Dkt.Shein
ameyasema hayo leo Septemba 28, 2020 katika ufunguzi wa jengo jipya la
abiria na eneo la maegesho ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Abeid Amani Karume (Terminal III), lililopo Kiembesamaki Unguja.
Viongozi
kadhaa walihudhuria akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi
Seif Ali Idd, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye pia ni
Mgombea wa Urais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi na viongozi wengine
na wananchi.
Katika maelezo yake, Rais Dkt.Shein amesema kuwa na
kiwanja cha ndege kikubwa na cha kisasa ni kivutio kizuri kwa wageni
wanaokuja hapa nchini kwa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Ameeleza
kuwa, katika sekta ya usafiri wa anga nchini, Zanzibar imepiga hatua
kubwa kwa kuendeleza ubora wa miundombinu yake kama ambavyo inaonekana
katika uwanja huo wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ambao kwa
sasa una vituo (Terminals) vitatu.
Rais Dkt.Shein ameongeza kuwa,
viwanja vya ndege ni injini za maendeleo ya kiuchumi duniani, kwa
sababu ni vichocheo vya kukuza na kuimarisha utalii pamoja na uhusiano
wa kibiashara kitaifa na kimataifa.
Amesema kuwa, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba kwa kutilia maanani umuhimu huo wa
viwanja vya ndege katika maendeleo ya nchi imefanya jitihada mbalimbali
za kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini.
Aidha, Rais Dkt.Shein alieleza kuwa kufunguliwa kwa jengo hilo jipya la uwanja wa ndege huo ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020 ibara ya 94 kifungu (a) ambapo Serikali ya Mpinduzi ya Awamu ya Saba iliagizwa kutekeleza ujenzi huo.
Rais Dkt Shein alisema kuwa, ujenzi wa jengo hilo ulianza mwezi Februari 2011, lakini licha ya changamoto mbali mbali za hapa na pale zilizojitokeza katika hatua za ujenzi wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imefarijika kwa kuzitatua changamoto hizo na kufikia mafanikio hayo ya kulizindua jengo hilo.
Pamoja na hayo, Rais Dkt.Shein alisema kuwa, badala ya ile gharama ya Dola za Kimarekani 70.4 milioni kwa mkataba wa mwanzo, mradi huo mpaka kukamilika kwake umegharimu dola za Kimarekani 128.75 milioni.
Ameongeza kuwa, Serikali ililazimika kuongeza mambo kadhaa ya marekebisho katika jengo pamoja na sehemu ya nje ya jengo hilo ili kuupa hadhi ya juu uwanja huo na uweze kuhudumia ndege za aina zote.
Amesema kuwa, kutokana na haja hiyo Serikali ilibidi kusaini mikataba miwili ya nyongeza na kampuni ya BCEG wa kwanza ukiwa na fedha za nyongeza zenye thamani ya Dola za Kimarekani 11,828,674.71 na wa pili wenye thamani ya Dola za Kimarekani 46,518,414.8.
Amesema kuwa, fedha hizo za nyongeza jumla ya Dola za Kimarekani milioni 58.35 zinalipwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia bajeti yake ya ndani kwa ajili ya uendelezaji wa mradi huo na hadi sasa Serikali hiyo inaendelea vizuri katika malipo hayo.
Ameongeza kuwa, hivi sasa uwanja huo wa ndege una uwezo wa kupokea ndege kubwa tatu aina ya “CODE E” kwa wakati mmoja ambapo pia, huduma zote ambazo zinastahiki kuwepo katika kiwanja cha ndege cha kimataifa cha kisasa tayari yapo.
Rais Dkt.Shein ametumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya Ujenzi ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG) ya Jamhuri ya Watu wa China kwa moyo wao wa kindugu waliouonesha kwa kukubaliana na Serikali kuendelea na ujenzi huo na kwa kukubali kusaini na Serikali mikataba hiyo ya nyongeza.
Ameupongeza uongozi wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji, Wakandarasi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wale waliotoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Wizara ya Fedha, Kilimo, Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Kampuni ya Coastal Dredging inayomilikiwa na S.S. Bakhresa Group Companies na Meneja wa Mradi huo Mhandisi Yassir DeCosta. Pia, aliipongeza Kampuni ya ADPI ya Ufaransa ambayo ndiyo Mshauri Mwelekezi katika ujenzi huo
Aidha, alieleza kuwa jengo hilo lenye viwango vya kisasa lina mifumo mbalimbali ya teknolojia inayokwenda na wakati ikiwemo mifumo ya kupokelea mizigo, mifumo ya kubaini ishara ya kuzuka kwa moto ambayo imejengewa ndani ya kituo hicho ambapo pia, ndege yoyote inaweza kutua na kupata huduma bila ya usumbufu pamoja na kuwepo kwa maduka yasiyotoza ushuru (duty free shops).
Sambamba na hayo, Rais Dkt.Shein alisema kuwa, jengo hilo litasaidia sana kuongeza abiria na mizigo kwa sababu lina uwezo wa kuchukua abiria milioni 1.6 kwa mwaka ambalo litapunguza msongamano wa abiria katika kituo cha pili cha uwanja huo.
