Wednesday, September 30, 2020

FORUMCC ,UMOJA WA ULAYA WAFANYA USAFI WA MAZINGIRA FUKWE YA COCO BEACH JIJINI DAR


Na Mwandishi wetu

BALOZI wa Umoja wa Ulaya(EU) Manfredo Fanti amesema ni lazima elimu kuhusu ufihadhi wa mazingira iendelee kutolewa kwa jamii hasa inayoelezea madhara ya utupaji taka hatarishi maeneo ya fukwe za bahari kwani madhara yake ni makubwa, hivyo jamii iache kutupa taka hovyo katika maeneo hayo.

Ametoa kauli hiyo wakati wa tukio la kufanya usafi katika ufukwe wa Bahari ya Hindi eneo la Coco Beach jijini Dar es Salaam.Usafi huo umefanyika chini ya usimamizi wa Shirika la Forumcc kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya(EU) kupitia mradi wa mradi EU beach clean up.Pia vikundi vya vijana ambavyo vimejikita katika utunzaji wa mazingira navyo vimeshiriki kufanya usafi huo wa fukwe.

Balozi Fanti amesema kwamba uchafu katika fukwe ni hasa wa plastiki ni hatari kwa mazingira na kwa afya za binadamu kwani uchafuzi huo unakwenda kuharibu maisha ya viumbe hai wakiwemo samaki , ambao watu wanakula, hivyo kuna haja ya kuelimisha watu kutambua umuhimu wa kutunza mazingira yakiwemo ya bahari.

Kwa upande wake Balozi wa Poland nchini Tanzania Krzysztof Buzalski amesema uchafu ambao unawekwa au kutupwa ukiwemo wa plastiki ndio ambao baadae unakwenda kuliwa na samaki na hivyo kusababisha madhara kwa viumbe vya baharini na binadamu kwa ujumla.

Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati wa tukio hilo la kufanya usafi wa mazingira Coco Beach, Ofisa Mazingira wa halmashauri hiyo Albam Njaguso amesema kuna haja ya plastiki kukaa peke yake na taka zinazooza kukaa peke yake. 

"Plastiki inatakiwa kuwekwa eneo la peke yake na ya kuoza inakaa peke yake, plastiki inarudi kiwandani ili kutengenezwa plastiki nyingine na inayooza inaweza kutengeneza mbolea , inaweza kuzalisha gesi au malighafi nyingine ambazo zinatokana na taka ngumu na zile ambazo zinaoza,"amesema.

Amesisitiza usafi maeneo ya fukwe za bahari ni muhimu kwani unasaidia kuweka bahari katika mazingira safi. "Tungependa kila mwanajamii kuwa miongoni mwa wapenda usafi kwa kuhakikisha wanajituma kuondoa uchafu unaotokana mabadiliko ya tabianchi pamoja na ongezeko la joto duniani yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu, "amesema.

 

No comments :

Post a Comment