Friday, October 9, 2020

Jengo jipya la biashara la “Michenzani Mall” kuinua uchumi wa Zanzibar

https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2020/10/DSC_6918-scaled.jpg

Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein (wa pili kushoto) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi akijumuika na Viongozi mbalimbali kuzindua Jengo la “Michenzani Mall”la ZSSF kwenye viwanja vya Mapinduzi Square, Michenzani Mjini Zanzibar Visiwani humo. (Na Mpigapicha Wetu)

Na Christian Gaya, Majira Ijumaa 09 Oktoba. 2020 

Majengo ya biashara yana mchango mkubwa kwa upande wa uchumi, kijamii, kisiasa, na kiutamaduni. Majengo ni alama au ishara ya maendeleo na ustawi wa jamii katika nchi yeyote

ile.

Ndiyo maana Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesema kuwa majengo ya biashara kama “Michenzani Mall” hayajengwi kwa ajili ya shughuli za kuuza na kununua vitu peke yake, bali yanajumuisha huduma za kijamii zinazohusiana na elimu, afya, urembo, manukato, burudani na kadhalika.

Dkt.Shein alisema hayo wakati wa ufunguzi wa jengo jipya la biashara la “Michenzani Mall”, hilo la “Michezani Mall” liliopo Jijini Zanzibar, lililojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).

Rais Shein alisema ya kuwa, eneo hilo kabla, ilikuwa hujaa makontena ya biashara ambayo hayakuwa na mpangilio maalumu, kwamba ndipo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya saba kwa kushirikiana na ZSSF, ilipofikiria kuwawekea wananchi wake mazingira bora ya kuvutia ya kufanya biashara za aina mbalimbali.

“Sekta ya biashara ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi na sekta hiyo ina uwiano mkubwa na sekta ya usafiri na usafirishaji ambayo huunganisha watu kutoka vijijini na mijini, kanda za Kitaifa na Kimataifa” Rais Dk. Shein alisema.

Alisema kuwa, ndiyo maana Serikali yake anayoiongoza ya awamu ya saba iliivalia njuga kazi ya uimarishaji wa sekta hiyo ya ujenzi kwa kuongeza ujenzi wa barabara mpya na kuzifanyia matengenezo zile ambazo zilikuwepo.

Akielezea historia ya biashara Zanzibar, Rais Shein alisema kuwa katika kujitafutia maisha kabla ya Mapinduzi wananchi wa Zanzibar hawakuwa na fursa za kumiliki biashara kubwa kwa sababu biashara za aina hiyo zilihodhiwa na mabepari.

“Majengo kama haya ya biashara tunayakuta katika nchi za wenzetu na yameanza zamani tangu 1922 kule Marekani katika jiji la Kansas na likiitwa “Country Plaza”, alisema.

Aidha, Rais Shein alisisitiza ya kwamba kwa wale wote waliokuwa wakifanya biashara katika eneo hilo kabla ya kujengwa jengo hilo jipya la “Michenzani Mall” watapewa kipaumbe katika maombi ya kuomba kufanya biashara katika eneo hilo, kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Rais Shein pia, anatoa wito kwa vijana kuitumia fursa hiyo kwa kujipanga, kutafuta utaalamu wa kuandaa miradi yenye tija na kuitumia fursa ya uwepo wa “Mall” hiyo kwani tayari Serikali imeshawaandalia mazingira mazuri ya kuwepo kwa Mfuko wa uwezeshaji utakaowakopesha fedha ili wafanye biashara waitakayo.

Rais Shein alikumbusha usemi wake wa kuacha kufanya kazi kwa mazoea, akitaka baadhi ya vijana ambao kwao wao kazi ni za kuajiriwa serikalini tu, waachana na mawazo hayo, badala yake wajitume na serikali itaendelea kuwaunga mkono.

“Kipindi hichi cha wiki mbili zilizopita nimekuwa nikifungua miradi mikubwa mbalimbali hapa Zanzibar ambapo matukio yote hayo yana maana kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi na nchi kwa jumla ambapo pia, ni kielelezo halisi cha Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964,” alisema.