Rais Dkt.Shein amewashauri viongozi na watendaji wa kiwanja hicho kufahamu kwamba mwelekeo wa Serikali wa baadae uwe ni kuzikaribisha zaidi ndege kubwa ambazo zitakuwa zinachukua abiria wengi na kuingiza mapato.
Ametoa wito kwa wananchi hasa wale walio kwenye utumishi wa umma wanapopata nafasi ya kutembelea nchi za wenzao wajifunze yale mazuri ya manufaa ambayo wao bado hawajawanayo ili waje kuyaanzisha hapa nchini kwa kuongeza ubora kama alivyofanya Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Marehemu Mzee Abeid Karume.
Amewasisitiza watendaji kuwa wazalendo, wawajibikaji, kutumia ujuzi na wenye bidii katika kazi zao za kuendesha uwanja huo huku akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya wajibu wake katika jitihada za kwuapatia maendeleo wananchi wa Zanzibar hivyo kuna haja ya kuzienzi na kuzithamini jitihada hizo.
“Ninaamini kwamba kiwanja chetu cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume na kile cha Pemba vitaweza kufikia ubora kama ule wa “Heathrow” kilichopo London Uingereza, au Changi kiliopo Singapore na vinginevyo ambavyo vinatajwa kuwa viwanja bora na vyenye shughuli nyingi duniani,"amesema.
Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dkt.Sira Ubwa Mamboya amesema kuwa, kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo kutaimarisha dira mpya kwa wananchi kwa kupata ajira sambamba na kuongezeka kwa pato la Taifa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa amesema jengo hilo la aina yake litaongeza mapato kutokana na kuongezeka kwa wageni wanaoingia na kutoka nchini, sambamba na kuondoa manung’uniko kutoka kwa wageni juu ya ufinyu wa nafasi uliokuwa ukiukabili uwanja huo.
Amesema, kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo kutaimarisha soko la utalii na hivyo kuwa sababu ya masoko mapya ya utalii kuongezeka kutokana na kuwepo kwa huduma hiyo muhimu.
Aidha, amesema Wizara ya Fedha na Mipango itaendelea na jukumu la kutafuta fedha ili kutekeleza miradi mbalimbali inayobuniwa, akibainisha umakini wa wizara hiyo na kutolea mfano wa juhudi zilizofanyika ili kupata dola milioni 58.3 ikiwa ni ongezeko la gharama za ujenzi wa jengo hilo.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafiri Mustafa Aboud Jumbe Mwinyi alitoa historia ya usafiri wa ndege hapa Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964.
Katibu Mkuu huyo pia, alieleza kuwa jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.6 kwa mwaka ambalo litamudu ongezeko la wageni hasa watalii ambao wamekadiriwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 kufikia 850,000 kwa mwaka kutoka idadi ya mwaka uliopita mnamo Disemba 2019 walikuwa 538,000.
Alieleza kuwa, wizara yake hivi sasa inaendelea na ukamilishaji wa mambo madogomadogo yaliobakia ikiwa ni pamoja na kuunganisha mifumo ya uendeshaji wa viwanja, ujenzi wa uzio wa kulihifadhi eneo hilo, uunganishaji wa njia ya kutoka eneo hio hadi njia kuu pamoja na kufanywa ukaguzi wa pamoja baina ya ICAO, IATA na Kampuni za ndege zitakazotumia jengo hilo ili kujiridhisha na kuanza kulitumia rasmi.
Aidha, alieleza namna ujenzi huo ulivyoonza ambapo saini ilitiwa mnamo mwaka 2010 huku Seriikali ikigundua mapugufu kadhaa mnamo mwaka 2012 ambapo hatua mbalimbali baada ya hapo zilichukuliwa.
Kwa malelezo ya Katibu Mkuu huyo jengo hilo lina ukubwa wa mita za mraba 25000,lina milango minne (gates) ambazo kwa kitaalamu inaitwa Mikonga mikubwa na midogo ya kupitia abiria wanaoondoka au kuwasili ambacho pia kina barabara ya kurukia ndege yenye ukubwa wa mita za mraba 36,000.
Pia, kuna kumbi za abiria wa ngazi mbalimbali na kuna eneo la maegesho ya gari lenye ukubwa wa mita za mraba 8,818 ambalo lina uwezo wa kuegesha magari 214 kwa wakati mmoja.
Naye Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar, Xie Xiaowu ametoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Shein kwa kukamilisha mradi huo na kuahidi kuwa Jamhuri ya Watu wa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Sherehe hizo za ufunguzi wa jengo jipya la abiria na eneo la maegesho ya ndege katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume (Terminal III), zilipambwa na ngoma pamoja na nyimbo mbalimbali za wasanii wakiongozwa na msanii maarufu wa bongo flava kutoka Dar es Salaam, Aslay Isihaka Nassor maarufu Aslay.
No comments :
Post a Comment