Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na
Viongozi Waandamizi wa Kiserikali alipofanya ziara fupi kwenye Ofisi ya
Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar
iliyopo Migombani Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi
Mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya
Zanzibar Bibi Kheriyangu Mgeni Khamis Kulia akimkaguza Balozi Seif Ali
Iddi sehemu mbali mbali za Vitengo vya Ofisi yake.
Katibu
Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif
Mohamed akifafanua jambo wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwenye jingo la Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za
Kulevya. Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwapongeza Watendaji
wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya kwa kazi
kubwa ya kudhibiti Janga la Dawa za Kulevya Nchini. Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kazi kubwa
inayoendelea kutekelezwa kwa pamoja kati ya Watendaji wa Tume ya Kitaifa
ya Kuratibu na udhibiti Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Vyombo vya
Dola imesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa wimbi la uingizwaji wa Dawa
za Kulevya Nchini.
Balozi
Seif Ali Iddi alisema hayo wakati alipofanya ziara fupi ya kuwatembelea
Watendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na udhibiti Dawa za Kulevya
waliohama kutoka Kidongo Chekundu kutokana na ufinyu wa Ofisi na hivi
karibuni kuhamia kwenye Jengo jengine liliopo Migombani Mjini Zanzibar.
Alisema
Serikali Kuu iliamua kukaza kamba katika mapambano yake dhidi ya janga
la Dawa za Kulevya ambalo ni hatari kwa Afya za Vijana wanaojihusisha na
matumizi ya Dawa hizo ambazo matokeo yake hupelekea kupunguza nguvu
kazi ya Taifa.
Balozi
Seif alieleza kwa mujibu wa Sheria Nambari 9 ya Mwaka 2009 ni kosa kwa
mmiliki, mkaazi au msimamizi wa Nyumba, jengo au mahali popote kuruhusu
kutumika katika kutayarisha Dawa za Kulevya kwa ajili ya matumizi au
kutengeneza, kuzalisha, kusambaza na kuuza.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha wazi kwamba wapo baadhi ya
Watu katika harakati zao za kimaisha wameamua kujihusisha na biashara ya
Dawa za Kulevya bila ya kujali kwamba bidhaa yao inayokwenda kwa
watumiaji wa kilevi hicho hatimae huathirika Kiafya na kushindwa
kujitegemea kimaisha.
Balozi
Seif aliwapongeza Watendaji wa Tume hiyo ya Kitaifa ya Kuratibu na
udhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar kwa kazi kubwa wanayoifanya licha ya
kuzunguukwa na mazingira magumu.
Mapema
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za
Kulevya Zanzibar Bibi Kheriyangu Mgeni Khamis alisema ipo faraja kubwa
kwa Watendaji wake kupata Ofisi nyengine kubwa itakayowapa nafasi kubwa
ya kufanya Kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Bibi
Kheriyangu alisema licha ya kuhamia kwenye jengo hilo lakini
kinachosubiriwa kwa sasa kwa jiengo hilo ni kufanyika kwa marekebisho
kwa mujibu wa maelekezo ya Wakala wa Ujenzi chini ya usimamizi wa
Wafanyakazi wahandisi Wazalendo.
Mkurugenzi
Mkuu huyo wa Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya
Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba yapo
mafanikio makubwa yaliyopatikana ya udhibiti wa uingizaji, usambazaji na
uuzaji wa Dawa za Kulevya hapa Nchini.
Bibi
Kheriyangu alisema katika kuhakikisha kwamba jukumu hilo linafikia
mafanikio ya juu tayari ipo miongozo iliyoandaliwa ya namna ya kuelekeza
taratibu za kupiga vita janga hilo thakili lililopoteza nguvu kazi ya
Taifa.
No comments :
Post a Comment