Saturday, August 15, 2020

WAZIRI HASUNGA ATANGAZA MSIMU WA MAUZO YA KOROSHO GHAFI MWAKA 2020/2021


Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga akisisitiza jambo kwa wakulima wa zao la Korosho Kijiji cha Tingi Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi wakati alipofanya ziara yake Kijini hapo. (Picha zote na Innocent Natai).

************************************

Na Innocent Natai, Lindi 

Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ametangaza rasmi  msimu wa mauzo ya korosho ghafi kwa

mwaka 2020 na 2021 ambao amesema kuwa Makadirio ya msimu wa uzalishaji kwa Mwaka 2020/2021 yanategemewa kuongezeka kutoka Tani 232,000 za msimu 2019/2020 hadi kufikia kiasi cha Tani 300,000

Akizungumza na Waandishi wa habari Leo Tarehe 15 Agosti 2020 mara baada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa wadau wa Korosho amesema kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu wa kutumia fursa ya kijografia ambapo Tanzania inapoingia kwenye msimu wa mauzo ya korosho nchi nyingi bado zinakuwa hazijaanza mavuno. Hivyo, kwa Msimu wa masoko na mauzo kwa mwaka 2020/2021 unatarajia kuanza tarehe 01 Septemba, 2020.

Aidha, amesema kuwa uzalishaji huo unatarajiwa kufikiwa endapo hali ya hewa itaruhusu sambamba na matumizi sahihi ya viuatilifu ikiwa ni pamoja na usimamizi thabiti wa mauzo ya korosho za wakulima kupitia mfumo rasmi wa stakabadhi ghalani.

Pia, amesema kuwa Bodi ya korosho kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali tayari imeandaa taratibu za usimamizi wa masoko na mauzo ya Korosho ghafi ambayo yanalenga kutoa majukumu kwa kila mdau katika usimamizi.

Aidha, taratibu zote na mgawanyo wa majukumu umezingatia maelekezo na maazimio ya Wadau kupitia mkutano mkuu wa Mwaka 2020 uliofanyika leo tarehe 15 Agosti, 2020 katika ukumbi wa Sea View Beach Resort, Mkoani Lindi.

Hasunga amesisitiza kuwa minada ya mauzo ya korosho itaanza mara tu baada ya korosho ghafi kuingia katika maghala ya minada na wanunuzi kukamilisha taratibu zote za kupata leseni ya ununuzi kutoka Bodi ya Korosho Tanzania. 

“Ni imani yangu kuwa kila mdau tayari amekamilisha maandalizi ya msimu kabla ya ununuzi kuanza” Amesisitiza Waziri Hasunga

Amewataka Wadau hao kuwa ni pamoja na; Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri za Wilaya, Wakulima, Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS), Vyama Vikuu vya Ushirika (UNION), Wakala wa Vipimo (WMA), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala, Waendesha maghala, Wasafirishaji, Wanunuzi, Mamlaka ya Bandari, na wengine wote ambao wanahusika kwa namna moja au nyingine.

No comments :

Post a Comment