Rais Shein pia, alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutekeleza mradi unaojulikana kwa jina la “BIG-Z” (Boosting Inclusive Growth for Zanzibar-Integrated Development Project), ambao Serikali kupitia Wizara ya Fedha itashirikiana na Benki ya Dunia (WB) kuufanikisha katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Alisema kuwa, mradi huo utakuwa wa miaka 5 hadi 7 na lengo lake kuu ni kuimarisha mazingira ya maeneo hayo na kushajiisha ushirikishaji wa kijamii na kiuchumi ambapo miongoni mwa shughuli hizo ni uhuishaji wa eneo la mji wa Zanzibar (Michenzani Green Corridor).

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alipongeza Kampuni ya CRJE kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa kazi nzuri walioifanya ambayo imeonekana, pamoja na kumshukuru na kumpongeza mshauri-muelekezi wa ujenzi huo Kampuni ya “Arques Africa ya Dar es Salaam kwa kuusimamia vizuri ujenzi huo, huku akiupongeza uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na ZSSF kwa hatua hiyo nzuri ya maendeleo iliyofikiwa.

Waziri wa Fedha na Mipango Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa amesema  kuwa mradi huo ni utekelezwaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwenye ukurasa wa 203, inayoeleza hatua za kuimarisha Mfuko wa ZSSF, ili uendelee kuekeza katika miradi mbali mbali ya kiuchumi inayozalisha faida kubwa na kukuza mapato ya mfuko huo.

Anasema kuwa, kati ya miradi hiyo ni ujenzi wa “Michenzani Mall”, na  kwamba katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Shein ZSSF imewekeza miradi 12 mikubwa pamoja na miradi mengine midogo midogo ambayo yote hiyo imegharimu shilingi bilioni 140 za Kitanzania.  

Anasema ya kuwa maendeleo yote hayo yamefanywa chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Khamis Mussa, anasema kuwa, baada ya kukamilika kwa michoro mnamo Aprili 2018 ilitolewa zabuni kumtafuta mkandarasi ambapo jumla ya wazabuni 28 walijitokeza na baada ya tathmini Kampuni ya CRJE kutoka China ilishinda zabuni hiyo na kupelekea kusaini Mkataba wa ujenzi baina ya Mfuko wa ZSSF na CRJE mwezi Oktoba, 2018 kwa gharama ya shilingi bilioni 27.9.

Katibu Mkuu huyo anasema kuwa Mfuko wa ZSSF waliamua kuwa kazi ya ukodishaji wa sehemu za jengo hilo ifanywe na Kampuni yenye uzoefu hivyo ilitangaza zabuni na kufanikiwa kuipata Kampuni ya Knight Frank (T) Ltd ambayo pia ina uzoefu wa shughuli hizo kwa soko la Zanzibar.

Pamoja na kutumia Kampuni ya ukodishaji, wafanyabiashara wanaotarajia kupata nafasi katika jengo hilo ni mchanganyiko wa wafanyabiashara wakubwa na wadogo, wageni na wazawa.

Anasema wafanyabiashara wapya ambao tayari wamejitokeza kukodi sehemu katika Mall hiyo ni pamoja na Kampuni ya GSM inayoendesha maduka maarufu ya Max, Baby Zone, Shirika la Bima la Taifa (NIC), Benki ya Afrika, Horizon Pharmacy na Shamshu Phamacy, huku ZSSF ikiendelea na uchambuzi wa maombi mengine.

Anasema jengo hilo la “Michenzani Mall” limegawanyika katika maeneo makuu manne ambayo ni eneo la ghorofa ya chini ya ardhi, ghorofa ya pili, sehemu ya kati kati ya jengo, ghorofa ya tatu na sehemu mbili ya sehemu ya jengo zenye ghorofa tano kila moja.

Mfuko wa ZSSF unadhamiria pia kutekeleza nia yake ya kujenga jengo la kisasa la maegesho ya magari litakalokidhi mahitaji ya wafanyabiashara wanaokuja kuuza au kununua katika jengo hilo, ambapo jengo hilo linatarajiwa kuwa la ghorofa tatu ambazo zote zitatumika kwa ajili ya maegesho na litakuwa na uwezo wa kuchukua gari 150 kwa wakati mmoja.

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni na kustaafu. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea hakipensheni website, Simu +255 655 13 13 41, info@hakipensheni.co.tz

 

No comments :

Post a Comment