Friday, October 23, 2020

MABADILIKO YA TABIA NCHI YAENDELEA KUIKUMBA DUNIA


KATIKA kipindi cha miezi michache iliypopita, dunia imekuwa na mabadiliko makubwa ya tabianchi kiasi ambacho hakikutarajiwa.

Kufuatia mabadiriko hayo, Umoja wa Ulaya (EU) utashirikiana na Tanzania

na kuunga mkono juhudi zake katika kuleta maendeleo yanayozingatia mazingira ambayo yatahakikisha uchumi unakuwa na mustakabali imara na wenye faida kwa wote.

Kutekeleza hill, EU imezindua Mpango wa Kijani wa Ulaya ukiwa na mkakati wa ukuaji wenye malengo makubwa ambao unakusudia kupambana na changamoto kubwa za tabianchi na mazingira ambazo zinatukabili. 

Licha ya kukumbwa na janga la COVID-19 tayari dunia ilikuwa imeishabadilika kwa namna ambayo isingeweza kutegemewa kwani teyari dunia ilikuwa imeanza kuyumba kwenye maendeleo kuelekea mustakabali endelevu.

Katika taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Ulaya wa Ushirikiano wa Kimataifa Jutta Urpilainen imeeleza kuwa, teyari dunia ilikuwa inakabiliwa na matatizo yanayohusiana na tabianchi, upotezaji wa bioanuwai na uchafuzi wa mazingira na hivyo kulihitajika kuchukuliwa kwa hatua ili  kurudisha maelewano kati ya dunia na uchumi.

 "Mafanikio yetu yatategemea kuungana na nchi mbalimbali tunazoshirikiana nazo kupitia ushirikiano wa kimataifa, pamoja na makubaliano ya biashara na mipango ya kimazingira." Imeeleza taarifa hiyo.

Amesema, ili kufanikisha hilo kunahitajika washirika na ushirikiano, na kwamba ushirikiano muhimu ni ule uliopo kutoka kwa jirani yetu wa karibu, bara pacha na mshirika wa miaka mingi: Afrika. Umoja wa Ulaya (EU) na bara la Afrika zinahitaji kuchagua mustakabali usioongeza hewa ukaa, matumizi bora ya rasilimali, na wenye kuweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.

"Tunaweza kufanikisha hilo kwa kuwa na ushirikiano thabiti wa kimataifa wenye malengo makubwa..., Hii inamaanisha kupendekeza hatua jumuishi zinazokabiliana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, na kuzingatia masuala ya kiuchumi na kijamii". Amesema Urpilainen

Ameongeza kuwa, kunapaswa kuwekwa mkazo juu ya kuwa na maendeleo ya haraka katika maeneo yenye uwezo wa kuwa na faida kubwa kwa mabara yetu,  nishati endelevu na mifumo ya chakula, kulinda bioanuwai kwa kurejesha mifumo ya ikolojia, kupambana na usafirishaji haramu wa nyara za wanyamapori, na usimamizi endelevu wa misitu, ardhi na maeneo ya hifadhi. 

Akitolea mfano mradi  wa Eco-Boma nchini Tanzania, amesema, wamejenga mfumo wa kukabiliana na tabianchi kwa wafugaji wakati dunia inapambana na janga la afya, na athari zake, ushirikiano wa kimazingira kati ya Afrika na Ulaya utakuwa muhimu katika miaka ijayo. 

Pia wamewajengea uwezo jamii ya Kimasai kwa kuboresha upatakinaji wa maji kwa ajili ya mifugo, usimamizi wa nyanda za malisho, huduma za afya za mifugo, kilimo kinachostahimili ukame, nishati na elimu ya mabadiliko ya tabianchi.

Jambo moja la uhakika ni kwamba mabadiliko ya kimazingira yatahitaji uwekezaji mkubwa. Fedha za umma pekee hazitatosha. Hii ndio sababu ambayo tunashughulikia kupunguza athari za uwekezaji ili kuwezesha ushiriki mkubwa zaidi wa sekta binafsi barani Afrika na kuunga mkono maendeleo yanayozingatia mazingira kwa wote.

 

No comments :

Post a Comment