Mratibu
wa Kitaifa wa Zao la Korosho kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI
Naliendele Mtwara, Dkt.Geradina Mzena (kulia), akiwaelekeza Afisa Kilimo
na Mratibu wa Zao la Korosho Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,
Isabella Chilumba (kushoto) na Afisa Kilimo wa Wilaya ya Gairo, Eunice
Kyungai jinsi ugonjwa wa Ubwiriunga unavyoathiri zao la korosho. Mafunzo
hayo kwa vitendo yalifanyika jana kwenye shamba la korosho la Shule ya
Msingi Mnjilili wilayani Gairo, Morogoro.
Mtafiti Mwandamizi na
Mdhibiti wa Visumbufu vya Wadudu na Magonjwa kwenye zao la korosho,
kutoka Tari- Naliendele Mtwara, Dkt.Wilson Nene, akiwaeleza Maafisa
Ugani na Wakulima namna ya kudhibiti magonjwa mbalimbali ya zao hilo.
Mtafiti kutoka Tari-
Naliendele Programu ya Zao la Korosho, Kasiga Ngiha, akitoa mafunzo ya
jinsi ya kuandaa shamba, kulipima na upandaji wa zao la korosho kwa
Maafisa Ugani na Wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Maafisa Ugani na Wakulima wakijifunza kwa vitendo namna ya upimaji wa shamba la korosho kabla ya kupanda.
Afisa Kilimo kutoka Kata ya
Madege Wilaya ya Gairo, Fideli Ntumo (Aliye chuchumaa akipima shamba kwa
kamba katika mafunzo hayo ya vitendo.
Mkulima Julius Senyagwa
kutoka Kijiji cha Majawanga wilayani Kilosa, akijifunza namna ya kuweka
‘mambo’ wakati wa mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho.
Afisa Kilimo kutoka Wilaya
ya Gairo, Mary Gasper (kulia) na wenzake, akijifunza namna ya kuweka
‘mambo’ wakati wa mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho.
Kushoto ni Afisa Kilimo, Lucy Mushi na Jacquline Roland.
Afisa Kilimo kutoka Wilaya
ya Gairo, Laya Abbas, akijifunza namna ya kuweka mambo wakati wa
mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho.
Mtafiti
Mwandamizi na Mdhibiti wa visumbufu vya wadudu na magonjwa kwenye zao
la korosho, kutoka Tari- Naliendele Dkt.Wilson Nene, akiwaonesha kwa
vitendo Maafisa Ugani na Wakulima namna ya kudhibiti magonjwa mbalimbali
ya zao hilo.
Afisa
Kilimo kutoka Wilaya ya Gairo, Nasibu Said, akishiriki mafunzo kwa
vitendo kwa kuchimba mashimo kabla ya kupanda miche bora ya mikorosho
katika shamba hilo lililopo shule ya Msingi Mnjilili, Gairo.
Mkulima
Elizabeth Senyagwa kutoka Gairo, akishiriki mafunzo kwa vitendo kwa
kuchimba mashimo katika shamba hilo la mfano la korosho la Shule ya
Msingi Mnjilili.
Mtafiti
kutoka Tari- Naliendele Programu ya Zao la Korosho, Kasiga Ngiha,
akitoa mafunzo ya jinsi ya kupanda mche wa korosho kwa Maafisa Ugani na
Wakulima.
Mtafiti wa Kilimo kutoka
Tari Naliendele, Selemani Libaburu, akitoa mafunzo ya jinsi ya
kuchanganya viuatilifu na maji kwa Maafisa Ugani na Wakulima kabla ya
kupulizia kwenye mikorosho.
Mtafiti wa Kilimo kutoka Tari Naliendele, Selemani Libaburu, akionesha namna ya kupulizia viuatilifu kwenye mikorosho.
Afisa Kilimo kutoka Kata ya
Magubike wilayani Kilosa, Iston Kutita, akijifunza kwa vitendo namna ya
kupulizia viuatilifu mikorosho.
Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Morogoro.
WAKULIMA wa zao la korosho mkoani hapa wameahidi kufanya
mageuzi makubwa ya kilimo cha zao hilo baada ya kuhamasika na programu
maalumu ya mafunzo ya nadharia na vitendo inayoendelea kutolewa na
Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi yake ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI)
Taasisi hiyo kupitia kituo chake cha Naliendele kwa sasa
kinaendesha mafunzo ya kilimo bora cha zao la korosho kwa wakulima na
maafisa ugani wa Halmashauri zilizo kwenye mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda
ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini lengo likiwa kuongeza tija
na kuinua kiwango cha uzalishaji wa zao hilo.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti wakati wa mafunzo
hayo eneo la Shule ya Msingi Mnjilili, Mji Mdogo wa Gairo mkoani hapa
wadau hao walisema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka.
“Mafunzo haya yamenisaidia na kunipa mwanga wa namna ya
kuboresha shamba langu la ekari mbili, kwa sasa nina matumaini makubwa
ya kulima kitaalam zao hili.” alisema mkulima wa korosho kutoka Dumila,
Samwel Dede.
