…………………………………………………….
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Kwa mara ya kwanza wataalamu
wabobezi wa moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya
moyo wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamepandikiza kifaa cha kuusaidia moyo
kufanya kazi vizuri (Pacemaker) nje ya Taasisi hiyo bila ya kutumia
mtambo wa Cathlab.
Mgonjwa aliyewekewa pacemaker
alipata ajali iliyosababisha uti wa mgongo kupata shida na kusababisha
baadhi ya viungo vya mwili kupoteza uwezo wa kufanya kazi ikiwemo
mishipa ya damu inayoratibu uwezo wa moyo kutengeneza mapigo yake
(Sympathetic Waves System).
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaama daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete Yona Gandye alisema kutoka na tatizo alilolipata
mgonjwa mara baada ya kupata ajali mapigo ya moyo yalishuka hadi
kufikia 30 kwa dakika na mgonjwa kuonesha dalili za ukosefu wa
mahitaji muhimu ya mwili yanayosambazwa na mapigo ya moyo ambayo ni
oxygen , virutubisho, madini na chakula.
“Mgonjwa huyo alikuwa amelazwa
katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) na alihitaji huduma ya haraka
ya kuwekewa kifaa kisaidizi ambacho kinausaidia moyo kufanya kazi vizuri
(Pacemaker) ili mapigo yafikie 60 hadi 100 ambayo ni mapigo ya kawaida
ya moyo”.
“Kutokana na mazingira ya mgonjwa
kutoweza kuhamishika kutoka MOI na kuletwa JKCI ilibidi tumfuate
kumwekea Pacemaker. Tulitumia vyumba vya upasuaji vya kawaida kutumia
mashine tofauti na yetu ambayo yao inajulikana kwa jina la C-ARM”,
alisema Dkt. Gandye.
Dkt. Gandye alisema huduma hiyo
wameitoa kwa mara ya kwanza nje ya Taasisi hiyo na kuifanya bila ya
kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambao ni maabara
ya uchunguzi wa mishipa ya damu ya moyo na tiba
Alimalizia kwa kusema ushirikiano
wa JKCI na MOI na utayari wa JKCI kuhudumia wagonjwa nje ya Taasisi hiyo
ulisaidia kufanyika kwa huduma hiyo kwa haraka. Aliziomba Hospitali
kuwasiliana na JKCI kama watapata mgonjwa mwenye matatizo ya moyo
ambaye hawezi kuhamishika ili waone namna ambavyo wataweza kumsaidia
mgonjwa huyo kwa kumfuata mahali alipo.
No comments :
Post a Comment