Katibu Mkuu Dkt. Leonard Akwilapo
akifungua maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya viongozi mbalimbali wa
Taasisi za Elimu walioshiriki katika maonesho ya 15 ya elimu ya Juu
Sayansi na Teknolojia wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wakati wa
ufunguzi wa maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja
Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akipata maelezo katika banda
la Chuo Kikuu Ardhi wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 15 ya Elimu ya
Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja
Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia wakipata maelezo katika banda la Chuo Kikuu Dodoma
Brass Band ikitumbuiza wakati wa
ufunguzi wa maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia
yanayofanyika Jijini Dar es Salaam
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo
Vikuu Charles Kihampa akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 15
ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya
Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam
……………………………………………………………
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo ametoa wito kwa Vyuo Vikuu
nchini kuhakikisha vinaanzisha programu za masomo zinazoendana na
vipaumbele vya kitaifa.
Dkt. Akwilapo ametoa wito huo
Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 15 ya Elimu ya
Juu, Sayansi na Teknolojia ambapo amesema kwa kuanzisha programu hizo
nchi itaongeza ujuzi wa wataalamu na pato la taifa.
Kiongozi huyo ametaja baadhi ya
programu za kipaumbele kuwa ni mafuta na gesi, afya, hususani udaktari
bingwa kwa ngazi za Uzamivu katika nyanja zote za magonjwa ya upasuaji
wa ubongo na mishipa ya fahamu, upandikizaji figo, ini na uboho (bone
marrow), tiba za ndani za moyo, na uhudumiaji wa wagonjwa wa dharura na
mahututi (emergency medicine and critical care).
“Tusingependa kama nchi kupeleka
wagonjwa wetu nchi za nje kutibiwa, bali nchi za nje waje kutafuta tiba
kwetu (medical tourism). Kwa kufanya hivyo tutaongeza ujuzi wa wataalamu
wetu pamoja na pato la taifa,” amesisitiza Dkt. Akwilapo.
Katibu Mkuu Akwilapo ameongeza
kuwa pamoja na kuanzisha programu za vipaumbele, nchi kwa sasa
inatekeleza miradi mingi mikubwa ambayo inahitaji wasomi wa kuendesha na
kusimamia miradi hiyo, hivyo ni jukumu la Taasisi za Elimu ya Juu
kuhakikisha hili linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kuhakikisha
wanatoa elimu bora na kwamba Serikali itaendelea kusomesha kwa wingi
wataalamu katika fani na ujuzi adimu na maalum kwa mahitaji ya nchi.
“Ni jambo la kutia moyo kuona
kwamba hivi sasa baadhi ya vyuo vikuu vimeanza kuelekeza jitihada zao
katika kutoa elimu ambayo inalenga kushughulikia changamoto za jamii na
kuweka msisitizo katika maeneo ya kimkakati ya nchi kama vile Kilimo,
Madini, Utalii, Uvuvi, Maliasili na Misitu na Afya,” amesema Dkt.
Akwilapo.
Katika hatua nyingine Dkt.
Akwilapo ameendelea kuzitaka Taasisi za Elimu ya Juu kuona namna bora ya
kupanua udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kutokana na ongezeko la
udahili wa wanafunzi katika ngazi ya msingi na sekondari na kwamba
wanapohitimu lazima wapate nafasi katika vyuo vya kati na vya juu ili
kuweza kuwapa ujuzi wa kujiajiri na hivyo kuchangia kikamilifu katika
ujenzi wa Taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi
ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini, Profesa Mayunga Nkunya amesema Tume
pamoja na mambo mengine imefanikiwa kuimarisha mfumo wa utoaji ithibati
ya mtaala, jambo ambalo lilionekana kuwa tatizo kwa muda mrefu na kwamba
itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia Watanzania katika
sekta ya elimu ili kuhakikisha Watanzania wa ngazi zote wanapata elimu
bora yenye kukidhi viwango vya ubora Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya
Vyuo Vikuu nchini, Profesa Charles Kihampa amesema lengo la maonesho
hayo ni kutoa fursa kwa vyuo vikuu kujitangaza na kuonesha huduma na
kazi wanazofanya pamoja na mchango wao katika ustawi wa elimu ya juu kwa
mustakabali wa maendeleo ya sayansi, teknolojia na manuufaa yake
kiuchumi na kijamii.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
wananchi waliotembelea maonesho hayo wamesema wamefurahishwa na kuwepo
kwa maonesho hayo kwani yanatoa fursa ya kuonana na wahusika na kupata
taarifa zinazowawezesha kuomba programu zinazoendana na ufaulu wao.
Jumla ya taasisi 67 za elimu ya juu zimeshiriki katika maonesho hayo.
No comments :
Post a Comment