Makamu
wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wakulima wa mazao
mbalimbali nchini kuongeza matumizi ya Mfumo wa Ushirika kwa kutumia
Stakabadhi za Ghala ili kupata uhakika wa masoko na bei zenye tija kwa
wakulima.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa akizindua Maadhimisho ya
Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima NaneNane, Kitaifa jana Agosti
01, 2020 katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.
Makamu wa Rais amesema kuwa ni muhimu wakulima kuuza mazao yao kupitia
vyama vya Ushirika nchini hususan maeneo ambayo tayari yana mifumo imara
ya Stakabadhi za Ghala. Aidha, ametoa wito kwa mikoa yote kujiandaa
vyema na matumizi ya mifumo ya Ushirika na Stakabadhi za Ghala ili
kupata bei zenye tija na zenye manufaa kwa wakulima.
“Tumeimarisha masoko ya mazao ya kilimo kupitia mfumo wa Stakabadhi za
Ghalani. Serikali imeimarisha mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa
kuhakikisha mazao yanauzwa kwa mfumo huo kupitia vyama vya ushirika ili
kuwapatia wakulima masoko ya uhakika na bei zenye tija,” alisisitiza
Makamu wa Rais
Akizungumzia kuhusu kauli mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu 2020, isemayo
“Kwa maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua viongozi Bora 2020”,
Mama Samia amesema kuwa inaendana na kipindi hiki ambacho tunaelekea
Uchaguzi Mkuu wa Viongozi mbalimbali nchini. Hivyo wananchi watumie
fursa hiyo kuchagua viongozi bora watakaoleta mapinduzi chanya katika
Sekta za Uchumi wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Wakati wa uchaguzi utakapofika tumieni fursa hiyo kuchagua viongozi
watakaoleta mapinduzi chanya kwa kusimamia Sera, uhakika wa masoko na
maslahi mapana ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na maendeleo ya Taifa,” alisema
Mhe. Samia.
Katika uzinduzi huo Waziri wa Kilimo, Mhe. Japhet Hasunga, alitaja
baadhi ya maeneo ambayo Serikali imeendelea kuweka msukumo wa maendeleo
ya kimkakati ni pamoja na usajili wa wakulima kwaajili ya upatikanaji wa
takwimu sahihi, kujua maeneo ya wakulima, mahitaji yao kwaajili ya
kuongeza ufanisi wa uzalishaji wa mazao. Sambamba na hilo Mheshimiwa
Hasunga amesema kuwa Serikali inafanya mapitio ya Sera ya Kilimo ya
mwaka 2003 kwa lengo la kuanzisha Sheria ya Kilimo, uzinduzi wa Bima ya
mazao, uimarishaji wa masoko ya mazao ya kilimo, uimarishaji wa mifumo
ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo sahihi kwa wakati.
No comments :
Post a Comment