Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia Kamati ya Maudhui imekifungia
kipindi cha Jahazi kinachorushwa na Clouds FM kuanzia leo tarehe 14
Agosti 2020 kutokana na kosa la kurusha maudhui yenye kuchochea kujichua
sehemu za siri na ngono.
Akizungumza na waandishi wa Habari Mwenyekiti wa Kamati hiyo Joseph
Mapunda amesema vyombo vya habari vinapaswa kuzingatia weledi na sheria
zilizowekwa kwa maslahi mapana ya ukuaji wa tasnia ya habari.
Katika hatua nyingine kamati hiyo imetoa onyo kali kwa baadhi ya vyombo
vya habari ikiwemo Kiss FM kwa kukiuka kanuni za utangazaji kwa kurusha
habari bila kuzingatia mizania ya habari kupitia kipindi cha Amka na BBC
wakati wakimhoji Makamu Mwenyekiti wa CHDEMA, Tundu Lissu kuhusu
wanachama wa chama hicho kuzuiwa kumuaga Hayati Rais Mstaafu, Benjamin
Mkapa.
Pia kituo cha Redio One kimepewa onyo kali kwa kukiuka kanuni ya
utangazaji kupitia Kipindi Amka na BBC kwa kurusha matangazo bila
kuzingatia mizani. Walimhoji Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu
akiituhumu serikali kuwazuia wanachama wa CHADEMA kumuaga Rais Mkapa.
Redio One walijitetea kuwa wana mkataba na BBC, na Redio One wanatakiwa
kupokea na kurusha vipindi vilivyoandaliwa na BBC kwa sababu BBC ipo
nchini kisheria.
Kamati ya Maudhui ya TCRA imesema Radio One wana usimamizi mbovu wa
vipindi cha nje na utetezi wao hauna mashiko kwa wao wanapaswa
kuzingatia sheria kwa chochote wanachorusha, na mkataba wao na BBC una
mapungufu.
Kamati imeshauri uongozi wa Redio One na vituo vingine vilivyokutwa na
makosa kuimarisha usimamizi wa maudhui, kupitia upya mikataba yao na
vyombo vya nje. Kituo hicho kimepewa onyo kali na kimewekwa chini ya
uangalizi kwa miezi mitatu.
Vituo vingine vilivyopewa onyo kali ni pamoja na Abood FM kwa Kufanya
uzembe wa kutangaza habari bila kuzingatia mizania, CG FM, huku Wasafi
Media Online TV wakipigwa faini ya milioni tano kwa kosa la kuhamasisha
ngono kupitia kipindi cha Women Matters.
Mamlaka ya Mawasiliano imetoa wito kwa vyombo vya habari kufuata kanuni
na taratibu zilizowekwa na mamlaka hiyo katika uendeashaji na usimamizi
wa vyombo vya habari.
No comments :
Post a Comment