Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akinyanyua bendera kuashiria uzinduzi rasmi wa programu ya ugawaji wa mbolea kwa wakulima katika ofisi za Kampuni ya YARA Tanzania jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (wa pili kushoto) wakizungumza na Balozi wa Norway nchini, Elisabeth Jacobsen (wa pili kulia) baada ya Waziri mkuu kuzindua rasmi programu ya ugawaji wa mbolea kwa wakulima katika ofisi za Kampuni ya YARA Tanzania jijini Dar es Salaam, Oktoba 11, 2020. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya YARA Tanzania, Winstone Odhiambo na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
……………………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA WIZARA YA KILIMO
*Ni kuhusu mbolea iliyotewa bure na kampuni ya YARA
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Kilimo ihakikishe mbolea iliyotolewa
bure kwa wakulima wadogo inawafikia na kuwanufaisha wahusika kama lengo la kampuni ya YARA lilivyokusudia.
Akizungumza wakati alipozindua rasmi mpango wa ugawaji wa mbolea bure kwa wakulima katika Ofisi za Kampuni ya YARA Tanzania jijini Dar es salaam leo (Jumapili, Oktoba 11, 2020) Mheshimiwa Majaliwa ameishukuru kampuni hiyo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwasaidia wakulima wadogo nchini.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Wizara ya Kilimo inapaswa ihakikishe mbolea hiyo inawafikia walengwa ambao ni wakulima wadogo na atakayebainika kujinufaisha kinyume na utaratibu wa ugawaji mbolea hiyo atakuchukuliwa hatua.
“Nawasihi Wizara ya Kilimo msimamie ugawaji wa mbolea hii na nisingependa kusikia kuwa baadhi ya watu wasiowaaminifu wanajinufaisha kwa kuwauzia wakulima mbolea hii. Serikali ya Tanzania imejizatiti katika kukuza na kuboresha kilimo nchini kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania ni wakulima.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema idadi kubwa ya wakulima wanaokadiriwa kuwa asilimia 75 ni wale wenye uwezo wa kulima hekari moja hadi tano na sababu kubwa ikiwa ni uwezo mdogo wa kumudu gharama hasa pembejeo na viuatilifu.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumshukuru Balozi wa Norway nchini, Balozi Elisabeth Jacobmsen kwani Kampuni Mama ya YARA makao yake makuu yako nchini Norway na kwa vyovyote vile Balozi huyo kachangia kuhakikisha programu hiyo ya ugawaji wa mbolea inafanikiwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema lengo kuu ya programu ya ugawaji mbolea bure kwa wakulima ni kuongeza tija kwa uzalishaji wa mazao ya chakula hasa mahindi na mpunga.
Amesema mbolea hiyo imefanyiwa utafiti na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kuthibitishwa kuwa inafaa kwa matumizi katika mazao ya mahindi na mpunga nchini na inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mazao hayo.
Mheshimiwa Hasunga amesema wakulima wadogo wanaolima hekari moja hadi mbili wapatao 83,000 wanatarajiwa kunufaika na programu hiyo katika mikoa 25 ya Tanzania Bara ukiondoa mkoa wa Dar es Salaam ambao umeondolewa kwa sababu hauna idadi kubwa ya wakulima.
Naye Balozi wa Norway nchini, Balozi Elisabeth amesema ni jambo muhimu kuwasaidia wakulima wadogo hasa katika kipindi hiki tunapoelekea msimu wa kupanda mazao kwani wakulima wanahitaji kupata mbolea kwa wakati.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya YARA Tanzania, Bw. Winstone Odhiambo katika hotuba yake amesema mbolea itakayogawiwa ni aina NPK tani 12,500 yenye thamani ya shilingi bilioni 16.5.
Amesema utaratibu unaotumika kuwapata wanufaika wa mbolea hiyo ni kwa wakulima kujisajili kwa kupiga *149*46*16# na amewaomba wakulima waendelee kujisajili kwa wingi.
No comments :
Post a Comment