………………………………..
Serikali za Tanzania na Ufaransa
zimeingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya mbinu za kufundishia lugha ya
Kifaransa kwa walimu 100 nchini ambao watakuwa na uwezo wa
kufundisha
wanafunzi 5,000 wa Kitanzania katika ngazi ya sekondari.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika
kikao kati ya Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia, Dkt. Leonard
Akwilapo kilichofanyika Jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya Dola za
Kimarekani 250,000 zitatumika ili kufanikisha mpango huo.
Katika kikao hicho wamekubaliana
kufanyika kwa vikao vya kitaalamu kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia na Kituo cha Ubalozi wa Ufaransa (Alliance Francais) ili
kupanga utekelezaji wa mafunzo hayo ya walimu.
Aidha, Balozi Clavier ameonesha
kuwepo kwa fursa za Watanzania kusoma programu zisizopungua 2,000 za
Kiingereza nchini Ufaransa. Ameeleza kuwa Ufaransa inaandaa Maonesho ya
Elimu ya Juu (Higher Education Fair) yatakayofanyika nchini Mei 2021
ambapo vyuo 20 vya Ufaransa vitashiriki kutafuta ushirikiano na Vyuo
Vikuu vya Tanzania na Sekta binafsi.
Akizungumza katika kikao hicho,
Katibu Mkuu Akwilapo ameushukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa kuendeleza
ushirikiano katika kukuza na kuimarisha elimu ya Juu nchini kupitia
ufadhili wa mafunzo hayo na kuagiza wahusika katika Wizara anayoisimamia
kuhakikisha vikao vya kitaaluma vinafanyika ili mafunzo hayo yaweze
kuanza kwa wakati uliopangwa.
Katibu Mkuu Akwilapo pia ameahidi
kuweka wazi kwa Watanzania kuhusu kuwepo kwa fursa hiyo ya kusoma
programu za Kiingereza nchini Ufaransa ili Watanzania waweze
kuchangamkia fursa hiyo.
No comments :
Post a Comment