Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma
Serikali
kupitia Wizara ya Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa
kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wanaochangia sekta ya afya kupitia
Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund imeridhia kuweka saini Hati
ya Shilingi Bilioni 125.69 kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya katika
ngazi ya msingi nchini
Akiongea
wakati wa kuidhinisha makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Prof. Mabula Mchembe amesema kuwa lengo kuu la Mfuko huo tangu
kuanzishwa kwake mwaka 1999 ni Kuimarisha huduma za afya katika ngazi ya
msingi (halmashauri) zote nchini.
Amesema
katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/21 Wadau nane (8)
watachangia jumla ya USD 53.84 sawa na Shilingi bilioni 125.69 kwa
kipaumbele cha kuimarisha huduma za afya katika vituo vya afya kwenye
halmashauri zote 184 nchini.
“Shilingi
bilioni 105.32 zitatumika kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za
afya katika vituo vya afya vipatavyo 5,533 kwenye halmashauri zote 184
nchini ikiwa ni pamoja na ununuzi wa dawa, vifaa na vifaa tiba,
uendeshaji wa vituo, ukarabati mdogo na huduma za chanjo na vikoba.
“Fedha hizo zitapelekwa moja kwa moja vituoni kwa utaratibu wa ‘Direct
Health Facility financing” Alisema Prof.. Mchembe.
Aidha,
Prof Mchembe alisema Shilingi bilioni 4.29 zitatumika kwa ajili ya
kuziwezesha Timu za Afya za Mikoa 26 kufanya ufuatiliaji na usimamizi
shirikishi katika halmashauri zote nchini na Shilingi bilioni 2.09
zitawezesha Ofisi ya Rais– TAMISEMI kusimamia na kutoa msaada wa
kitalaam katika halmashauri na mikoa yote nchini.
Aliongeza
kuwa Shilingi bilioni 5.13 zitawezesha Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutekeleza masuala ya sera, mikakati na
miongozo kwa ajili ya kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa kiwango
na ubora stahiki na Shilingi bilioni 8.86 zitakuwa kwa ajili ya
kutekeleza maeneo mengine ya kipaumbele katika sekta.
“Vipaumbele
tulivyoidhinisha na kamati ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalam 620
wa dawa za usingizi; kununua machine za kisasa za kutolea dawa za
usingizi katika vituo vya afya ngazi ya halmashauri na kufanya ukarabati
mkubwa katika vyuo vinne (4) vya kutolea mafunzo ya watalaam wa afya”.
Prof.
Mchembe alitaja maeneo mengine ya kipaumbele yaliyoidhinishwa na Kamati
Kuu ya Mfuko huo kuwa ni kuhuisha Mkataba wa Makubaliano (MOU) baina ya
pande zote mbili kwa kipindi cha 2021 – 2026, kununua mashine za
kutolea dawa za usingizi katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja
na kuvijengea uwezo vituo vya afya katika kusimamia na kutumia fedha kwa
kuzingatia miongozo na taratibu mbalimbali.
Maazimio
ya uwekaji saini Hati hiyo yamefanyika kwenye ofisi ya Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyoko mji wa Serikali
Mtumba ambapo ulihudhuriwa na watalaam kutoka Wizara ya Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Fedha na
Mipango, OR – TAMISEMI, Bohari ya Dawa na Wadau wa Maendeleo
wanaochangia Mfuko huo kutoka Canada, Denmark, KOICA, Ireland,
Switzerland UNICEF, UNFPA na Benki ya Dunia. walioshiriki kwa njia ya
‘video conference’.
No comments :
Post a Comment