Sunday, September 20, 2020

BRELA yataja athari wanaotumia vishoka kusajili makampuni

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Makampuni na Majina ya Biashara wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mainrad Rweyemamu akizungumza na waandishi wa habari.

Na David John, TimesMajira,Online GEITa

KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Makampuni na Majina ya Biashara wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mainrad Rweyemamu, amewataka wananchi kuacha kutumia vishoka

pindi wanapofanya usajili wa kampuni, zao, kwani kufanya hivyo ni kujichelewesha wenyewe.

Amesema wao kama BRELA wanakutana na changamo wakati wa kufanya usajili kutokana na mtu anayesajili kampuni wakati mwingine kuwa sio mhusika, hivyo hulazimika kuchelewa kupata usajili wake wa kampuni au Alama ya jina la kampuni yake.

Rweyemamu ameyasema hayo jana mkoani Geita kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya Uwekezaji wa Madini ambayo yanaendelea mkoani hapa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.

“Tunawashauri wadau kuacha kutumia vishoka, kwani wakati mwingine watu hao wanaweka vizingiti kwa kuchelewesha mtu sahihi kupata usajili wake pale zinapohitajika nyaraka kwa wakati panajitokeza changamoto,”amesema.

Amesema na hata kwenye mawasiliano wao kama BRELA watawasiliana na mtu ambaye sio mhusika sahihi kwa sababu yeye ndiye anakuwa amekamata usukani, jambo ambalo hawakubaliani nalo na badala yake wanamtaka mhusika mwenyewe ili wawe wanawasiliana moja kwa moja kwa maana mwenye kampuni.

Mkurugenzi huyo amewataka wananchi hususani wafanyabiashara wote katika Kanda ya Ziwa kujitokeza kwenye viwanja vya maonesho ya madini mkoani Geita ili kupata fursa ya kusajili kampuni zao au majina ya kampuni.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Makampuni na Majina ya Biashara wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mainrad Rweyemamu, akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na madhara ya wananchi kutumia vishoka kusajili kampuni, mkoani Geita jana.

Amesema wao watakuwa mkoani hapa hadi Semptemba 27 kwa ajili kuhakikisha wanawapatia huduma wananchi na hivyo wahakikishe wanajitokeza kwa wingi.

Amefafanua kuwa majukumu yao makubwa wao kama BRELA ni pamoja na kufanya usajili wa kampuni, uandikishaji wa majina ya biashara ,usajili wa alama za biashara na huduma na kutoa leseni za viwanda vikubwa daraja A pamoja na kusajili Ubunifu.

Amesema hivi sasa kila kitu kinafanyika kwa mtandao, hivyo hakuna haja ya kubeba nyaraka mkononi kwa kuwa kila kitu kinamalizwa kwa mtandao tofauti na ilivyokuwa awali.

Hata hivyo amesema pamoja na kufanya mambo hayo yote wanatoa na ushauri na kazi yao kubwa ni kuwezesha watu kufanya biashara na si vinginevyo .

 

No comments :

Post a Comment