Wednesday, September 30, 2020

WIZARA YA KILIMO YASAINI MAKUBALIANO NA SHIRIKA LA BRITEN KUKUZA KILIMO BIASHARA

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya ( kulia) akibadilishana mkataba wa makubaliano ya kuendeleza sekta ya kilimo na Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika la BRITEN Bi.Josephine Kaiza leo jijini Dodoma.

 Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (kulia) akisaini mkataba wa makubaliano na shirika lisilo la kiserikali la Building Rural Incomes Through Entrepreneurship -BRITEN. Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa BRITEN Josephine Kaiza .Mkataba huo unalenga kuimarisha ujuzi wa biashara kwa wakulima wadogo-dogo ili kukifanya kuwa cha kibiashara.

Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ( wa tatu toka kulia) na watendaji wa shirika la BRITEN mara baada ya kusaini mkataba wa makubaliano leo jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya ( wa pili toka kulia) akiongoza kikao cha maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani ambayo kitaifa yatafanyika tarehe 10 Octoba mkoani Njombe.Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Prof.Siza Tumbo na toka kushoto wa pili ni Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Katalina Revocati.

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya (katikati) akiongoza kikao cha kamati ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yatakayofanyika kitaifa mkoani Njombe kuanzia 10-16 Octoba mwaka huu.Kushoto ni Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Katalina Revocati na kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Prof.Siza Tumbo.
( Habari na Picha- Wizara ya Kilimo)

…………………………………………………………………………………

Wizara ya Kilimo imesaini mkataba wa makubaliano na taasisi ya BRITEN kuhusu  kuendeleza sekta ya kilimo kwa kufanya kilimo biashara na kuongeza upatikanaji wa pembejeo na masoko kwa wakulima.

Makubaliano hayo yanahusisha kuimarisha ujuzi wa biashara kwa wakulima wadogo ili kufanya

kilimo biashara na kuimarisha uwezo wa kutunza mazao kabla na baada ya mavuno ili kupunguza upotevu.

Mkataba huo wa makubaliano umesainiwa leo (30.09.2020) baina ya Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya na Afisa Mtendaji Mkuu wa Building Rural Incomes Through Entrepreneurship (BRITEN) Josephine Kaiza jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa utiaji saini Kusaya alisema mkataba huo utasaidia wizara kutumia fursa ya kuongeza ujuzi wa wakulima kufanya kilimo biashara, matumizi ya teknolojia na kuwapatia  mbinu bora za kuongeza kipato.

“Tunataka kupitia ushirikiano huu na BRITEN tuwasaidie wakulima hususan wadogo kuongeza kipato , usalama wa chakula ili sekta ikue zaidi na kuongeza tija na pato la taifa” alisisitiza Kusaya

Eneo jingine la ushirikiano ni kutoa huduma za upatikanaji habari,pembejeo na kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa wakulima wadogo wadogo kutumia tafiti na uvumbuzi wa teknolojia mpya za kilimo.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Kusaya alieleza mkakati wa wizara kuhakikisha inapima sampuli za udongo katika wilaya zote nchini ili kuwasaidia wakulima na wawekezaji kujua virutubishi gani na aina ipi ya mbolea au zao la kupanda.

Alisema tayari kituo cha utafiti wa kilimo (TARI) Selian cha Arusha kimekusanya sampuli za udongo toka kata zote 3,956 za Tanzania bara ili kujua aina  gani ya zao inastahili wapi na mbolea gani ya kutumia ili kuwa na uhakika na kilimo.

“ Tunahitaji tabia za udongo ziwe wazi na kuwezesha wakulima na  wawekezaji kujua eneo la kwenda kulima na aina gani ya zao na pembejeo za kutumia’ alisema Katibu Mkuu huyo.

Ili kutekeleza mkataba huo wa makubaliano ,Katibu Mkuu Kusaya ameelekeza iundwe kamati ndogo ya watalaam wa wizara itakayofanya kazi ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mkataba uliosainiwa na mingine ya aina hiyo.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa BRITEN Josephine Kaiza alisema shirika lao limebobea katika kutekeleza miradi ya kilimo kibiashara na kutengeneza ushindani wa kibiashara kwa kuwafundisha wakulima mbinu za uzalishaji bora wa mazao.

Josephine alitaja mafanikio ya taasisi hiyo kuwa imewafanikiwa kuongeza muunganiko wa wadau wa sekta ya kilimo kufanya kazi kwa pamoja na kugusa maisha ya wakulima 165,000 mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

“ Tunaamini kupitia makubaliano haya tutaweza kuchangia maendeleo ya kilimo kwa ufanisi zaidi na kufikia wakulima wengi zaidi “ alisema Josephine

Taasisi ya BRITEN imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kilimo kwa takribani miaka 10 na kupitia makubaliano na wizara ya kilimo wataendelea kutekeleza mpango mkakati wa pili wa ukuzaji sekta ya kilimo nchini (ASDP II).

 

No comments :

Post a Comment