watanzania ili kuchochea uzalishaji, kuwaunganisha wenye viwanda na wazalishaji mbalimbali wa malighafi na huduma zingine zinazotumika viwandani na kuwaunganisha wenye viwanda na wasambazaji wa teknlojia ya viwanda.

Maonesho haya yamebeba kauli mbiu ya “Tumia Bidhaa za Tanzania, Jenga Tanzania” ili kuhamasisha Watanzania waendelee kupenda, kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda nchini na yanatarajiwa kufanyika tarehe 3 hadi 9 Desemba, 2020 katika uwanja wa Maonesho wa Mwl J.K.Nyerere Barabara ya Kilwa Dar es Salaam.

 

No comments :

Post a Comment