Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dk. Donald J. Wright, katika hafla iliyofanyika katika makazi yake jijini Dar es Salaam, alitoa ruzuku kwa asasi za kiraia, taasisi zisizojiendesha kibiashara na taasisi za kidini zilizosajiliwa zipatazo 13 kutoka pande zote za Tanzania. Ruzuku huyo ilitolewa kutoka katika Mfuko wa Balozi wa Marekani wa Kusaidia Mapambano Dhidi ya
Ukimwi (AFHR) ili kutekeleza miradi ya kukabiliana na VVU nchini.
Fedha zinazotolewa na mfuko huu hutolewa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR), ambao unawasilisha ahadi na dhamira ya dhati ya Serikali ya Marekani ya kukabiliana na janga la VVU/UKIMWI. Mpango huu bado unaendelea kuwa mpango mkubwa zaidi kuwahi kutekelezwa na nchi yoyote duniania katika kukabili ugonjwa wa aina moja. Toka kuanzishwa kwa PEPFAR hapo mwaka 2003, Serikali ya Marekani imechangia zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 4.6 kukabiliana na VVU nchini Tanzania pekee.
Wapokea ruzuku waliwasilisha maombi na maandiko yao ya miradi kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu VVU/UKIMWI katika jamii zao. Miradi iliyopendekezwa ililenga kuongeza uelewa kuhusu VVU, kuimarisha upatikanaji wa huduma miongoni mwa watu wanaoishi na VVU, yatima na watoto walio katika mazingira hatarishi pamoja na makundi ya ya watu walio katika hatari zaidi ya kuambukizwa ikiwemo wanaume na vijana wa kiume, wasichana na vijana wa kike.
Miradi iliyoshinda na kupatiwa ruzuku inalenga katika vipaumbele vya kimkakati ikiwa ni pamoja na kuinua ufahamu kuhusu tiba miongoni mwa watu wanaoishi na VVU; kupunguza unyanyapaa na ubaguzi; mbinu bunifu za kupunguza ukatili wa kijinsia na upatikanaji wa huduma kwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia; kuwafikia na kuwahimiza wanaume kupima VVU na kuwaunganisha na huduma za matibabu; na kuinua ubora wa huduma za kukabiliana na VVU kwa kupitia ufuatiliaji unaoendeshwa na jamii (community-led monitoring).
Toka kuanzishwa kwake mwaka 2009, Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI (AFHR) umeshatoa ruzuku kwa asasi za kijamii ma taasisi za kiraia zipatazo 130 nchini Tanzania. Marekani ina fahari kuendelea kuwa mbia imara wa asasi na taasisi hizi ili kufikia malengo ya Tanzania ya kudhibiti VVU.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na Kitengo cha Habari cha Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kwa simu: +255 22 229-4000 au barua pepe: DPO@state.gov.
Wapokea Ruzuku kutoka katika Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI kwa mwaka 2020:
- Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa BAKWATA utashughulikia vikwazo mbalimbali vinavyowafanya watu wanaoishi na VVU kuacha kuendelea kutumia dawa (ARVs) kwa kuimarisha mitandao ya watu wanaoishi na VVU kupitia waelimisha rika (peer educators) kwa ushirikiano na wahudumu wa afya katika wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma.
- Chimaba Sanaa itaimarisha uelewa kuhusu matibabu kwa kutumia dawa za kufubaza VVU (ARVs) na kuongeza kiwango cha wanaume na vijana wa kiume wanaoishi na VVU, pamoja na wenza wao kutumia dawa hizo bila kukoma katika wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya.
- Development for All (DEFOA) itainua ubora wa huduma kwa watu wanaoishi na VVU wanaopatiwa dawa za kufubaza VVU (ARVs) katika vituo vya afya kwa kupitia watoa huduma za afya ndani ya jamii (Community health workers) na walengwa wenyewe.