Mkulima mwingine Elizabeth Senyangwa kutoka Gairo alisema
kabla ya kupata mafunzo hayo miongoni mwetu tulikuwa kwenye mtazamo wa
kustawisha zao hilo kimazoea. Lakini kwa sasa nimejifunza mengi hasa
kwenye eneo la udhibiti wa wadudu na magonjwa na namna bora ya kuandaa
shamba langu.
Naye Afisa Ugani Elina Dastan kutoka Kilosa anaeleza kuwa
anaona fahari kwa Taifa la Tanzania kupitia watafiti wake kuzidi kubuni
teknolojia mpya kwa ustawi wa sekta ya kilimo nchini.
“Ugunduzi wa teknolojia za aina zote hizi za mbegu bora za
korosho kutoka Tari ni fursa kubwa kwa wakulima na watanzania kwa
ujumla.” alisema Dastan.
Aidha, kutokana na hamasa iliyotawala wakati mafunzo
yakiendelea, wadau hao wa zao la korosho walitaka kufahamu kwa kina ni
aina ipi ya mbegu za korosho ambazo ni bora zaidi na zinazaa kwa wingi
kama mkulima atahitaji kupata mavuno zaidi?.
Lingine lililojitokeza kwenye majadiliano ni je mbegu za
zao hilo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo zinachukua muda gani hadi
kuanza kuvunwa korosho yake sanjari na umakini wa palizi yake?
Na washiriki wa mafunzo hayo walitaka kufahamishwa endapo wanataka mbegu za Tari kwa haraka watazipataje na kwa utaratibu gani?.
Na zaidi wakionesha mwamko mkubwa walitaka kujua uhakika wa
mwenendo wa soko kwa sasa…huku wale wengine waliopatiwa mbegu na
Serikali huko nyuma wakitaka kuhakikishiwa ubora na uhalali wa mbegu
hizo.
Akijibu maswali hayo Mratibu wa zao hilo kitaifa, Dkt
Geradina Mzena alisema mbegu zote zilizogunduliwa na kufanyiwa utafiti
na Serikali kupitia taasisi hiyo zina ubora na zinafaa kwa matumizi ya
mkulima katika kupata tija inayostahili.
Huku Mtafiti kutoka Kituo cha Tari Naliendele Mtwara,
Kasiga Ngiha akibainisha kuwa mbegu za korosho zinazozalishwa na kituo
hicho huchukua kati ya miaka miwili mpaka mitatu kabla ya kukomaa na
korosho yake kuanza kuvunwa.
Ngiha alisema mkulima anapaswa kuzingatia kanuni bora za
kilimo cha zao hilo ili kuleta tija na ustawi, na anapofikia wakati wa
kupalilia hupaswa kuwa makini kwa kuhakikisha jembe analotumia lisizame
zaidi ya sentimeta 20 kinyume chake anaweza kujikuta akikata mizizi ya
mkorosho inayoota kwa kwenda chini na ile inayotambaa.
Akifafanua utaratibu wa kupata mbegu hizo hususan kwa
wakulima wa mkoa wa Morogoro, Dkt Mzena alisema mkulima yeyote
anayehitaji mbegu hizo awasiliane na Bwana Shamba aliye karibu naye, na
yeye atawasiliana na Tari Naliendele ili kupatiwa huduma hiyo.
Aidha kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro wanaweza kutumia kituo
cha mauzo ya mbegu cha Tari kilichopo Bagamoyo maarufu ‘Cash
Development Centre (CDC)’
Akifafanua kuhusu uhakika wa soko la korosho Mzena
aliwahakikishia wakulima kuwa zao hilo kwa miaka yote limeendelea kuwa
ni ‘dhahabu ya kijani’ na soko lake halijawahi kuyumba.
Alisema zao hilo linauzwa kwa mfumo kamili unaosimamiwa
hatua kwa hatua yaani mfumo wa stakabadhi ghalani sambamba na mkulima wa
zao hilo kuendelea kuwa na fursa lukuki za kukopesheka kupitia taasisi
za fedha.
Na kuhusu hoja iliyoibuliwa juu ya zile mbegu zilizotolewa
na Serikali huko nyuma kipitia mabwana shamba alisema mbegu hizo zipo
salama na zinafaa kwa matumizi.
Kwa upande wake Afisa Kilimo na Mratibu wa Zao la Korosho
mkoani hapa Isabella Chilumba alisema azma ya mkoa huo ni kuzalisha tani
500 za korosho ifikapo 2023, huku msimu ujao 2020/21 wakitarajia
kuzalisha tani 300 ya zao hilo.
Hata hivyo Chilumba alibainisha hatua kwa hatua maendeleo
kadhaa ya ongezeko la uzalishaji wa zao la korosho kwa misimu 3
iliyopita, ambapo mwaka 2017/18 mkoa ulipata tani 63, na 2018/19 ulipata
tani 155, mwaka 2019/20 kiwango hicho kiliongezeka na kufikia tani
181.5, huku shabaha ya taifa ni kufikia tani milioni 1 ifikapo 2023.
“Naamini kwa mafunzo haya yanayotolewa na taasisi ya
utafiti wa kilimo, pamoja na stratejia zingine tulizonazo kama mkoa
yatachochea kwa kiasi kikubwa kasi ya ongezeko la uzalishaji kwa tija na
ubora.” alisema Chilumba.
No comments :
Post a Comment