Friday, July 3, 2020

UDSM WAGUNDUA KIFAA CHA KUTAMBUA MISHIPA YA DAMU KWA URAHISI


Kifaa cha kutambua mishipa ya damu kwa haraka (Low Cost View vein).
Meneja Mradi wa kifaa cha kutambua mishipa ya damu kwa haraka (Low Cost View vein), Fredrick Isingo akionesha kifaa cha kutambua mishipa ya damu kwa haraka.
Namna ambavyo kifaa hicho kinaonesha mishipa ya damu.

CHUO kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) chagundua kifaa cha kusaidia utambuzi wa mishipa ya damu wakati wa kuchoma sindano.

Kifaa hicho kinaweza kusaidia kutambua mishipa ya damu kwa watu wenye matatizo yaliyotokea kwa dharula na watu wanene sana pamoja na watoto wadogo.

Akizungumza na michuzi Blog Meneja Mradi wa kifaa cha kutambua mishipa ya damu kwa haraka (Low Cost View vein), Fredrick Isingo kwenye viwanja vya Julius Nyerere maarufu kama Sabasaba, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam leo,  amesema kwa kushirikiana chuo kikuu cha Dar es Salaam na Tume ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH) waliweza kugundua kifaa hicho ambacho ni mhimu zaidi kwa watu ambao wakiugua mishipa yao ya damu haionekani kwa urahisi na kumsaidia wauguzi kutambua ni sehemu gani wanaweza kumchoma sindano.
Isingo amesema kifaa hicho kinaweza kutumika sehemu yeyote kwani kinatumia nishati ya umeme hata wa jua.

"Kifaa hiki kinasaidia kuokoa maisha ya mtu ambaye akipata mshtuko, mwenye kiharusi na aliyeungua moto na watoto wadogo kwani mishipa ya damu hujificha, kifaa  hiki kinauwezo wa kutambua mshipa gani unaweza kuchoma sindano."
Aidha Isingo amesema kuwa kuna baadhi ya maradhi yanasababisha kutokuonekana kwa mishipa ya damu na kusababisha uchomaji wa sindano kuwa mgumu, kukosea na kusababisha maumivu kwa mgonjwa.

"Kifaa hiki kinajulikana kwa jina la Low Cost view Vein kimetengenezwa hapa nchini na watanzania wenyewe kinasaidia sana katika hospitali mbalimbali hapa nchini". 

Amesema kuwa kifaa hicho ni gharama nafuu na kinatumika kwa muda mrefu na endapo kikiharibika wanatoa huduma ya msaada ya kutengeneza  hapa nchini.

Amesema kuwa teknolojia ya kifaa hicho inamanufaa makubwa zaidi kwa watu waliokula chumvi nyingi pamoja na watoto wa dogo ambao mishipa yao ya damu haionekani kwa urahisi.

Hata hivyo ameomba wadau wa afya kutoa maoni yao na ushauri au maboresho ya kifaa hicho kupitia namba ya simu 0768000422 au Email fmisingo@jafrexsystems.com . 

Isingo amewashukuru Chuo kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia kwa kulikubali wazo lao la ubunifu wa kutengeneza kifaa hicho.

No comments :

Post a Comment