Kampuni
ya Hyatt inayomiliki Hoteli za hadhi ya Kimataifa saba Barani Afrika
kufungua Hoteli nyingine jijini Cape Town, Afrika Kusini Mwezi Desemba
mwaka huu. Hoteli hiyo mpya itakayokuwa na jumla ya vyumba 137 itakuwa
ni ya nane ambapo mbili zitakuwa nchini Afrika Kusini.
Hyatt imeingia makubaliano ya uendeshaji wa Hoteli hiyo mpya na Kampuni ya Majengo, Millat Properties ya Afrika Kusini.
Bara la Afrika hasa Kusini mwa
Jangwa la Sahara inatajwa kama moja ya maeneo ambayo yanaonyesha
matumaini ya mazingira mazuri ya kibiashara hivyo hali hiyo imeifanya
Kampuni ya Hyatt kuliweka eneo hilo kama eneo lake la kimkakati.
Pia eneo la Kusini mwa Janga la
Sahara ni kati ya maeneo yenye vivutio vingi vya Utalii na huvutia idadi
kubwa ya wageni kutoka Bara la Ulaya na Marekani kuja kutembelea
vivutio hivyo. Takwimu zinaonyesha kuwa kipindi cha janga la Corona,
idadi ya Watalii wa Kimataifa imekuwa kwa asilimia 6 Kusini mwa Janga la
Sahara kinyume na matarajio, ambapo idadi hiyo haikutarajiwa.
JIJI LA CAPE TOWN
Cape Town ambapo Hoteli hiyo ya
Hyatt itafunguliwa ndio jiji la pili linaloongoza kwa idadi kubwa ya
watu baada ya Johannesburg nchini Afrika Kusini. Vilevile, ni mji wa
kwanza ulioanzishwa katika eneo la Afrika Kusini hivyo huitwa mara
nyingi “Mji Mama” wa nchi. Kihistoria mji ulianzishwa kama kituo
cha mapumziko kwenye njia ya safari za meli kati ya Uholanzi na makoloni
yake huko Asia, hasa Indonesia ya leo.
Cape Town pia ndimo kuna jengo
la Bunge la Taifa hilo tajiri Barani Afrika. Mwaka 2014, jiji la Cape
Town lilitajwa kama sehemu bora zaidi duniani ya kutembelea na magazeti
mawili ya The New York Times na The Daily Telegraph.
Cape Town pia huvutia matukio ya
kimichezo makubwa duniani, mfano imewahi kuwa mwenyeji wa kombe la
dunia la mwaka 1995 la mchezo wa Rugby na pia Kombe la Dunia la Soka
mwaka 2010.
Pia jiji la Cape Town linasifika
kwa fukwe nzuri zenye kuvutia na upepo mwanana ambapo idadi kubwa ya
watalii hufika kuzitembelea hasa kipindi cha kiangazi.
Takwimu zinaonyesha Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Cape Town hupokea wageni milioni tano kwa mwaka,
pia husifika kwa maeneo ya kupumzika na starehe kwa watu wanaokuwa
kwenye mapumziko.
Makamu wa Rais anayehusika na Maendeleo wa Hyatt Barani Afrika na Mashariki ya Kati amesema, “Tunafuraha
kufanya kazi na Millat Properties kuileta Hyatt Cape Town, kama eneo
lenye kuvutia wasafiri wengi ni lengo letu kubwa kuwa na Hoteli ya Hyatt
Cape Town na tunaamini kuna uwezekano wa kukua zaidi nchini Afrika
Kusini. Hyatt Regency Cape Town ni mkakati wetu wa kukua kwenye soko
ambalo tunajua wageni wetu hutembelea.”
Hoteli hiyo ya Hyatt Regency
Cape Town itakuwa katika eneo maarufu la Mlima Meza (Table Mountain)
ambalo ni maarufu kwa kuvutia watalii.
Kampuni ya Millat Properties
itahusika kwenye kuitengeneza kisasa hoteli hiyo mpya kwa ndani kabla
haijafunguliwa rasmi. Pia itatumia wabunifu wa viwango vya kimataifa ili
kuifanya hoteli hiyo kuwa na muonekano mzuri wenye hadhi.
Hoteli hiyo itakuwa na jumla ya
vyumba 137, ikiwemo 15 vyenye hadhi ya rais (Presidential Suites), pia
vyumba maalumu vya kufanyia mazoezi vyenye vifaa vya kisasa na eneo kwa
ajili ya kuogelea kwa nje.
Kwa wageni ambao watafika kwa ajili ya mikutano imeandaliwa eneo lenye mita za mraba 400 mahususi kwa shughuli hizo.
Waziri wa Utalii wa Afrika
Kusini Mmamoloko Kubayi-Ngubane amesema kuwa habari ya kufunguliwa kwa
hoteli mpya ya Hyatt Afrika Kusini ni njema kwa utalii wa taifa hilo
ambalo ni miongoni mwa nchi za uchumi mkubwa zaidi barani Afrika na
kitovu cha utalii.
‘’Habari kuwa hoteli ya Hyatt
itafunguliwa ndani ya jiji la Cape Town ni njema kwa sekta ya utalii,
na ni kiashiria chema kinachoonesha kufufuka kwa sekta ya usafiri na
utalii’’, Waziri Mmamoloko amesema.
“Kama ilivyo kwa sehemu
nyingine nchini kwetu, Cape Town ni ya kipekee kweli, ikiwapatia wageni
uzoefu ambao hautasahaulika na uzuri wa asili na vivutio vya kutembelea.
Hyatt Regency Cape Town itakuwa nyongeza kamili kwa sekta ya ukarimu
katika jiji hili la kihistoria”, Mmamoloko ameongeza.
Taarifa hizi za kufunguliwa kwa
Hoteli hii Afrika Kusini zinakuja wakati tayari Hyatt ina Hoteli za
kisasa ambazo ni Hyatt Regency Johannesburg, Hyatt Regency Dar es
Salaam, The Kilimanjaro na Hyatt Regency Addis Ababa.
Nyingine mbili zinatarajiwa
kufunguliwa ndani ya miaka mitatu ijayo, ambazo ni Hyatt Regency
Nairobi, Kenya na Hyatt Regency Lagos Ikeja, Nigeria.
No comments :
Post a Comment