Monday, September 21, 2020

SERIKALI YAKARIBISHA WAWEKEZAJI MAZINGIRA NI SALAMA


………………………………………………………………………………..

Na Mwandishi wetu

SERIKALI ya Tanzania imewakaribisha wawekezaji katika kuongeza thamani ya mnyororo wa

bidhaa za kilimo, ufugaji na uvuvi na kusema mazingira ya uwekezaji ni rafiki.

Akizungumza katika kuitangaza Tanzania na vivutio vyake katika Jukwaa la kilimo biashara lililoandaliwa na taasisi ya Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRF), na kufanyika Kigali Rwanda kwa njia ya video, Naibu Waziri  wa Kilimo, Omar Mgumba alisema  Tanzania ipo tayari kwa uwekezaji.

Alisema pamoja na kuwezesha mazingira rafiki, kuwa kisiwa cha amani,Serikali ya Tanzania imetengeneza miundombinu ambayo inawezesha  wawekezaji kufikia soko la ndani na nje.

Alisema pamoja na kuwa na uhakika wa umeme mpaka vijijini, serikali pia imeboresha miundombinu ya barabara kiasi cha  mwekezaji kufika kokote anakotaka.

Alisema katika mkutano huo wa kutambulisha Tanzania katika uchumi wa Kilimo biashara, Naibu Waziri Omar Mgumba alisema kwamba  pamoja na kuita wawekezaji katika mashamba makubwa ya miwa kwa ajili ya sukari, pamba kwa ajili ya kusokota nyuzi na kuuza mavazi, uvuvi wa kina kikuu,fursa zilizopo nchini katika Kilimo, ufugaji na uvuvi; zinaambatana na uwapo wa soko la ndani lenye wananchi takribani milioni 60, soko la Afrika Mashariki na soko la Kusini .

Alisema wawekezaji hawatajutia uamuzi wao wa kuwekeza nchini kwa kuwa Tanzania tangu Uhuru  ni nchi yenye  amani na imethibitishwa na  Global Peace Index kuwa Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika ndio yenye amani; uchumi wake unakua na ina raslimali tosha za asili kwa ajili ya kutumika kama malighafi.

“Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 7 za ardhi zinazofaa kulimwa zikiwa na uwezo wa kulima kwa umwagiliaji kutokana na kuzungukwa na mito na maziwa” alisema Mgumba.

Alisema ni lengo la serikali kuwa ifikapo mwaka 2025 taifa hili linakuwa na uchumi wa kati unawezesha kuwapo kwa mnyororo wa thamani kwa bidhaa za viwandani na hivyo kuinua ajira uya wakulima ambayo ni asilimia 66 ya ajira nchini.

Aidha kilimo ndicho kinachoingiza asilimia 28 ya pato la taifa.

 Waziri Mgumba pia alizungumzia  fursa katika ufugaji na katika uvuvi wa samaki.

Alisema serikali imefanya mabadiliko mengi katika sera,sheria na tozo ili kuwezesha uwekezaji kuwa rafiki zaidi na hasa uwekezaji wa uvuvi  kina kikuu.

Naibu waziri huyo alisema kuna mambo mengi ambayo yanatoa fursa ya uwekezaji  na yametanabaishwa katika ASDP 11 sehemu  ya tatu.

Katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa  Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) Dk Maduhu Kazi alisema kwamba Tanzania inawakaribisha wawekezaji na kwamba wapo tayari kuwahudumia.

Alisema taifa ni salama lenye amani likifuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na kwamba uchumi wetu unakua na  uko salama kutokana na  kuwa na utulivu muda wote hata wakati na baada ya uchaguzi.

 Pia Tanzania ipo kimkakati ikiwa inazungukwa na mataifa manane na bandari kuu tatu zinazohudumia nchi 6, viwanja vya ndege vya kimataifa vitatu na soko la watu milioni 177 kwa Afrika mashariki, SADC watu milioni 342, ikiwa na watu milioni 650 soko la TFTA na soko la AGOA lenye bidhaa 6,000. Pia lipo soko la EBA (Ulaya).

Aidha alisema kuna fursa nyingi nchini za uwekezaji kama katika viwanda vya kemikali  kwa ajili ya mbolea na dawa za mashambani; viwanda vya kusindika bidhaa mbalimbali za kilimo na pia viwanda vya kutengenezea zana za Kilimo, uvuvi na ufugaji.

 Naye Dk Andrew Komba alisema  kwamba  mazingira ya Tanzania kwa sasa yapo tayari kupokea wawekezaji baada ya marekebisho ya sheria sera kuhusu masuala ya uwekezaji.

Jukwaa la  AGRF  ndio  jukwaa kubwa la kilimo barani Afrika likiwakusanya wadau mbalimbali ili kuchukua hatua za kiutendaji zitakazoweza kusukuma mbele kilimo barani Afrika na kuwa cha biashara chenye tija kwa wakulima.

 Watu zaidi ya 4000 walishiriki katika jukwaa hilo wakiwemo viongozi wa kitaifa, mawaziri, wadau mbalimbali wa kilimo na watu binafsi kwa kutumia njia ya mtandao.

 

No comments :

Post a Comment