Monday, October 19, 2020

LUGHA YA KISWAHILI YAZIDI KUPAA ,YAANZA KUFUNDISHWA SHULENI NCHINI BOTSWANA

(Na Lilian Shembilu – MAELEZO)

Kiswahili ni lugha ya kibantu inayozungumzwa katika nchi za Afrika Mashariki, Afrika ya Kati 

na baadhi ya nchi za Falme za Kiarabu. Nchi za Afrika Mashariki zinazotumia lugha hii kwa wingi ni pamoja na Tanzania ambayo inatumia Kiswahili kama  lugha rasmi ya mawasiliano huku ikitumika kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi na kama mojawapo ya kipindi katika shule za sekondari.

Aidha, Kiswahili kinatumika katika nchi za Uganda na Kenya kama lugha ya mawasiliano na pia inatumika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nchi nyingine zinazotumia lugha hii ni Uganda, Kenya, Burundi, Msumbiji, Oman, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Afrika ya Kusini ikizungumzwa na watu takribani milioni 98.

Akithibitisha kukua na kupanuka kwa lugha ya Kiswahili Duniani, Profesa Mshiriki na Mgoda, Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Nyerere katika Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Aldin Mutembei anasema makala yake ya “Kiswahili kama lugha ya Mawasiliano mapana barani Afrika”, aliyoiwasilisha mapema mwezi Februari mwaka huu katika mkutano wa lugha za Afrika uliofanyika jijini Paris, Ufaransa kuwa Kiswahili ni lugha ya 10 kutumiwa Duniani na katika nchi za Afrika inatumiwa na watu milioni 224.9.

Msukumo wa kuenea kwa Kiswahili katika nchi za maziwa makuu, unatajwa na  Mtaalamu wa lugha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mugyabuso Mulokozi katika makala yake ya “Mustakabali wa Kiswahili katika Ukanda wa Maziwa Makuu “, kuwa ni pamoja na sababu za kiuchumi hasa biashara na ajira, kisiasa, vita na sababu za kiutamaduni hasa shughuli za dini, sanaa, michezo na elimu, ambapo anaongeza kusema kuwa, “ Kiswahili kilienea kwa sababu kilihitajika”.

Hata hivyo, Kiswahili ni lugha rasmi Tanzania, Uganda na Kenya na inatumika kama lugha ya mawasiliano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, lugha ya Kiswahili ilikubaliwa kuanza kutumika katika Umoja wa Afrika kuanzia Julai, mwaka 2004 na pia lugha hii inatumika katika Bunge la Afrika. 

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imekuwa mshirika mkuu  wa biashara ikiwa na nchi nyingi zinazozungumza Kiswahili, jambo ambalo Botswana inalihitaji kwani inataka uchumi wake kukua kutokana na biashara za nje ya nchi.

Kiingereza, Kifaransa na Kireno na Kiswahili ndizo lugha nne rasmi zinazotumika SADC kwa sasa.

Botswana imeingia kwenye orodha ya mataifa ya Afrika ambayo yametangaza kuwa yataanza kufundisha Kiswahili shuleni, ambapo ikianza kuifundisha lugha hiyo itakuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika inayotumiwa na watu wengi kuzungumzwa nchini humo.

“Tunataka watoto na raia wa nchi hii waifahamu lugha ambayo inaendelea kukua kwa kasi ya Kiswahili. Mataifa yaliyo kwenye eneo la Maziwa Makuu yanaendelea kuwa na ushawishi mkubwa wa kiuchumi na hatuwezi kushirikiana nao bila ya kuifahamu lugha yao,” alisema Waziri wa Elimu ya Msingi nchini Botswana, Fidelis Molao.

Mpango huo wa kufunza Kiswahili nchini Botswana unafuata mkondo wa Afrika Kusini ambako Kiswahili kinafunzwa kama lugha ya ziada baada ya Kingereza na Kiafrikana.

Mbali na Kenya na Tanzania, Kiswahili kinazungumzwa pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Uganda, Kaskazini mwa Malawi, Msumbiji, Zambia, Madagascar, Ethiopia na Comoros.

Lugha ya Kiswahili inafunzwa pia katika vyuo vikuu vingi ulimwenguni. Kwa upande wa Marekani zaidi ya vyuo 100 vya elimu ya juu vinafundisha lugha ya Kiswahili kwa mfano vyuo vinavyofundisha Kiswahili ni Harvard, Yale, Stanford na Princeton.  Kiswahili pia kinafundishwa kwenye nchi mbalimbali duniani kwa mfano,  Uingereza, Ujerumani, Canada, Poland, Mexico, Urusi, Japan, China, India na Australia kati ya mataifa mengine mengi.

Kutokana na Kiswahili kupata nafasi ya kufundishwa katika shule na vyuo mbalimbali duniani, walimu na wataalamu wa lugha hii wanapata fursa ya pekee ya kufundisha katika nchi mbalimbali ambazo zimeamua kujifunza lugha hiyo, hivyo ni sahihi kusema kuwa lugha hii inaweza kutumika kama bidhaa. 

Umuhimu wa Kiswahili unazidi kuisukuma Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), kuhakikisha kuwa lugha hiyo inatumika zaidi kwa ufasaha na kubidhaishwa ulimwenguni kote.

MWISHO

 

No comments :

Post a Comment