- Foster Community Creative Solutions (FCCS) itaongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kupima VVU; kuanza matibabu ya dawa za Kufubaza VVU (ART) kwa kutumia dawa mchanganyiko za TLD miongoni mwa wakulima wadogo wadogo na wafugaji na kuinua ujuzi wa kutoa matibabu yanayohusisha dawa za kufubaza VVU miongoni mwa Watoa Huduma za Afya wa Jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
- Katandala HIV/AIDS Free Club (KFC) itafuatilia ili kuboresha huduma zitolewazo kwa watu waishio na VVU wanaopa dawa za kufubaza VVU (ARVs) katika Kituo cha Afya cha Usevya kwa kutumia mbinu ya kuishirikisha jamii katika kutathmini huduma zitolewazo (community score card approach).
- Kilio cha Waathirika na Waathiriwa UKIMWI Tanzania (KIWWAUTA) itapunguza kiwango maambukizi mapya kwa makundi ya watu walio katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya VVU.
- Participatory Development Concern (PADECO) itafuatilia ili kuboresha huduma zitolewazo kwa watu waishio na VVU wanaopa dawa za kufubaza VVU (ARVs) katika Kituo cha Afya kwa kutumia mbinu ya kuishirikisha jamii katika kutathmini huduma zitolewazo (community score card approach).
- Social Action Trust fund (SATF) itaboresha maisha ya yatima na watoto walio katika mazingira hatarishi pamoja na walezi wao na kuwezesha upatikanaji wa huduma bora kwao kwa kuwajengea uwezo na kufanya ushawishi.
- SHDEPHA+ MPANDA itaongeza idadi ya watu wazima na vijana wa kiume walio katika hatari ya maambukizi ya VVU wanaojua hali zao za kiafya kuhusu maambukizi ya VVU kwa kuendesha upimaji wa VVU katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi lakini yasiyopata huduma za kutosha katika mkoa Katavi.
- Hospitali Teule ya Wilaya ya SUMVE itatoa elimu ya VVU/UKIMWI kuhusu matibabu kwa kutumia dawa za kufubaza VVU, matumizi ya dawa mseto ya Tenofovir, Lamivudine, na Dolutegravir (TLD) na ngono salama kwa vijana wa kuanzia umri wa miaka 15 -24 katika mashule, vituo vya afya na jamii kwa ujumla.
- Tanzania Health Promotion Support (THPS) itaboresha huduma za kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa jamii na kuboresha huduma za kinga na matibabu katika vituo vya afya katika wilaya ya Mkuranga, Mkoani Pwani.
- Umbrella of Women and Disabled Organization (UWODO) itaimarisha upatikanaji wa huduma za upimaji wa VVU kwa wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu katika wilaya ya Makambako Mjini, na kuhakikisha kuwa makundi hayo yanapewa elimu kuhusu huduma za matibabu pamoja na kuunganishwa na huduma hizo.
- Tanzania Youth Behavior Change Organisation (TAYOBECO) itajenga uelewa kuhusu matumizi ya dawa mchanganyiko ya Tenofovir, Lamivudine, na Dolutegravir (TLD) kama tiba ya mwanzo inayopendekezwa wa watumiaji wa ARV na kukufa ufahamu kuhusu tiba inayopendekezwa sasa kwa kuzingatia miongozo ya utoaji huduma ya dawa za kufubaza makali ya VVU kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizewa VVU katika wilaya 5 za mkoa wa Dar es salaam.
Kufahamu zaidi kuhusu Mfuko wa Balozi wa Kukabiliana na VVU/UKIMWI, tafadhali tembelea tovuti ya PEPFAR Tanzania (https://tz.usembassy.gov/our-relationship/pepfar/) au wasiliana na Mratibu wa PEPFAR anayeshughulikia Asasi za Kiraia (Civil Society Outreach Coordinator) kwa barua pepe: PEPFARGrantsDar@state.gov
No comments :
Post a Comment