Monday, July 13, 2020

NAIBU WAZIRI WA MADINI ATEMBELEA BANDA LA TUME YA MADINI MAONESHO YA SABASABA







Leo tarehe 13 Julai, 2020 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametembelea Banda la Tume ya Madini na Taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Saalaam.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho, amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imejipanga kuwawezesha wachimbaji wadogo ili wawe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini.

Akielezea mikakati ya Serikali katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakua zaidi amesema kuwa ni pamoja na kuhakikisha madini ghafi yanaongezewa thamani nchini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi hivyo kuongeza ajira kwa watanzania.

“Kama Serikali tunataka kuhakikisha kuanzia mchimbaji, mchenjuaji, mwongeza thamani hadi mfanyabiashara wa madini ananufaika pamoja na watoa huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini,” amesema Naibu Waziri Nyongo.

Katika hatua nyingine Nyongo amewataka wachimbaji wa madini kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.

No comments :

Post a Comment