Wednesday, September 30, 2020

SERIKALI KUSIMAMISHA MISHAHARA YA MAAFISA UTUMISHI WATAKAOSABABISHA WATUMISHI KUTOLIPWA MISHAHARA


Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael akizungumza na washiriki wa mafunzo ya wiki mbili ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 140 yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.

Baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya wiki mbili ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 140 wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua mafunzo hayo yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.

Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi akitoa ufafanuzi wa utekelezaji wa maelekezo ya Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael aliyoyatoa wakati akifungua mafunzo ya kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Utawala 140 yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.

Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Bw. Boniface B. Chatila akiahidi kutekeleza maelekezo ya Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa niaba ya kundi la pili la  washiriki 140 wa mafunzo ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.

***************************************

Na. James Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 30 Septemba, 2020.

Maafisa Utumishi watakaozembea na kusababisha Watumishi wa Umma nchini kutolipwa

mishahara yao kwa wakati, watasimamishiwa mishahara na Serikali mpaka watakapohakikisha watumishi hao wamelipwa mishahara yao.

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Francis Michael wakati akifungua mafunzo ya wiki mbili ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara kwa kundi la pili la Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala 140 kutoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Kigoma na Tabora yanayofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa VETA.

DKt. Michael amesema, kuna tatizo katika baadhi ya Taasisi za Umma kwani wapo Maafisa Utumishi wanajifanya miungu watu wakati wajibu wao ni kumtengenezea mazingira mazuri ya kikazi mtumishi ili ajisikie yuko sehemu salama na aweze kutekeleza ipasavyo jukumu la kuwahudumia wananchi.

“Msiwafanye watumishi mnaowasimamia kuona sehemu ya kazi kama jehanamu, hivyo mbadilike kwani Serikali haitomvumilia yeyote atakaye kinzana na azma yake ya kuboresha huduma kwa wananchi”, Dkt. Michael alisisitiza.
Ameongeza kuwa, ni lazima Maafisa Utumishi wabadilike kwa kuwajengea mazingira Watumishi wa Umma kuipenda Serikali yao kwasababu inawajali na kuthamini mchango wao katika maendeleo ya taifa.

Dkt. Michael amefafanua kuwa, Serikali inamhakikishia mtumishi usalama wa ajira yake tofauti na sekta binafsi, hivyo hakuna Afisa Utumishi atakayevumiliwa pindi akisababisha Serikali kulaumiwa na Watumishi wa Umma au Wananchi.

Naye, Mkuu wa Idara ya Utawala na Utumishi, Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Bw. Boniface B. Chatila kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, ameahidi kuwa, wakirejea katika maeneo yao ya kazi watahakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuondoa kero ya Watumishi wa Umma kufuata huduma Ofisi ya Rais Utumishi Dodoma, huduma ambazo wanastahili kupewa katika maeneo yao ya kazi.

Aidha, Bw. Chatila amemhakikishia Dkt. Michael kuwa, ujuzi watakaoupata kupitia mafunzo ya Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara watautumia ipasavyo kuongeza ufanisi kiutendaji ili kuboresha utoaji huduma kwa umma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, ACP Ibrahim Mahumi amesema, suala la mtumishi kukosa mshahara hivi sasa linachukuliwa kama ni kosa kubwa hivyo Afisa Utumishi atakayebainika atasimamishiwa mshahara ikiwa ni hatua ya awali na atachukuliwa hatua za kinidhamu ikizingatiwa kuwa, mfumo mpya utaonesha uzembe wa afisa huyo.

Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara utaanza kutumika rasmi Mwezi Novemba, 2020 mara baada ya kukamilika kwa mafunzo ya makundi yote ya Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala ambao ndio wenye jukumu la kuutumia mfumo huo kiutendaji.

 

No comments :

Post a Comment