Thursday, July 9, 2020

NSSF YAENDELEA KUBORESHA HUDUMA KIDIJITALI ZAIDI


Mwanachama wa  Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Amos Erasto akionesha muonekano wa programu ya “NSSF TAARIFA” aliyopakua kwenye simu yake ya mkononi ambapo itamuwezesha kupata na kufuatilia taarifa zake zote za kiuanachama.

Na NSSF -Sabasaba

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeendelea kuboresha huduma zake kwa kuzisogeza karibu zaidi na wanachama wake kupitia
mifumo ya kidijitali.

Akizungumzia uboreshwaji uliofanyika alipokuwa akiwahudumia wanachama wa NSSF waliofika  katika maonesho ya 44 ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam katika banda namba 13 kwenye viwanja vya Julius Nyerere, Meneja Uandikishaji,Ukaguzi na Matekelezo NSSF Cosmas Sasi anasema NSSF imeboresha huduma zake zaidi na sasa wamekuwa na huduma za kidijitali ambapo mwanachama anaweza kupata huduma kupitia mtandao mahala popote pale alipo.

Maboresho haya yanampa mwanachama wa NSSF nafasi ya kupata huduma kwa njia ya WhatsApp, ujumbe wa maandishi kwenye simu, tovuti pamoja na programu ya simu maarufu kama “NSSF TAARIFA” ambapo mwanachama anaweza kuipakua na kuitumia katika simu ya kiganjani.

“Kwa sasa mwanachama haitaji kufika kwenye ofisi zetu, tumekuwa na huduma za kidijitali na kupitia simu yake ya mkononi anaweza kupata taarifa zake zote za uanachama,” Sasi anasisitiza.

Miongoni mwa huduma ambazo mwanachama anaweza kuzipata kupitia simu yake ya kiganjani ni pamoja na uwasilishwaji wa michango yake pamoja na salio lililopo kwenye akaunti yake.

Vilevile, maboresho hayo yanarahisisha uwasilishaji wa michango ya mwezi kwa mwajiri kwani michango inaweza kuwasilishwa kwa njia ya kieletroniki kupitia mfumo wa malipo ya kiserikali (GePG).

Meneja huyo ameongeza kuwa kwa kadiri siku zinavyokwenda, NSSF itaendelea kupiga hatua kuboresha mifumo na kuendelea kuwahudumia wanachama wake kwa ufanisi na urahisi zaidi.

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) linashiriki Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam Sabasaba Jijini Dar es Salaam, ambapo wataendelea kuwahudumia wanachama wake mpaka tarehe 13 mwezi huu wa Julai 2020.

No comments :

Post a Comment