
…………………………………………………………………………….
Na Karimu Meshack, Mvomero.
Mazungumzo ya amani ni muarobaini uliothibitika kutumika kama tiba ya migogoro ya ardhi Mvomero Mkoani Morogoro.
Hayo yamesemwa na
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Albinus Mgonya wakati akitoa taarifa ya
hali ya amani wilayani humo kwa Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na
Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliyofika walayani kwake hivi karibuni.
Wakulima na wafugaji
ni watanzania wanaoishi pamoja na kushirikiana katika shughuli
mbalimbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika maeneo wanaoishi na
zaidi, wengi wao ni wakulima na ni wafugaji kwa wakati mmoja hivyo njia
ya mazungumzo ya amani imejipambanua kuwa tiba ya utatuzi wa migogoro
inayowakabili.
“Unajua, hawa
wakulima na wafugaji wanafahamiana kwasababu wanaishi pamoja, matumizi
ya nguvu hususani vyombo vya ulinzi na usalama isingekuwa muarobaini,
badala yake kwa kuwakutanisha na kuzungumza nao kumeonesha kuwa ni
suluhisho la migogoro na ujenzi wa amani na utulivu baina yao.”
Kwa niaba ya wakulima
na wafugaji ndugu Moringe Kwinasei ameungana na Mkuu huyo wa Wilaya kwa
kuthibitisha hali ya uwepo wa utulivu na amani uliotokana na utatuzi wa
migogoro kwa njia ya mazungumzo ya amani na kuwataka wakulima na
wafugaji kuacha tabia ya uchochezi kwa kisingizio cha migogoro baina
yao.
“Unajua sisi ni ndugu
na wote tunahitajiana katika mambo mengi ikiwemo mazao ya mifugo na
mimea ambayo ndiyo yanatugombanisha, tunagombana shambani baadae tunakaa
hotelini tunakula wali-nyama! sasa kwanini tuendelee kugombania mambo
ambayo ni sehemu ya mahitaji yetu muhimu? Ameongeza kwa kuuliza Martine
Matingise.
Aidha, Mhe. Mgonya
amesema Wilaya yake imeanzisha programu ya michezo mbalimbali hasa
mashindano ya mipira wa Miguu kati ya Wakulima na wafugaji, mbinu hii
imeonesha kuwa na tija katika ujenzi wa amani katika Wilaya hiyo
kwasababu michezo imewaleta wakulima na wafugaji pamoja na kuishi kwa
upendo.
“Nimeanzisha na
kuhamisisha michezo mbalimbali hasa mpira wa Miguu kati ya wakulima na
wafugaji, na nimekuwa nikishiriki nao katika michezo husika. Kwakweli
njia hii pia imeonesha mafanikio makubwa katika jitihada za Serikali
katika ujenzi wa amani na kuzuia migogoro katika jamii.” Amemaliza Mhe.
Mgonya.
Kamati hii
imehitimisha ziara yake ya utekelezaji wa majukumu muhimu ya Ujenzi wa
Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari katika Wilaya ya Mvomero mkoani
Morogoro baada ya kufanya kazi kama hiyo katika Mikoa ya Arusha, Manyara
na Rukwa.
No comments :
Post a Comment