Tuesday, August 4, 2020

BILIONEA LAIZER AIALIKA TENA SERIKALI MIRERANI


Ni baada ya kupata jiwe jingine kubwa lenye uzito wa zaidi ya kilo 6 
KWA mara nyingine tena Bilionea Saniniu Laizer ameifanya Serikali kufika Mirerani mkoani Manyara yaliko machimbo ya madini ya Tanzanite katika hafla ya kukabidhi jiwe lingine la Tanzanite lenye uzito wa kilo 6.3317 lililopatikana katikati ya mwezi Juni katika mgodi wake uliopo katika kitalu D ndani ya ukuta unaozunguka machimbo hayo katika eneo la Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
 
Jiwe hili ni la tatu kupatikana na kuuzwa Serikalini baada ya mawe mengine mawili kununuliwa na Serikali katika hafla iliyofanyika tarehe 24 Juni, 2020 mara baada ya mchimbaji huyo kuiarifu Serikali juu ya uwepo wa mawe mawili yenye uzito mkubwa yaliyochimbwa mgodini kwake mnamo tarehe 17 Juni, 2020 yaliyokuwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7.
 
Imeelezwa kwamba ndani ya muda mfupi baada ya Serikali kununua madini hayo kutoka kwa mchimbaji huyo mdogo, mchimbaji huyo alitoa taarifa ya kupatikana kwa jiwe jingine ambapo Serikali imeridhia kununua jiwe hilo na kuifanya Serikali kuwa na mawe matatu ya tanzanite yenye uzito mkubwa kwa uzito wa kufuatana ambapo zito zaidi lina kilo 9.27, kilo 6.33 na kilo 5.103.
 
Akizungumza katika hafla iliyofanyika leo tarehe 03 Agosti, 2020, Waziri wa Madini, Doto Biteko amewataka wachimbaji wadogo wa madini kuacha tabia ya kutorosha madini na kueleza kuwa tabia hiyo haina faida yeyote kwao na zaidi itawasababishia hasara kubwa na kupelekea kukamatwa na kushughulikiwa na vyombo vya dola.
 
Waziri Biteko aliendelea kubainisha kuwa, mnamo tarehe 17 Juni 2020 mgodi wa bilionea Laizer ulizalisha kilo 32.872 za Tanzanite katika umbali wa mita 1800 chini ya ardhi kwenye mgodi wake uliopo kitalu D uliokuwa na thamani ya shilingi bilioni 8.4 ambapo malipo ya mrabaha na ada ya ukaguzi yalikuwa ni shilingi milioni 507.5.
 
Akiendelea kuchambua uzalishaji huo, Waziri Biteko alisema ndani ya kilo hizo 32 ndipo yalipopatikana mawe mawili yaliyokuwa na uzito mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi ambapo kipande kimoja kilikuwa na uzito wa kilo 9.27 na kingine kikiwa na uzito wa kilo 5.103.
 
"Mnamo tarehe 29 Juni, 2020, Serikali iliarifiwa juu ya kupatikana kwa kipande kingine cha tanzanite chenye uzito wa kilo 6.33 kilichopatikana wakati wa zoezi la kusafisha eneo la uzalishaji wa awali yaani ule wa tarehe 17 Juni, 2020 ambapo wachimbaji walikuwa na zoezi la kuondoa miamba iliyokuwa ikikaribia kuanguka ili kuruhusu zoezi la uchorongaji na ulipuaji mwingine kuendelea," Biteko alifafanua.
 
Biteko alieleza kuwa, kwa mara nyingine Serikali imeridhia kununua kipande hicho kwa gharama ya shilingi 4,846,537,271.12 kufuatia uthaminishaji uliofanywa na wataalamu wa uthaminishaji madini ambapo shilingi 290,792,236.28 zimelipwa kama mrabaha na shilingi 48,465,372.71 zimelipwa kama ada ya ukaguzi.  
 
Akizungumzia faida za ukuta unaozunguka machimbo ya madini hayo ya Tanzanite, Waziri Biteko alisema taifa limeshuhudia kuongezeka kwa maduhuli ambapo ndani ya miaka miwili baada ya kujengwa kwa ukuta huo kiasi cha kilo 3,935.43 za tanzanite zenye thamani ya shilingi bilioni 53.141 zilizalishwa na Wizara kukusanya mrabaha wa shilingi bilioni 3.9.
 
Biteko aliendelea kusema kuwa Serikali imeridhia kununua kipande hicho kwa gharama ya shilingi bilioni 4.8 kufuatia uthaminishaji uliofanywa na wataalamu wa madini ambapo shilingi 290,792,236.28 imelipwa kama mrabaha na shilingi 48,465,372.71 imelipwa kama ada ya ukaguzi.
 
Akizungumzia kuhusu eneo la kitalu C, Waziri Biteko aliwataka wananchi wa Simanjiro na Tanzania kwa ujumla kutokuvamia eneo hilo kwani Serikali ina taratibu inazozifanya na zitakapokamilika taarifa itatolewa ili kuruhusu shughuli kufanyika sawasawa na maamuzi yatakayofanyika.
 
Aidha, aliuhakikishia umma kuwa kamwe eneo hilo halitatolewa kwa wageni ili liweze kunufaisha wazawa na taifa kwa ujumla. 
 
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kuwa Sekta ya Madini ni muhimu kwa uchumi wa nchi na kukiri kutambua kazi nzuri zinazofanywa na wachimbaji wa madini katika kukuza uchumi wa nchi.

 “Baada ya ujenzi wa ukuta mapato yatokanayo na uchimbaji wa Tanzanite yameongezeka mara nne,” Waziri Mpango alisema.
 
Aidha, Waziri Mpango ameipongeza kazi kubwa inayofanywa na  Rais John Magufuli kwa usimamizi madhubuti wa Sekta ya Madini na kuahidi kuendelea  kumwombea baraka za Mungu kwa mambo mazuri anayoifanyia nchi na wananchi wake.
 
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amempongeza, Rais Magufuli kwa namna anavyoisimamia sekta kwa kutoa maelekezo yanayopelekea mafanikio mazuri yanayoonekana kwenye sekta.
 
Pamoja na hayo Naibu Waziri Nyongo amempongeza mchimbaji Laizer kwa kupata jiwe jingine na kuwaahidi wachimbaji wadogo kuwa serikali yao itawapa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha wananufaika na rasilimali madini zilizopo nchini. 

No comments :

Post a Comment